WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, April 11, 2014

BUNGE LA KATIBA:Mapambano makali

  Shirikisho, Muungano vyawagawa wabunge
  David Kafulila amtetea Jaji Joseph Warioba

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, David Kafulila (katikati),akipongezwa na wajumbe wenzake, nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma jana baada ya kutoa hotuba ya maoni ya wachache kwenye kamati namba tano ya Bunge hilo na kuwakuna wapinzani wengi. Picha/Khalfan Said
Muundo wa Muungano umeligawa Bunge Maalum la Katiba baada ya wajumbe wengi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakitetea serikali mbili, huku wachache wakiwamo wa upinzani na wawakilishi wa asasi na makundi maalum, wakisema maoni ya wananchi yaliyomo katika rasimu ya kuwapo serikali tatu yaheshimiwe.
Tofauti hizo zilionekana wakati kamati kadhaa zilipowasilisha taaarifa na mapendekezo yao bungeni jana baada ya kuchambua, kujadili na kupiga kura katika kamati 12 nje ya Bunge kuhusu sura ya kwanza na ya sita za Rasimu ya Katiba mpya.

Sura ya kwanza inahusu jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mipaka, alama, lugha na tunu za Taifa, wakati ya sita inahusu muundo wa Jamhuri ya Muungano.

Ibara ya 1 (1) ya Rasimu inasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi na shirikisho lenye mamlaka kamili, ambalo limetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, zilikuwa nchi huru.

Akiwasilisha maoni ya wengi ambao ni kutoka CCM, Mwenyekiti wa Kamati Namba 2, Shamsi Vuai Nahodha, alisema katika kamati ulizuka mjadala mkali kuhusu maana ya maneno: “Muungano na Shirikisho” na baada ya ufafanuzi kutolewa, wajumbe walifanya maamuzi katika ibara hiyo na wengi ambao hawakufikia theluthi mbili, walipendekeza shirikisho lifutwe kwa sababu tatu.

Sababu ya kwanza, hati ya makubaliano ya Muungano inazungumzia kuwapo kwa serikali mbili; yaani serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya  Zanzibar.Sababu ya pili, Hati ya Muungano haijafutwa wala kubadilishwa na ya tatu shirikisho la serikali tatu linalopendekezwa katika rasimu, litakuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kudhibiti ulinzi wa eneo la bahari ya Hindi lenye rasilimali nyingi, ambazo mataifa makubwa yanaziwania.

Alisema kutokana na sababu hizo, wajumbe walitaka yafanyike marekebisho isomeke kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi yenye mamlaka kamili, ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya hati ya makubaliano ya mwaka 1964, zilikuwa nchi huru. 

Kuhusu sura ya sita ya rasimu inayopendekeza kwamba, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na muundo wa shirikisho lenye serikali tatu, ambazo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika, Nahodha alisema wajumbe wengi walikubaliana kwamba, muundo wa serikali mbili kama ulivyoainishwa katika hati ya Muungano ndiyo msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema baada ya kupiga kura, theluthi mbili ya upande wa Tanzania Bara haikupatikana na kwamba, ingawa theluthi mbili haikupatikana, wajumbe wengi kutoka pande zote mbili wanapendekeza ibara hiyo ifanyiwe marekebisho na kusomeka kwamba, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hata  hivyo, Nahodha alipata wakati ngumu wakati wa kuwasilisha kutokana na wajumbe kutoka upinzani kusimama na wengine kupiga kelele kumlalamikia wakati akisoma maoni ya wajumbe wachache, wakidai kuwa alikuwa anaacha kwa makusudi baadhi ya maneno.

Miongoni mwa wajumbe waliosimama na kumlalamikia Nahodha ni Mchungaji Christopher Mtikila na Godbless Lema ingawa hawakupewa nafasi ya kuzungumza, hali iliyomlazimisha Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta, kuingilia kati na kutoa ufafanuzi kwamba, asingeweza kusoma taarifa nzima kutokana na kanuni kutaka zisizidi dakika 60.

WAJUMBE WACHACHE
 Wajumbe wachache katika taarifa yao iliyosomwa na Nahodha, walisema wanashangazwa na msingi na utashi wa wajumbe walio wengi kutaka kubadili kiini cha rasimu na hivyo kupoteza kabisa maudhui na utashi wa wananchi kuhusu upatikanaji wa katiba mpya.

“Kama tayari kundi la walio wengi wanaamini kuwa kwa wingi wao wanaweza kubadili rasimu wenye maoni ya wananchi kwa kusingizia kuwa wananchi waliotoa maoni walikuwa wachache, basi hapakuwa na sababu ya serikali kutumia mabilioni ya shilingi katika mchakato mzima wa upatikanaji wa Katiba mpya,” walisema wajumbe wachache katika taarifa hiyo na kuongeza:

“Kwa hiyo basi, kama maoni ya walio wengi ndani ya kamati ni kufanyia marekebisho madogo ya Katiba ya sasa, kulikuwa na haja gani ya kuwa na Bunge Maalumu la Katiba kwa wajibu, ambao ungeweza kufanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano pamoja na Baraza la Wawakilishi?”    

Walisema wameamua kulinda maoni ya wananchi kama yalivyowasilishwa na Tume ya ya Mabadiliko ya Katiba kwa gharama yoyote na kuyataja maeneo yaliyoleta utata kuwa ni utata wa uwapo na uhalali wa hati ya Muungano.
 
KAFULILA AIBUKA SHUJAA KUMTETEA JAJI WARIOBA
Wakati hayo yakijiri, Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, David Kafulila, aliibuka shujaa kwa wajumbe wa Bunge hilo wanaounga mkono muundo wa Muungano wa serikali tatu, baada ya kuwashambulia watu wanaomdhihaki aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, huku akipinga hoja za wanaotaka muundo wa serikali mbili akisema hazina mashiko.

Kafulila alisema hayo wakati akitoa ufafanuzi wa taarifa ya wachache kuhusiana na sura ya kwanza na ya sita ya Rasimu ya Katiba mpya bungeni jana.

Alitoa ufafanuzi huo baada ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati Namba Tano ya Bunge hilo, Assumpter Mshama, kusoma ndani ya Bunge zima ripoti ya mwenendo wa mjadala ulivyokuwa wakati kamati hiyo ilipokuwa ikichambua na kujadili sura hizo mbili.

Mshama pia alisoma maamuzi na mapendekezo yake, kwa utaratibu wa maoni ya waliowengi na ya waliowachache kabla ya kuanza kwa mjadala wa Bunge zima kuhusiana na sura hizo.

Kafulila, ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), alisema inashangaza kuona baadhi ya watu wasiokubaliana na muundo wa serikali tatu uliopendekezwa katika Rasimu ya Katiba mpya wakimshambulia kwa maneno makali na ya kumdhalilisha Jaji Warioba.

“Jaji Warioba katika nchi hii siyo wa level (kiwango) ya kutukanwa. Warioba amesimamia maoni ya wananchi, ikiwamo ya Ofisi ya Rais. Haiwezekani leo. Serikali tatu ni mahitaji ya wakati,” alisema Kafulila.

Alisema muundo wa serikali tatu siyo hoja ya Jaji Warioba, bali ni wananchi waliotoa maoni na hata tume zilizowahi kuundwa miaka ya nyuma zilipendekeza muundo huo zikisema kuwa ndiyo unaofaa zaidi.

“Hii ndiyo ya fursa sasa ya kuweka muundo wa serikali tatu, kwani ni mahitaji ya wananchi. Hii haiwezi kuepukwa. Zisipopatikana sasa, zitakuja kupatikana kwa nguvu siku zijazo,” alisema Kafulila.

Aliongeza: “Kuna watu wanasema hatuwezi kubadilisha yaliyoanzishwa na waasisi wetu. Lakini Mwalimu Nyerere hakuwa Nabii. Alifanya mambo kutokana na wakati. Mwaka 1992 alianzisha mfumo wa vyama vingi baada ya kuona ni mahitaji ya wakati.”

Kuhusu hoja ya takwimu kuwa idadi ya wananchi waliotoa maoni yao ni ndogo, hivyo haiwezi kuwakilisha maoni ya wananchi zaidi ya milioni 40, Kafulila alisema haina msingi kwani haiwezekani kuchukuliwa maoni ya wananchi wote.

“Hoja kuwa watu 17,000 waliotoa maoni ya kutaka serikali tatu hawawakilishi maoni ya Watanzania milioni 45 haina mashiko. Hii ni sample tu. Haiwezekani kuchukuwa maoni ya wote. Kama mnaona idadi ya watu 17,000 ndiyo nyie 600 humu ndani mnapata uhalali gani wa kubadilisha maoni ya wananchi?” alihoji Kafulila.

Kuhusu hoja kuwa serikali ya Muungano haitakuwa na vyanzo vya kutosha vya mapato hivyo, kushindwa kujiendesha, Kafulila alipendekeza kuwa badala ya kutegemea kodi ya ushuru na michango ya serikali za nchi washirika, ushuru wa Bandari ya Dar es Salaam pia utumike kuhudumia serikali ya Muungano, kwani utaiwezesha kujiendesha bila kutegemea michango ya serikali washirika.

“Badala ya kutumia kodi ya ushuru na michango ya nchi washirika, utumike ushuru wa Bandari ya Dar es Salaam, ambao ni asilimia 40 ya Pato la Taifa sawa na zaidi ya Sh. trilioni 3.3 ambao ni zaidi ya Sh. trilioni tatu zinazokadiriwa kuendesha wizara za muungano,” alisema.

Aidha, madai kuwa Tanganyika itachangia zaidi gharama za kuendesha Serikali ya Muungano, alisema ina eneo kubwa na matumizi yake ni makubwa, hivyo ni lazima pia mchango wake uwe mkubwa, kwani hata kwa mfumo wa sasa inachangia zaidi kuliko Zanzibar.

Maelezo hayo ya Kafulila yalionekana kuwakonga nyoyo wajumbe wa Bunge hilo wanaounga mkono muundo wa serikali tatu, ambao walikuwa wakimshangilia mara kwa mara na kikao cha asubuhi cha Bunge kilipositishwa hadi mchana walipotoka nje ya ukumbi, walimbeba juu juu kumpongeza.

Awali, akitoa ufafanuzi wa maoni ya wachache ya Kamati Namba Mbili, Mjumbe wa Bunge hilo, Dk. Emmanuel Makaidi, alisema Tanganyika bado ipo, hivyo wanaunga mkono Rasimu ya Katiba, kwani serikali tatu haziepukiki.

Alisema hata waasisi wa Taifa, akiwamo Mwalimu Julius Nyerere walipigania Uhuru wa Tanganyika.

“Nawapongeza Zanzibar kwa kuchukua nchi yao. Watanganyika wamelala. Ndiyo maana mambo yanakwenda mzobemzobe,” alisema Makaidi na kupendekeza kwamba, wajumbe wabaki na msimamo wa maoni ya Tume ya Warioba.

Alisema maoni yaliyotolewa na Tume ya Warioba kuhusu serikali tatu hayana shaka, kwani yametokana na maoni ya wananchi wengi.

Alisema maoni hayo yanapaswa kuheshimiwa kwa sababu Warioba ni mwana CCM na ndiye anayemfahamu vizuri Mwalimu Nyerere.

Awali, akisoma maoni ya waliowengi, Mshama alisema wajumbe wengi wamependekeza muundo wa serikali mbili uendelee, kwani unadumisha mshikamano, kujenga uzalendo na unadumisha Muungano.

“Kama itaonekana kuna haja ya kuwapo muundo wa serikali tatu, basi kwanza inabidi Muungano uvunjwe halafu liundwe taifa la Tanganyika, ambalo litaungana na Zanzibar kuunda Muungano wa serikali tatu, jambo ambalo haliwekekani kwani linakwenda kinyume na mapendekezo ya Rasimu ya Katiba,” alisema Mshama.

Kuhusu maoni ya wachache, alisema wajumbe walipendekeza muundo wa serikali tatu kwa hoja kuwa unatokana na maoni ya wananchi na kwamba, utaondoa malalamiko ya pande zote mbili.

WAANZA KWA KULALAMIKIANA KUHUSU MUDA
Wakati jana ilikuwa ni siku ya kwanza ya kuwasilisha maoni ya kamati kuhusu sura ya kwanza na ya sita za rasimu ya katiba, ilianza na hofu baada ya wajumbe waliowengi kuanza kulalamika kuwa upande wa wajumbe wachache wenye maoni tofauti unapendelewa.

Kufuatia hofu hiyo, baadhi ya wajumbe wa kundi la waliowengi, akiwamo Dk. Zainabu Gama na Dk. Khamis Kigwangallah, waliomba muongozo wa Mwenyekiti kutaka kanuni ziangaliwe upya ili kuleta ulinganifu wa muda katika kuwasilisha ripoti hizo.

Dk. Gama (kundi la 201) akitumia kanuni ya 58 (3) (1), alisema inaruhusu kamati ya uongozi kuweka mambo vizuri inapoona hayaendi inavyopasa, hivyo akaomba mwongozo wa Mwenyekiti kurekebisha suala la muda na utaratibu wa kuwasilisha ripoti za kamati, maoni ya wachache na pia kutoa muda wa ufafanuzi.

Dk. Kigwangala (Nzega-CCM) alimtaka Mwenyekiti kutumia mamlaka yake anayopewa na kanuni namba 85(1&2) kutengua kanuni kwa kurejea ripoti za kamati zilizowasilishwa bungeni.

Akijibu maoni hayo, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, alisema utaratibu upo kwenye kanuni ya 31(1) inayoelekeza kuwa Mwenyekiti wa kila kamati au mjumbe mwingine atasoma kwa saa moja taarifa ya kamati.

Maoni hayo yanahusisha pia ya wajumbe wengi na maoni ya wachache kwa pamoja.

“Kwa hili kuna fursa, ambayo maoni ya wachache yameheshimiwa kwa sababu yanapata muda mrefu kuliko ya wengi. Dakika 40 kwa maoni ya wengi na 20 kwa maoni  ya wachache. Pia  dakika 30 tena anazopewa mjumbe wa maoni ya wachache kwa ufafanuzi wa maoni yao,” alisema Sitta.

Hivyo, alisema wachache wana dakika 50 na wengi wana dakika 40 na kwamba, kama imeonekama kuna upungufu, hiyo ndiyo nafasi ya kuwasilisha mapendekezo kwa kamati ya kanuni kuangalia zaidi.

Licha ya maelezo hayo suala la muda lilianza kuleta manung’uniko ndani na nje ya ukumbi wa Bunge. Walio wengi wakilalamikia kupunjwa na wachache wakitoka vifua mbele.

MAONI YA WAJUMBE

Wakizungumza na NIPASHE kuhusu hofu hiyo, Mjumbe Kangi Lugola, alisema kulalamikia utaratibu wa kusoma ripoti ya pamoja ya kamati yenye maoni ya wengi na kinzani kisha wachache kupewa muda wa kufafanua, ni hofu isiyo ya lazima.

Alisema kinachojiri bungeni ni kuibuka makundi mawili, la wengi linaloonekana kuwa ni la wanaCCM na la maoni ya wachache linalohusishwa na wapinzani.

“Hofu inajengeka upande wa wengi unaojihisi kuwa hauna muda, kama vile wachache na kuwa na hofu kuwa wanapendelewa wakati siyo hivyo ,” alisema Lugola.

Alisema kinachofanyika kilikubalika kwenye kuandaa kanuni na iliandaliwa, kwani  wachache, ambao pia ni sehemu ya wajumbe wa kamati walionekana kuwa badala ya kupewa muda wa kusoma taarifa zao kivyao, zichanganywe na kuzungumziwa na Mwenyekiti kwa pamoja.

“Maoni yao ni sehemu ya ripoti ya kamati, hivyo yanachanganywa, lakini kwa kuwa wana maoni tofauti wanapewa dakika 30 kufafanua hoja zao,” alisema Lugola.

Alionya kuwa awali, ilionekana kuwa waliowengi wamewashughulikia waliowachache, lakini leo Bunge linaanza kutekeleza kanuni iliyodaiwa kuwabana wachache hofu inaibuka.
“Suala hapa si wachache wala wengi. Ni hoja zenye mashiko zitakazoleta katiba bora.” alisema Lugola.

STEVEN WASSIRA

Mjumbe Stephen Wasira, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) aliungana na waliowengi kuwa wachache wanatumia muda mwingi zaidi, kwani wanakuwa na muda mrefu zaidi kuliko maoni ya kamati nzima.

Lakini akasisitiza kuwa: Hakuna haja ya kuwa na wasiwasi kwa kuwa ndivyo wanavyoingia kwenye utekelezaji wa kanuni na kujadili rasimu na shughuli za Bunge zinaendelea,” alisema Wasira.

Kuhusu kubadili kanuni, alisema wanaotaka zibadilishwe wapeleke mapendekezo kwenye kamati ya kanuni zitizamwe upya.

Akizungumzia hoja ya serikali tatu kutikisa Bunge, Wasira alisema hoja za muundo wa serikali na Muungano zisilete mashaka, kwani wote wana nafasi kueleza hoja zao na kuzitetea mwisho wa yote uamuzi utafanyika.

KUNDI LA WACHACHE
Walisema kinacholalamikiwa siyo muda, ila ni kupinga hoja ya wachache ya serikali tatu.

Walinukuu ripoti ya Tume ya Warioba iliyoeleza kuwa wataalamu wote na tume  zilizotangulia zimetaka serikali tatu, wao ni nani wazipinge, unaposema tatu zinavunja Muungano ni kwa vapi?

KHATIBU SAID HAJI

Mjumbe Khatib Said Haji alisema waliowengi wanaona wanabanwa, cha kushangaza walipitisha wenyewe kanuni kuwa maoni ya wengi yapewe dakika 40 na ya wachache yawasilishwe kwa dakika 20 na  dakika 30 za ufafanuzi kinachowauma ni nini?

“Ninachokiona ni ushindi  kwani jua limechomoza na dalili zimeonekana wazi. Watanzania wanahitaji serikali tatu na viongozi wa nchi walisema wanahitaji muundo huo wa serikali,” alisema na kuongeza kuwa suala siyo muda, bali waliowengi kushindwa.

NAOMI KAIHULA
Mjumbe Naomi Kaihula alisema hakuna haja ya kulalamikia kanuni, ambayo wakati wanaiandaa waliowachache walikataliwa kuwasilisha maoni yao.

“Wenye maoni kinzani walitaka kusoma hizo taarifa. Lakini waliowengi wakawakatalia, wakasema lazima iwekwe kwenye ripoti ya kamati na isomwe na Mwenyekiti, ambaye ni mjumbe kutoka CCM,” alisema Kaihula.

Alisema inashangaza kuona kuwa kile kilichoamuliwa na wengi dhidi ya wachache kinalalamikiwa wenye maoni kinzani wanapoleta maoni yao.
“Huu ndiyo ushindi, kwani tunachofanya ndicho kilichoko kwenye rasimu ya katiba tunayoijadili bungeni sasa,” alisema Kaihula.
FATMA FEREJI
Mjumbe Fatma Fereji alipinga kwamba, wachache wanapendelewa kwa kupewa dakika nyingi.

Alikumbusha kuwa kanuni ilikubali kuwa waliowachache watazibwa midomo na waliowengi na hivyo kupewa muda zaidi kufafanua hoja zao ni sahihi na hakuna la kulalamikiwa.

Alisema wachache wameanza kushinda kwani serikali tatu zipo japo zimejificha.

Katika hatua nyingine, wajumbe wanaowasilisha maoni ya wachache wameanika jinsi serikali zilivyoshiriki kuvunja hati za Muungano na kupinga dhana inayotolewa na wajumbe waliowengi kuwa kuunda serikali tatu ni kuvunja hati za Muungano.

Akifafanua hoja kinzani za Kamati Namba 9 yenye wajumbe  53, wakiwamo tisa wenye maoni ya wachache, Mjumbe Hezekiah Wenje, alisema: 

“Walio wengi wanapingana na mapendekezo yaliyoletwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa serikali tatu ni kuvunja Muungano, lakini hoja wanazowasilisha hazina ushahidi.”

Alisema walio wengi walidai kuwa na serikali ya shirikisho yenye serikali tatu itavunja Muungano na kuondoa umoja, mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Wajumbe hao pia walisema serikali ya shirikisho itaelea na haitakuwa na mapato, rasilimali na watu kwamba, kwa kutaka muundo huo, Tume ya Jaji Warioba imevunja Muungano na kukiuka hati za Muungano.

Akipangua hoja hizo, Wenje alianza na hoja ya kuvunja hati, alisema wa kwanza aliyevunja hati hizo tangu 1964 ni serikali ya  serikali mbili ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)  na ya Muungano.

Imeandaliwa na Theodatus Muchunguzi, Abdallah Bawazir na Gaudensia Mngumi, Dodoma
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment