WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, April 24, 2014

Hakuna atakayeshinda Katiba mpya, suluhu ni maridhiano

Na Gaudensia Mngumi


Niliwahi kuandika kuwa mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba katika mjadala wa Sura ya Kwanza na Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba hautakuwa mzuri kutokana na kuwapo kwa makundi yanayotofautiana kiitikadi.

Uwasilishaji wa ripoti bungeni kuhusu maoni ya kamati 12 zilizochambua, kujadili na kuamua kwa kura sura hizo kuhusu jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na muundo wa Muungano ndio ulioanza kuonyesha dalili kwamba mjadala bungeni ungezua mvutano mkubwa na mwishowe bunge hilo lishindwe kuzipitisha.

Uwasilishaji wa taarifa hizo uliwagawa wajumbe hao kiitikadi, kiasi kwamba kila upande ulikuwa unatetea upande wake kwa kuwa maoni ya kundi la walio wengi linaloongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwasilisha maoni ambayo yaliifumua kabisa rasimu kuhusu sura hizo na kuja na mapendekezo mapya huku kundi la walio wachache linaloongozwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), likitunga mkono mapendekezo ya Tume ya Warioba na kutaka yapitishwe kama yalivyo.

Hoja za kundi la wengi za kuibomoa na kuisuka upya rasimu hiyo katika sura ya kwanza na ya sita ni kwamba mosi, jina linalopendekezwa na tume kwamba ni shirikisho la nchi tatu siyo sahihi kwa kuwa hati ya Muungano inasema kuwa ni Muungano wan chi mbili.

Kundi hilo la wengi pia linakataa sura ya sita inayopendekeza muundo wa serikali tatu na kusema kwamba serikali tatu haziwezekani na kuonekana kwamba muundo wa sasa waliouacha waasisi wa serikali mbili uendelee.

Kimsingi, maoni na msimamo wa kundi la walio wengi wanaikataa rasimu katika suala zima la mapendekezo ya kutaka muungano ufanyiwe marekebisho kwa maana ya jina la Jamhuri ya Muungano na pamoja na muundo wa serikali tatu.

Hoja zao kuanzia katika maoni ya kamati ni kuwa serikali tatu zitakuwa na gharama kubwa ya kuziendesha na serikali ya Muungano haitakuwa na mapato ya kutosha na kubakia kuwa tegemezi na kwamba inaweza kushindwa kulipa mishahara ya wanajeshi na matokeo yake wakaipindua serikali.

Wanaendelea pia kujenga hoja kwamba serikali tatu zitaibua hisia za utaifa na kwamba matokeo yake ni kuhatarisha amani, umoja na mshikamano, hivyo Muungano utavunjika. Kundi hili linakuja na mapendekezo kwamba muundo utakaolinda Muungano ni wa serikali mbili zilizoboreshwa.

Kwamba pamoja na mambo mengine, Rais wa Zanzibar arejeshewe nafasi yake ya kuendelea kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, kuwapo kwa mabunge matatu kwa maana ya Baraza la Wawakilishi, Bunge la Tanzania Bara na Bunge la Muungano.

Yapo mapendekezo ambayo hayajawekwa wazi, lakini yanayoonekana kama kutaka kuwapoza Wazanzibari ambao wanalalamika kwamba Muungano unawadhulumu haki zao na kuwa Tanzania Bara imevaa koti la Muungano.

Baadhi ya ahadi hizo ni kuwa Zanzibar itaruhusiwa kukopa katika benki na taasisi za fedha nje ya nchi na kuwa itaruhusiwa kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC).

Ahadi hiyo inatumiwa na wajumbe wa CCM Zanzibar kushawishi kama njia ya kuponda hoja za wajumbe wa upinzani hususani Chama cha Wananchi (CUF), ambao wanasema kwa miaka 50 kero zao zimeshindwa kushughulikiwa na kwamba ahadi hizo hazitatekelezeka.

Wajumbe hao wa CCM wanatoa hoja hizo za kuwapa matumaini Wazanzibari baada ya kusikia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ya kulizindua Bunge hilo, aliposema kwamba mambo hayo yataangaliwa.

Hata hivyo, kuna ugumu wa kutekelezwa kwa ahadi hizo kwa kuwa kwa kuiruhusu Zanzibar iingie katika mikataba na mahusiano ya nje kitakuwa ni kitendo cha kuipa mamlaka kamili ambayo yanaweza kuipa nafasi ya kujitenga.

Kuiruhusu Zanzibar ikope nje na kujiunga na OIC kutakuwa ni uvunjaji wa makubaliano yaliyomo katika Hati ya Makubaliano ya Muungano ya Aprili, 22, 1964.

Ibara ya (iv) ya Makubaliano hayo inataja mambo ya Muungano kuwa ni katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Mambo ya Nje, Ulinzi, Polisi, Mamlaka ya dharura, uraia, uhamiaji, biashara ya nje na mikopo, utumishi katika Jamhuri ya Muungano, kodi ya mapato, ushuru wa forodha, bandari, anga, posta na simu.

Wajumbe wachache wanasema kwamba hakuna sababu ya kuhofia serikali tatu kwa kuwa zinaweza kuendeshwa bila tatizo kwa kuwa jambo la msingi ni serikali kuacha matumizi ya anasa pamoja na ufisadi.

Kundi hilo lilisema kwamba tatizo lililoko ni kwamba serikali inashindwa kukusanya kodi na kuacha mianya mingi ambayo ingeingiza mapato ya kutosha na kutolea mfano katika Bandari kwamba matrilioni ya Shilingi yanaweza kukusanywa.

Kundi hili linaponda hoja za wengi kuhusu uwezekano muungano kuvunjika iwapo zitaundwa serikali mbili kama ilivyotokea katika nchi kadhaa duniani kama Muungano wa Jamhuri za Kisovieti (USSR), Spain na Ujerumani, kwa kusema kwamba muungano wowote unaweza kuvunjika bila kujali ni wa serikali moja, mbili au tatu kwa kuwa la msingi ni kuwa na maslahi na wananchi wake.

Wanasema kwamba kubadili rasimu ni makosa kwa sababu mapendekezo yaliyomo yanatokana na maoni ya wananchi na wanahoji kuwa CCM wanapata wapi uhalali wa kubadili maoni ya wananchi na kwamba kama hawaiamini tume, basi waandae kura ya maoni ili wanancni waamue muundo wanaoutaka kasha Bunge lipitishe.

Kwa ujumla, hoja kinzani zilizotawala wakati wa uwasilishaji wa maoni ya kamati hizo ndizo zilizotawala wakati wa mjadala wa sura hizo ambao utaendelea hadi Ijumaa wiki hii wakati wa kuahirishwa kwa Bunge hilo ngwe ya kwanza kwa ajili ya kupisha Bunge la Bajeti.

Sitapenda kurudia kuhusiana na mambo yalivyokuwa wakati wa mjadala yakiwamo matusi ya nguoni, kashfa, vijembe, mipasho, lakini ukweli unabakia kwamba kuna mpasuko mkubwa katika bunge hilo.

UKAWA KUSUSIA
Itakumbukwa kwamba Jumatano iliyopita, wajumbe wa ukawa walitoka nje ya ukumbi wakati wa kikao cha jioni wakilalamikia mambo mbalimbali zikiwamo kauli za vitisho na ubaguzi kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.

Profesa Ibrahim Lipumba wakati wa kuchangia, alidai kuwa serikali imekuwa ikitoa vitisho ili wananchi waogope muundo wa serikali tatu na kutolea mfano hotuba ya Lukuvi aliyoitoa hivi karibuni katika Kanisa la Methodist mjini Dodoma wakati wa kumsimika, Askofu Joseph Bindara kwamba ilikuwa ya ubaguzi na vitisho.

Alisema kauli kwamba ikiwa zitaundwa serikali tatu, jeshi litachukua nchi na kuwa zikiundwa serikali hizo Zanzibar itakuwa nchi ya Kiislamu ni za vitisho na ubaguzi.
Lipumba alisema mwenendo wa katika Bunge hilo ni wa ubaguzi na baada ya hapo alisema wao (Ukawa) hawatapenda kuwa sehemu ya ubaguzi wa Bunge hilo aliloliita Interahamwe, yeye na wajumbe wa Ukawa waliamua kutoka nje kususia.

Kutoka kwa wajumbe hao licha ya kubezwa na wajumbe wa kundi la wengi, kulionekana kuliathiri kwa kuwa mijadala ilidorora kutokana na kuegemea upande mmoja ambao ulikuwa ukirudiarudia kauli na nyingi zikiwa ni za kuwalaani Ukawa.

MGAWANYIKO KUNDI LA 201
Wajumbe wengi wa kuteuliwa 201 wameonyesha kushindwa kusimamia misimamo yao, hali inayoonyesha kwamba wamegawanyika katika mchakato wa kuwatafutia Watanzania Katiba.

Sitawataja wote kwa majina wajumbe hao, lakini kimsingi, misimamo yao kuanzia uwasilishaji wa ripoti za kamati 12 na mjadala inatia mashaka.

Kwa mfano, Dk. Francis Michael, kutoka Taasisi za Elimu ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati Namba Tatu wakati wa kuwasilisha maoni ya kamati yake, alionyesha dhahiri kuegemea katika chama kimoja, lakini kibaya zaidi alikuwa akikataa kusoma maoni ya wachache kinyume na kanuni huku akitoa kauli za kuwaponda.

Hali hiyo ilisababisha mjumbe wa kundi la wachache, Mchungaji, Peter Msigwa kuponda kwa takwimu na kusahihisha baadhi ya taarifa alizozitoa msomi huyo ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Ezekiah Oluoch kutoka Vyama vya Wafanyakazi, wakati wa kuchangia alisema kwamba walimu wanataka serikali tatu na kutoa mifano ya maeneo aliyoyapitia na kupata maoni hayo kama Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT). Hata hivyo, mjumbe kutoka Shirikisho Huru la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), alisema kwamba msimamo wao ni serikali moja. Oluoch pia alitoka nje na Ukawa.

Asha Mtwangi, kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali, alisema kuwa msimamo wao ni wa serikali mbili, lakini akaonekana kuegemea chama kimoja kutokana na kuponda kauli za wapinzani.

Vile vile, Asha aliongozana na kundi la Tanzania Kwanza linaloongozwa na wajumbe wa CCM katika mkutano wa waandishi wa habari Alhamisi kuponda hatua ya wajumbe wa Ukawa kutoka nje ya bunge.

Mjumbe mmoja kutoka Zanzibar katika taasisi ambaye pia anatoka Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (Tamwa), licha ya Tamwa kupendekeza serikali tatu, lakini aliongozana na wajumbe wa Tanzania Kwanza katika mkutano huo.

Vile vile mgawanyiko huo unadhihirishwa na msimamo wa wajumbe 25 wa kundi hilo kutoka nje kususia bunge sambamba na wajumbe wa Ukawa.

Wapo baadhi ya wajumbe kutoka kundi la 201 waliozungumza na kueleza misimamo yao bila kuegemea upande wowote. Kwa mfano, Fahm pamoja na kuwa Mwenyekiti wa UPDP na kubaki ndani ya ukumbi, lakini alipochangia aliunga mkono serikali tatu na kueleza sababu zake bila kuponda upande wowote.

Lakinnaweza kusema kwamba mjumbe pekee ambaye alionyesha kuwa huru wakati wa kuchangia ni Profesa Bernadeta Kilian, ambaye hakutaja anataka muundo gani wa Muungano zaidi ya kutoa angalizo kwa wajumbe akionyesha hofu yake kwamba malumbano yatasababisha katiba ishindwe kupatikana.

Profesa Kilian alisema kwamba wajumbe wakiendelea na misimamo ya vyama bila kukubaliana, Katiba haitapatikana kinyume cha matarajio ya Watanzania na kwamba kinachotakiwa ni maridhiano kwanza.

Kwa vyovyote ilivyo, kanuni inayotaka maamuzi yote yafanyike baada ya kupatikana theluthi mbili ya wajumbe kutoka Bara na idadi kama hiyo kutoka Zanzibar haitaliruhusu kundi moja kuamua katiba.

Kuna uwezekano wa kupatikana kwa idadi hiyo kwa upande wa Bara, lakini ni vigumu kwa upande wa Zanzibar.

Kutokana na hali hiyo, itabidi maamuzi ya kupitisha sura hizo mbili na ibara zake yafanyike na kukubalina baada ya kufikiwa kwa maridhiano. Maridhiano hayo yanaweza kufanyika katika kipindi ambacho bunge hilo litakuwa katika mapumziko ya kusubiri Bunge la Bajeti kuanzia Ijumaa ijayo hadi Agosti.

Ni wakati mwafaka wa kuvishirikisha vyama vya siasa, viongozi wa dini na watu wanaoheshimika nchini, ambao hawaegemei katika itikadi za kisiasa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment