WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, April 24, 2014

Sitta:Katiba mpya itapatikana

Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba,Samuel Sitta.
Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, kwenda Zanzibar na kukutana na Rais Ali Mohamed Shein na Makamu wa Kwanza wa Rais ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, kutafuta mwafaka kufuatia wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia Bunge, amesema ana imani katiba mpya itapatikana.

Sitta alisema hayo bungeni jana, mara baada ya kusomwa dua ya kuliombea Bunge na kisha kuzungumza na wajumbe kabla ya kuanza mjadala kuhusiana na sura ya kwanza na ya sita ya Rasimu ya Katiba.

Bila kufafanua kauli yake wala kueleza katiba itapatikanaje, Sitta alisema pamoja na mambo yote yanayotokea bungeni, ana imani kuwa mwisho wa siku katiba mpya itapatikana.

“Kazi ya utungaji wa katiba inahitaji uvumilivu, hekima na busara, ninaamini kwa namna moja ama nyingine katiba mpya itatungwa,” alisema.

Aidha, Mjumbe wa Bunge hilo, Hamisi Dambaya, wakati akichangia mjadala huo, alimuomba Sitta kufanya jitihada kukutana na viongozi wa Ukawa ili kuwashawishi warudi bungeni kwa pamoja watengeneze katiba kwa njia ya maridhiano.

Dambaya alisema haitawezekana kutungwa katiba mpya ikiwa wajumbe wamegawanyika, huku wengine wakiwa nje ya Bunge.

“Bila ya maridhiano hakuna katiba mpya, kukimbia Bunge hakuna maana kwenda nje ya Bunge kutatengeneza mzozo wa kisiasa, tumekuja pamoja tuondoke pamoja, tukigawanyika tutawagawanya Watanzania … Mwenyekiti fanya jitihada wenzetu warudi bungeni tutengeneze katiba ndani ya Bunge,” alisema Dambaya.

Akijibu, Sitta alisema: “Kijana usiwe na wasiwasi. Kazi hiyo tumeshaianza. Jana (juzi), nilikuwa Zanzibar. Kwa hiyo, usiwe na wasiwasi.” Sitta hakueleza yaliyoazimiwa katika vikao alivyofanya Zanzibar na viongozi hao.

ALICHOTETA NA RAIS SHEIN
Hata hivyo, taarifa ya Ofisi ya Bunge ilieleza kwamba Sitta pamoja na mambo mengine, alimueleza Rais Shein jinsi wajumbe wa Ukawa walivyoondoka bungeni na alivyoshindwa kuwapata ili kujadili sababu zilizowatoa nje na kupata mwafaka.

SHEIKH THABITI NAYE ANA MATUMAINI
Mjumbe mwingine, ambaye ni kiongozi wa kidini, Sheikh Thabit Jongo, akichangia mjadala huo, naye alisema ana matumaini kuwa pamoja na mivutano inayotokea, katiba mpya itapatikana.

“Katiba bora itapatikana japo baadhi ya wajumbe wameondoka. Lakini huku kuna makundi mengine muhimu yamebaki. Kuna wanasiasa, kuna makundi ya wakulima, wafugaji, wavuvi. Kwa nini tusipate katiba mpya iliyo bora?” alihoji Sheikh Jongo.

Hata hivyo, Sheikh Jongo aliwasihi wajumbe wa Ukawa kurejea bungeni ili watetee mambo ambayo wanaona yanafaa kuwamo katika katiba mpya.

“Wametoa hoja wa serikali tatu lazima waitetee ili watushawishi kama kweli inafaa. Wakitoka nani watatetea hoja zao?” alihoji.

Aliongeza: “Kama kuna mambo hawaridhiki nayo kuna Kamati ya Maridhiano, mambo yote yaliyopelekwa kwenye kamati hii hakuna lililoharibika.”

OLUOCH AWASIHI UKAWA KURUDI BUNGENI
Mjumbe mwingine, Ezekiah Oluoch, aliwasihi wajumbe wote waliosusia Bunge kurudi ili kuendelea na kazi iliyowapeleka Dodoma ya kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata katiba wanayoitaka.

Pia aliwataka wajumbe wa Bunge hilo kutoka CCM kuchukua dhamana ya kuhakikisha kuwa nchi inapata katiba mpya ikiwa na umoja na mshikamano.

“Kwa mantiki hiyo, wasibweteke kuwa wanaweza kuwapa wananchi katiba wakiwa peke yao na wapambe wao bila ya wajumbe wa upinzani walioko nje ya Bunge Maalumu la Katiba,” alisema Oluoch katika mkutano wa waandishi wa habari.

Aidha, aliwataka wajumbe wa kundi la 201 waisotokana na vyama vya siasa na asasi zao kutoshabikia katika mjadala huo, bali wawe tayari kupatanisha pande mbili za wanasiasa wanaogombana katika mchakato huo.

“Kuunga mkono msimamo fulani haukatazwi, tatizo ni kuhusika moja kwa moja katika mivutano ya pande mbili ndani ya Bunge na kushiriki katika vikao vyao vya kuweka mikakati,” alisema.

WADAU WAONYESHA WASIWASI
Wakati Sitta na Sheikh Jongo, wakionyesha matumaini kuwa katiba mpya kupatikana, sheria ya mabadiliko ya katiba na kanuni za Bunge Maalumu la Katiba inataka vifungu vipitishwe kwa theluthi mbili ya wajumbe kutoka kila upande wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

Uwezekano huo haupo kwa sasa kama wajumbe wa Ukawa wataendelea kususia Bunge.

POLISI YASOGEZA MKUTANO WA UKAWA Z’BAR
Wakati huo huo, mkutano wa hadhara wa Ukawa uliokuwa ufanyike kesho Zanzibar umeahirishwa tena hadi Aprili 30, mwaka huu.

Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Abdul Kambaya, alisema Jeshi la Polisi Zanzibar limekubali kuwa mkutano huo ufanyike Jumatano ijayo bila ya maandamano.

“Tumeridhishwa na kauli ya Jeshi la Polisi kuwa mkutano tuufanye tarehe 30 katika viwanja vya Kibanda Maiti na tarehe 1 Mei tufanye kisiwani Pemba,” alisema Kambaya.
Alisema Ukawa wataendelea na msimamo wao wa kutorudi bungeni kutokana na CCM kuendelea na matusi katika Bunge hilo.

Kambya alisema kazi waliyopewa na wananchi ya kutetea rasimu ya katiba imekuwa ngumu kwao kwa sababu ya mikakati ya CCM kujadili rasimu ya chama chao na siyo ya wananchi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, alisema Ukawa wameruhusiwa kufanya mkutano wiki ijayo bila ya maandamano.

“Tumesitisha mkutano wa Ukawa uliokuwa ufanyike kesho (leo) kwa sababu Jeshi la Polisi lipo katika maandalizi ya kushiriki sherehe za miaka 50 ya Muungano zitakazofanyika Tanzania Bara,” alisema Kamanda Mkadam.

BAVICHA YAMJIA JUU MAKONDA

Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema (Bavicha) limesema hakuna kikundi chochote kinachoweza kujitwalia mamlaka ya kwenda kinyume au kupindua maoni ya wananchi kwenye Rasimu ya Katiba, ambao ndiyo wenye hati miliki na nchi yao.

Ofisa Utawala na Fedha wa Bavicha, Daniel Naftal, alisema wananchi wanafuatilia kwa makini namna watawala wanavyotaka kupoka na demokrasia kwenye jambo nyeti kwa manufaa ya CCM.

Kutokana na hilo, alisema Bavicha kwa kushirikiana na vijana wengine wenye machungu na Tanzania, watashawishi, kuratibu na kusimamia hoja za msingi katika kuhakikisha kizazi cha sasa na vingine vijavyo, vinanufaika na matunda yatakayoandaliwa sasa.

Alisema njama hizo zimeendelea kudhihirika baada ya CCM kupitia kwa kada wake, Paul Makonda, kutoa tamko la kuhamasisha vurugu na ‘kuanzisha’ vita, kwa nia ya kuwatisha wananchi washindwe kudai katiba yao inayotaka kupokwa na chama hicho.

Imeandikwa na Abdallah Bawazir na Jacqueline Massano (Dodoma) na Rahma Suleiman (Zanzibar).
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment