WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, April 10, 2014

Wabunge tangulizeni utaifa katika kujadili sura za katiba

Katuni
Wajumbe  wa Bunge Maalum la Katiba wanatarajia kuingia katika hatua nyingine muhimu kuanzia leo. Ni hatua ya kuwasilishwa na kisha kuanza kujadiliwa kwa sura za kwanza na sita za rasimu ya Katiba Mpya.
Baadhi ya wajumbe wameanza kuingiwa hofu, akiwamo Mwenyekiti wa Baraza la Vyama. Wanaamini kwamba hatua hii itakuwa ngumu kutokana na malumbano makali yanayotarajiwa kuibuka miongoni mwao, hasa wakati wa kuzungumzia vifungu vinavyohusiana na muundo wa muungano.

Sisi tunawatakia kheri wajumbe, tukiamini kwamba pamoja na kuwapo kwa hofu ya kuzuka kwa malumbano hayo, bado hatua hii itamalizika salama na mwishowe shughuli za kuendelea kupitia rasimu zitaendelea na kutimiza lengo la kuwapo kwa Bunge hilo.

NIPASHE tunatambua msingi wa kuwapo kwa hofu hii ya kuibuka kwa malumbano.

Ni kutokana na ukweli kuwa jambo hili haliepukiki. Kila anayefuatilia kwa karibu mchakato huu wa kuundwa kwa katiba mpya anatambua kwamba hakuna namna ya kupitishwa kirahisi kwa sura hizo mbili za rasimu ya katiba, hasa kwa kuzingatia kuwa wajumbe wana mitazamo tofauti juu ya masuala mengi yakiwamo ya idadi ya serikali katika muundo wa muungano.

Hata hivyo, pamoja na ukweli huo, NIPASHE tunaona kuwa ni vizuri wajumbe wa Bunge hili maalum wakatanguliza maslahi ya taifa dhidi ya kitu kingine chochote wakati wakiingia katika hatua hii.

Kwa kufanya hivyo, ndipo watakapotimiza lengo; ambalo ni kupitisha rasimu ambayo mwishowe itapelekwa kwa wananchi ili ipigiwe kura ya ndiyo au hapana.

Aidha, ni imani yetu kuwa wajumbe wote wa bunge hili wataifanya kazi waliyotumwa na Watanzania kwa umakini mkubwa ili hatimaye kuwa na rasimu itakayoungwa mkono na Watanzania walio wengi.

Kwa kuzingatia matumaini makubwa waliyo nayo Watanzania juu ya kupata katiba mpya, sisi tunaona kwamba ipo haja kwa wajumbe wote kutambua kuwa wanapaswa kuwa makini zaidi kwani safari ya kuelekea mafanikio itaendelezwa leo wakati watakapoanza kupitia sura hizo mbili zinazotajwa kuwa miongoni mwa maeneo nyeti ya rasimu.

Kama ikitokea wajumbe wakateleza kwa namna yoyote ile na mwishowe kutanguliza malumbano yasiyo na tija na kukosa mwisho mzuri, ni wazi kuwa mchakato mzima utakuwa shakani. Na gharama za kukwama kwa mchakato huo zitakuwa kubwa kwa Watanzania.

Mathalan, tunajua kuwa hakuna chochote chenye manufaa kwa taifa kitafanyika ndani ya Bunge hilo ikiwa wajumbe wataamua kutanguliza itikadi za vyama vyao dhidi ya maslahi ya Tanzania.
Taifa litakabiliwa na janga kubwa ikiwa wajumbe watapuuzia umuhimu wa kujenga hoja zao pasi na kujali mustakabali mwema wa nchi yao.
Hatari hii iko wazi. Kwamba, wajumbe wanapoamua kujenga hoja zao kwa kuzingatia utashi binafsi na maslahi ya vyama au makundi yao badala ya taifa, wanaweza kukosa uungwaji mkono wa kutosha kuhusiana na kile watakachokipigania. Mwishowe, theluthi mbili ya kura zinazohitajika ili kupitisha vifungu husika itakosekana.

Hivyo, tunawakumbusha wajumbe wote wa Bunge la Katiba kuwa Watanzania wengi hawapendi kuona mchakato mzima ukikwama kwa sababu ya malumbano yasiyokuwa na hoja zenye mashiko.

Tunakumbushia yote haya huku tukitambua kuwa si rahisi kwa kila upande, hasa ule unaopingana juu ya idadi ya serikali katika muundo wa muungano wataridhishwa na kila jambo. Bali, hekima, busara na uvumiliu ndivyo vitakavyowekwa mbele na kila mmoja kwa manufaa ya taifa.

Kila mjumbe atambue kuwa ili kufikia mwafaka, kuna baadhi ya mambo wanayoyataka sana yawemo kwenye rasimu ya katiba mpya yanaweza kukosa nafasi.
Hivyo, ni wajibu wao wakaendelea kushawishi wengine kwa hoja madhubuti na pia kupima uzito wa hoja mbadala kabla ya kutoa misimamo yao.
Hakika, kama wajumbe watakuwa makini katika hatua hii ya kuwasilishwa rasmi kwa sura za kwanza na pili za rasimu ya katiba, ni wazi kuwa watawatendea haki Watanzania.
Wataendelea kuwapa matumaini juu ya kutimia kwa ndoto za kuwa na katiba mpya kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho. Mungu ibariki Tanzania.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment