WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, January 29, 2013

Pinda, mawaziri wajichimbia Mtwara


NA WAANDISHI WETU

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ameendelea kujichumbia mkoani Mtwara sambamba na mawaziri watatu kwa ajili ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa gesi na vurugu zilizotokea wiki iliyopita.

Pinda aliwasili mkoani hapa juzi na kufanya vikao na viongozi wa vyama vya siasa kutafuta mwafaka wa mgogoro huo ambao unawahusisha wakazi wa mkoa huo na serikali.
 
Wakazi wa mkoa huo wanapinga kujengwa kwa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam hadi hapo serikali itakapowahakikishia jinsi gani watanufaika na nishati hiyo.

Jana, Pinda aliendelea kukutana na makundi mbalimbali katika ukumbi wa Veta kwa ajili ya kusikiliza maoni yao.

Waziri Mkuu kwa nyakati tofauti, alikutana na baadhi ya makundi hayo yakiwamo ya viongozi wa dini, wafanyabiashara, viongozi wa chama tawala, madiwani na wenyeviti wa mitaa.

Waziri Mkuu alitarajiwa kukutana na waandishi wa habari kueleza yaliyojiri katika mazungumzo hayo, lakini mkutano huo uliahirishwa jana jioni na wanahabari kuelezwa kuwa watapata fursa ya kusikiliza yaliyojadiliwa leo wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya Waziri Mkuu.

Hata hivyo, habari zilizopatikana kutoka katika vikao kati ya Waziri Mkuu na makundi hayo, zinaeleza kuwa makundi hayo yalimuomba Pinda mtambo ujengwe katika kijiji cha Madimba Wilaya ya Mtwara Vijijini.

Mtoa taarifa kutoka katika kikao kati yake na viongozi wa vyama vya siasa alisema Pinda aliwaahidi viongozi hao kuwa atakuwa mshauri mwema kwa Rais kwa suala la gesi ili kuona jinsi ya kutatua na kuwanufaisha watu wa Mtwara.

Habari zaidi zinasema kuwa Waziri Mkuu aliombwa kumuondoa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia, lakini aliwaeleza kuwa ombi hilo atalifanyia kazi.

Katika tukio lingine, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, wanatarajiwa kuwasili mjini hapa leo kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kwa wananchi wa Mtwara kuhusiana na utekelezaji wa mipango ya serikali.

Habari zinasema kuwa Dk. Mwakyembe, ataitumia ziara hiyo kueleza mpango wa ujenzi wa bandari ya Mtwara, ambayo ni miongoni mwa ahadi ambazo wakazi wa mkoa huo wanalalamikia kwamba serikali imeshindwa kuzitekeleza hivyo kupinga usafirishaji wa gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Kwa upande wa Dk. Magufuli, habari zinaeleza kuwa ataitumia ziara yake kueleza ukamilishaji wa ujenzi wa barabara kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.   Kabla ya mawaziri hao kwenda Mtwara, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliwasili Mtwara juzi kuangalia hali ya usalama kufuatia vurugu zilizotokea wilayani Masasi wiki iliyopita na kusababisha vifo vya watu wanne. Dk. Nchimbi alikwenda Masasi na kukutana na viongozi wa Jeshi la Polisi na hadi kufikia jana, hakutoa tamko lolote kuhusiana na vurugu hizo.

Aidha, serikali imetakiwa kuacha tabia ya kutafuta ufumbuzi baada ya kutokea maafa na badala yake imeshauriwa kuwa karibu na wananchi kwa kusikiliza kero zao ili kuliepusha Taifa dhidi ya vitendo vya  uvunjifu wa amani vilivyoanza kujitokeza mkoani Mtwara.

Wito huo ulitolewa jana na Katibu wa Umoja wa Vyama vya Siasa mkoani Mtwara, Said Issa Kulaga.

Kulaga  alisema serikali imeamua kufika Mtwara na kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa gesi baada ya  kutokea vurugu kubwa na maafa yaliyosababisha watu kupoteza maisha.

“Mimi kama mwananchi wa Mtwara na kiongozi wa CUF, kwa fikra zangu na mtazamo wangu, ujio huu wa Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya ndani mkoani hapa, ni matokeo ya vurugu na fujo zinazoendelea mjini hapa…naweza kusema kuwa serikali imeshinikizwa kuja kuzungumza na makundi mbalimbali ili kupata mwafaka wa gesi,” alisema.

Alisema katika mazungumzo kati ya viongozi  wa vyama vya siasa na Pinda juzi kuhusiana na  suala la gesi, yanaonyesha kuwa Waziri Mkuu anatofautiana na viongozi wengine wa juu kuhusiana na mradi mzima wa gesi.

“Waziri Mkuu anaonekana kutofautiana na viongozi wenzake kwani yeye anachokifahamu ni kuwa kutokana na uhaba wa umeme nchini, basi mradi wa gesi utasaidia kuzalisha umeme kwa wingi ili kunusuru viwanda vyetu vya ndani na uchumi kwa ujumla, ila cha kushangaza Waziri wa Nishati na Madini, yeye anasema serikali lazima ihamishe gesi na kupelekwa kwa watu wenye matumizi zaidi kwani huko wanakopeleka gesi ndiko kwenye kila kitu,” alisema. Hata hivyo, Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa CUF, Yassin Majaliwa, alisema ingawa Waziri Mkuu hakuja kwa ajili ya kutoa mwafaka wa gesi, alikuja kusikiliza ushauri wa viongozi mbalimbali ili wananchi na serikali wafikie maelewano.

Na kaatika hatua nyingine, Jeshi la Polisi wilayani Masasi, limelazimika kufyatua risasi tatu hewani baada ya kundi la vijana kutaka kuandamana kupinga kitendo cha polisi kumpiga dereva wa bodaboda. Polisi waliamua kutumia nguvu kwa kufyatua risasi hizo jana majira ya asubuhi baada ya madereva hao kutaka kuandamana kupinga kitendo cha askari kumpiga mwenzao juzi usiku.

Matumizi ya nguvu yalisababisha kundi la vijana hao kutawanyika, ingawa hakuna taarifa zozote kama kuna madereva waliokamatwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Maria Nzuri, alipotafutwa kutoa ufafanuzi kuhusiana na tukio hilo, alisema hakuwa na taarifa zozote.

MIILI YA WALIOUAWA YAZIKWA
Wakati huo huo, miili  ya watu wanne wa kiume waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi wilayani Masasi, imezikwa katika maeneo ya makaburi mbalimbali yaliyopo mjini Masasi.

 Maiti hizo ambazo mbili kati ya nne zimefahamika majina yao, zilizikwa juzi katika maeneo ya makaburi ya Masasi Mbovu, Nyasa na Upanga kati ya saa 4:00 asubuhi na 10:00 jioni.
 .
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment