WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, January 18, 2013

Gesi ya Mtwara sawa, maji ya Morogoro?

KAMA ilivyotarajiwa na wengi wetu, kwamba neema iliyonayo nchi yetu, ya kugundulika hazina kubwa ya mafuta na gesi asilia inaweza kuwa chanzo cha vita yetu wenyewe kwa wenyewe na mgawanyiko wa utaifa wetu kutokana na historia na uzoefu wa mataifa yenye hazina hizo duniani, ndivyo dalili za sasa zinavyoanza kujionyesha.

Ilianzia Zanzibar kwa baadhi ya Wazanzibari kutaka Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, uvunjwe kwa sababu tu ya kuwapo kwa dalili ya kuwapo hazina kubwa ya mafuta katika eneo la Zanzibar. Suala hili la hazina ya mafuta kuwapo Visiwani na kutaka umiliki wa maliasili hiyo ubakie mikononi mwa miliki ya Wazanzibari wenyewe, limekuwa likiibuka mara kwa mara na hadi sasa halijapatiwa suluhu.

Baadhi ya Watanzania wenzetu wa upande wa Zanzibar hawataki kusikia kabisa kitu kinachoitwa mafuta kikiwa kwenye orodha ya mambo yaliyomo ndani ya mamlaka ya Muungano. Wako tayari kuvunja Muungano, wako tayari kujitenga kwa sababu tu ya kugundulika kwa hazina ya mafuta, moja ya bidhaa muhimu sana kwa uchumi wa taifa lolote lile duniani.

Mikoa ya Lindi na Mtwara nako kumegunduliwa hazina kubwa ya gesi asilia katika maeneo ya Songosongo na Mnazi Bay. Huko nako mgogoro umeanza, na hasa baada ya Serikali kwa kutambua umuhimu wa gesi hiyo kwa uchumi wa nchi na maendeleo ya watu wake kwa ujumla wao, kuamua kwa makusudi kuwekeza mabilioni ya shilingi katika ujenzi wa mradi wa bomba kubwa la kusafirisha gesi itakayozalishwa katika maeneo hayo mawili na mengine ambayo uzalishaji wake haujaanza, hadi Kinyerezi, Dar es Salaam, ambako kunajengwa kituo kikubwa cha kusambazia gesi hiyo katika maeneo mbalimbali nchini yatakayohitaji matumizi hayo ya gesi.

Katika mgogoro huo uliopewa jina la ‘wananchi wa Mtwara’ ambao kila siku unazidi kuchochewa na baadhi ya wanasiasa wetu, baadhi ya wakazi wa Mtwara Mjini walijikusanya na kuandika mabango yenye ujumbe mbalimbali katika kile kilichoripotiwa na baadhi ya vyombo vyetu vya habari kwamba ni maandamano ya kupinga ‘gesi yao’ kusafirishwa hadi Dar es Salaam.

Rais Jakaya Kikwete, kama mkuu wa nchi na msimamizi mkuu wa rasilimali za nchi katika hotuba yake ya Salamu za Mwaka Mpya, alilizungumzia suala hili la gesi ya Mtwara na Lindi kama sehemu ya majibu yake kwa waandamanaji wale wa Mtwara na wote walioko nyuma yao.

Katika hotuba yake hiyo, kuhusu suala hilo la gesi ya Lindi na Mtwara alisema: “Rasilimali inayopatikana popote katika nchi hii, ni mali ya Taifa zima na hutumika kwa manufaa ya Taifa. Katu si mali ya watu wa pale (eneo) ilipogundulika au pale shughuli hizo zinafanyika...jumla ya makusanyo ya mapato yatokayo sehemu zote za nchi yetu na kutokana na vyanzo mbalimbali, ndiyo yanayotumika kuhudumia watu wote popote walipo.”

Siku mbili baada ya msimamo huo wa Rais Kikwete, Waziri mwenye dhamana na hazina hiyo ya rasilimali hiyo ya gesi, Profesa Sospeter Muhongo, aliwaita waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi ofisini kwake Dar es Salaam, kwa nia ya kutoa ufafanuzi juu ya madai hayo ya baadhi wananchi wa Lindi na Mtwara, lakini pia akaeleza maeneo mengine ya nchi yetu ambayo yana dalili ya kuwa na hazina kubwa ya gesi na mafuta.

Kwa kifupi, alichokifanya Profesa Muhongo, ilikuwa ni kutoa ufafanuzi kwa mapana zaidi kutokana na ukweli kwamba hotuba ya bosi wake, Rais Kikwete, ilikuwa na mambo mengi ya kitaifa ya kuzungumzia na kwa hiyo suala la gesi ya Lindi na Mtwara ambalo mjadala wake ulikuwa umepamba kila kona, akalizungumzia kwa ufupi tu akiamini kwamba anawaambia wananchi wake wenye uelewa juu ya nani mmiliki mkuu wa rasilimali zote za nchi hii.

Kilichofuata baada ya majibu na ufafanuzi huo wa Rais na Waziri Muhongo, ndicho kimenifanya nami nijiingize katika mjadala huu, ambao kimsingi kabisa haupaswi kuwapo wala kupoteza muda wa watu katika kuujadili.

Baadhi ya kauli zilizotolewa na baadhi ya wanasiasa wetu, baadhi ya wanaharakati na baadhi ya viongozi wa dini zetu kuhusu msimamo wa Serikali juu ya gesi ile ya Lindi na Mtwara kusafirishwa hadi Dar es Salaam, tena kauli zenyewe zikitolewa na watu ambao wanaheshimika sana ndani ya jamii kwa sababu ya weledi wao mpana wa masuala ya msingi, zinatia kinyaa, hazieleweki ni nini hasa malengo na agenda yao.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Sheria ya 1984, Na.15 (6), inayohusu ulinzi wa mali za umma, inatamka bayana kwamba kila mtu ana wajibu wa kulinda maliasili ya Jamhuri ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine. Watu wote watatakiwa na sheria (hii) kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu, na kuendesha uchumi wa Taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya Taifa lao.

Kwa hiyo, kwa mujibu wa kifungu hicho cha Katiba, kama Taifa, tunazo maliasili na mali za mamlaka ya nchi, ambazo ni mali ya Jamhuri ya Muungano na zote hizo zinamilikiwa kwa pamoja na wananchi wa nchi hii, na zinapaswa kulindwa na kila mwananchi. Lakini pia kwa mujibu wa kifungu hicho, kuna mali za mtu mmoja mmoja ambazo nazo zinapaswa kulindwa kwa mujibu wa Katiba yetu.

Ndiyo kusema kwamba rasilimali ya gesi ya Lindi na Mtwara, kama ilivyo rasilimali ya gesi na mafuta yanayopatikana na yatakayopatikana katika eneo lolote la mipaka ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, kwa mujibu wa sheria hiyo, na kwa mujibu wa Katiba yetu ya mwaka 1977, ni mali la Mamlaka ya Nchi, na mali yote hiyo inamilikiwa/itamilikiwa kwa pamoja na wananchi wa Jamhuri hii.

Binafsi, sitaki kuamini kwamba hao wanaosema kwamba wananchi wa Lindi na Mtwara wana ‘gesi yao,’ na hivyo lazima kwanza waombwe na Serikali na waridhie hivyo kabla ya gesi hiyo kufanywa chochote kile, ni mambumbumbu wa Katiba yetu. Wanaijua vizuri, wanajua ni nani mmiliki na mgawaji wa rasilimali za Taifa hili, lakini kutokana na malengo yao na agenda zao za kisiasa, wanajaribu tu kuiyumbisha Serikali ili ipoteze mwelekeo.

Kauli ya Rais Kikwete niliyoinukuu hapo juu, ya kwamba: “Rasilimali inayopatikana popote katika nchi hii, ni mali ya Taifa zima na hutumika kwa manufaa ya Taifa. Katu si mali ya watu wa pale (eneo) ilipogundulika au pale shughuli hizo zinafanyika,” hii si kauli ya Kikwete kama Kikwete mtoto wa Mzee Mrisho wa Ukwereni, Chalinze au Bagamoyo.

Ni kauli inayotokana na matakwa ya Katiba ya nchi ambayo aliapa kuilinda kwanza kabla ya kingine chochote kile mara tu baada ya Watanzania kumpatia ridhaa ya kuwaongoza. Kwamba rasilimali asili yoyote inayopatikana ndani ya ardhi ya Taifa hili, inamilikiwa kwa pamoja na wananchi wote wa Tanzania, kuanzia kona ya Mtwara, Pemba, Kilimanjaro, Kagera, Rukwa hadi Ruvuma.

Sasa inapotokea baadhi ya wanasiasa wetu, tena baadhi yao na vyama vyao vya siasa wakiwa na ndoto za siku moja kuwa watawala wa nchi hii, wakazungumza na kulishupalia jambo ambalo mwongozo wake unapatikana ndani ya Katiba, kwa kutumia hisia zao za kisiasa, tutarajie nini pindi watakapokuwa wameingia Ikulu kwa bahati njema au mbaya?

Gesi ya Lindi na Mtwara ni mali ya Watanzania wote, kila Mtanzania anayo haki ya kufaidika na rasilimali hii. Iliwekwa katika ardhi iliyo ndani ya mipaka ya nchi yetu na Mwenyezi Mungu wetu, tena wakati Mungu anaiweka hazina hiyo mahali hapo, hakuna kitu kilichokuwa kinaitwa Mtwara, Lindi wala Tanganyika au Tanzania. Aliweka ndani ya ardhi yake aliyoiumba, sisi binadamu ndio tuliotoa majina hayo ya maeneo katika msingi mkuu wa kujitambulisha na kujitofautisha. Kama kuna mkazi yeyote wa Mtwara ambaye babu yake, kwa jasho lake aliiweka gesi ile ardhini, aseme ili Watanzania, kupitia Serikali yao wamlipe fidia!
Hoja kwamba mikoa ya Lindi na Mtwara ilikuwa ni kitovu cha vita ya ukombozi kusini mwa Afrika na kwa hiyo wanapaswa kufidiwa kwa kuachiwa gesi hiyo, ni hoja za kitoto na za upotoshaji mkubwa zinazotolewa na watoto wa kizazi cha baada ya vita hiyo ya ukombozi kusini mwa Afrika na ile ya Kagera iliyomtoa Nduli Idi Amini ndani ya Uganda. Vita ya ukombozi kusini mwa Afrika na ile ya Kagera haikupiganwa na wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara au wa Kagera pekee. Ilipiganwa na Watanzania wote kwa ujumla wao.

Magunia ya maharage na mahindi kwa chakula cha wapiganaji hao yalitoka Rukwa, Mbeya, Iringa, Ruvuma na Arusha. Makundi ya ng’ombe na mbuzi kwa ajili ya kitoweo yalitoka mikoa ya Shinyanga na Mwanza na mikoa mingine ya wafugaji. Magunia ya dagaa yalitoka Kigoma na Mwanza. Kambi na makaburi ya Mazimbu walipozikwa wapigania uhuru kusini mwa Afrika, hayako Lindi na Mtwara, bali Morogoro. Kambi ya Jeshi ya 41KJ ya Nachingwea iliyotumiwa na wapigania uhuru kusini mwa Afrika, ni ardhi tu lakini chakula kilitoka nje ya mkoa huo!

Kilicho muhimu na sahihi hapa, ilikuwa ni kwa wanasiasa wetu hawa kuandaa mijadala kupitia semina na makongamano yenye lengo la, pamoja na mambo mengine kuishauri Serikali juu ya kuona umuhimu wa kuwapa kipaumbele wananchi wa Lindi na Mtwara katika mgawanyo huo wa rasilimali asili hiyo ya gesi, na lakini pia kuwapatia elimu ya kutosha wananchi wa Lindi na Mtwara na maeneo mengine yenye dalili ya kuwa na hazina ya rasilimali asili ni namna gani wanaweza kufaidika na rasilimali hizo.
Lakini kusema hapana, wananchi wa Lindi na Mtwara wana haki ya kuandamana kupinga ‘gesi yao’ isichimbwe na Serikali wala kusafirishwa kwenda nje ya mikoa hiyo kwa manufaa mapana ya Taifa hili, huko ni kuvunja Katiba ya sasa ya nchi yetu, na kwa kuwa mchakato wa kuandika Katiba Mpya uko uwanjani, basi ni muhimu kwa wanasiasa wetu hao kuelekeza nguvu zao katika kuhakikisha kwamba katiba mpya hiyo inamilikisha rasilimali za kila eneo kwa wananchi wa eneo husika, na kwa maana hiyo kuiondoa mamlaka ya umiliki wa pamoja wa rasilimali za Taifa hili.

Na ikiwa hivyo, basi wakazi wa Dar es Salaam, ambako pia ndiko yaliko makazi makuu ya wanasiasa na wanaharakati wetu, wajiandae kurudi makwao kwenye asili yao kwa sababu jiji la Dar es Salaam na mkoa wa Pwani utakaukiwa na maji na nishati ya umeme kwa kuwa maji ya Mto Ruvu wanayotumia kwenye mabomba yao, wenye nayo ni watu wa Milima ya Urugulu, umeme wa Gridi ya Taifa wanaotumia unatoka Kidatu na Mtera, kwa hiyo watu wa Morogoro na Dodoma nao tuwaruhusu wazuie maji yao na umeme wao kusafirishwa hadi Dar es Salaam

source: Raia Mwema Mayage S. Mayage

1 comment: