WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, January 27, 2013

Hii ni harufu mbaya tu, Ibilisi bado hajaenda msalani



BAADHI ya masuala ambayo nimekuwa nikiyajadili yanajitokeza hivi sasa kwa mshindo mkuu.
Nimekuwa nikisema kwamba tunajitahidi mno kujenga taifa dogo ndani ya nchi kubwa. Hili linadhihirika sasa. Nimekuwa nikisema pia kwamba tunaonekana kuwa na haraka ya kufanya mambo kama vile tunakwenda kwingine, hapa si kwetu na wala hatujafika. Hili nalo linajionyesha.
Hivi sasa tumetekwa na kelele zinazopigwa kuhusu gesi asilia inayochimbwa kusini mwa Tanzania, na tayari tumeanza kuona dalili za nchi kuparaganyika kutokana na ‘utajirihuo.
Tunachokishuhudia si mjadala wa jinsi gani tunaweza kunufaika kama taifa kutokana na gesi inayochimbwa nchini ( na pia utajiri mwingine unaotokana na rasilimali za nchi) bali ni ghadhabu za makundi hasimu yanayokinzana kuhusu namna ya kugawana kidogo tulicho nacho.
Kwa muda sasa, wataalamu duniani wamekuwa wakijadili kile kinachoitwa ‘resource curse’, au laana ya rasilimali. Hii ni laana ya nchi kama yetu ambazo zinajikuta zikiwa na rasilimali kubwa, lakini badala ya rasilimali hizo kuzinufaisha nchi hizo inageuka kuwa ni balaa, laaana. Hili ndilo linaelekea kutokea hapa nchini.
Bado hatujui kwa uhakika ni kiasi gani cha gesi asilia tulicho nacho. Nimesoma mahali kadhaa kwamba gesi hii ni nyingi mno na inaweza ikaifanya Tanzania kuwa mojawapo ya nchi zenye machimbo ya gesi makubwa duniani. Bila shaka hilo lingekuwa jambo jema kwa nchi inayoendeshwa kwa utaratibu unaoeleweka na inayojadili masuala muhimu kwa uwazi wa kutosha.
Kwa bahati mbaya, hii si kweli. Tumekuwa tukishuhudia usiri unaogubika mikataba juu ya rasilimali nyingine kwa muda mrefu sasa, na hakuna dalili kwamba tutaanza kesho au keshokutwa kuwa wawazi zaidi.
Hadi leo serikali inakataa kuanika hadharani maudhui ya mikataba inayoingia kwa niaba ya Watanzania, na serikali  ikiulizwa inajibu kwamba mikataba hiyo ni siri baina ya serikali na ‘ wawekezaji.’
Hii ni mantiki iliyopinda, kwa sababu rasilimali za nchi si mali ya serikali, ni mali ya wananchi na serikali inatakiwa ifanye kazi ya kuzisimamia kwa niaba ya wananchi wake, waliopo na watakaokuja baadaye.  Serikali kujifanya inaweza kutoa, kugawa, kuuza au kuhaulisha mali hizo bila wenye mali kujua nini kimefanyika kwa sababu ni siri kati ya serikali na ‘mwekezaji’ ni sawa na msimamizi wa shamba kumwambia tajiri wake kwamba ameuza ng’ombe wake lakini bei ya mauzo hayo ni siri kati ya bwana-shamba na mnunuzi. Uliona wapi jambo kama hilo ?
Jazba zimepanda, ghadhabu zinazidi kuumuka, kimsingi kwa sababu tunakabiliwa na nakisi ya imani. Wananchi wengi hawaiamini serikali yao kwa sababu wamezoea kuiona ikiwatendea kinyume cha haki, na mara kadhaa imedhihirisha udhaifu wake katika kusimamia rasilimali za nchi.
Iliwahi kutokea waziri mhusika wa sekta ya madini alitembelea machimbo ya dhahabu, akapitishwa sehemu kadhaa, lakini alipotaka kuingia chumba cha kuhifadhia dhahabu akazuiwa kwa sababu za ‘kiusalama.’ Ungedhani waziri angefoka, angelazimisha chumba hicho kifunguliwe au angejiuzulu. Mawe ! Alifyata mkia, akarudi Dar es Salaam kimya kimya, na akaendelea na kazi yake ya uwaziri bandia.
Wananchi wa kusini wameiona serikali yao inavyofyata mkia kwa ‘wawekezaji’ katika maeneoe mengine, na hawana imani kwamba itawatendea haki. Na wala matamshi ya wakuu wa serikali hayasaidii kutuliza hisia. Waziri anapowaambia wananchi wanompinga kwamba hawana elimu ya kuelewa nini kinaendelea, ni nani hasa anakuwa hana elimu, wananchi au waziri mwenyewe ?
Mkuu mwingine anaposema kwamba wapo watu wanaotaka kuingiza siasa katika masuala ya maendeleo, hajui kwamba masuala yote ya maendeleo ni masuala ya kisiasa?  Binafsi huwa najiuliza mara kwa mara, hivi hawa watu wamejifunza nini na wapi kuhusu siasa na uendeshaji wa nchi na uchumi wake ?
Zipo shutuma kwamba mradi wa kujenga bomba ni ‘dili’ ya watu fulani, na kwamba umebambikizwa gharama maradufu ili wajanja wapate mgawo wao. Sina uhakika kuhusu hilo, lakini siwezi kushangaa kama ni kweli kwani hivyo ndivyo tunavyoenenda. Wizi, ubadhirifu, utapeli, ulaghai, uchakachuaji, udhalimu na udanganyifu vimekuwa ni sehemu ya utamaduni wa utawala wetu, hadi nimesoma mahali ikipendekezwa kwamba mbinu hizi zingefundishwa shuleni. 
 Naangalia mbele tunakokwenda, na ninachokiona ni giza kwa sababu sioni umakini wa watawala wetu katika kuhimili  vishindo vya wakubwa wa dunia hii mbele ya utajiri mkubwa wa rasilimali kama gesi na mafuta ya peteroli. Wababe wa dunia wanaodhibiti biashara hii hawana huruma wala uvumilivu kwa vijinchi vyetu vinavyoendeshwa kama NGO.
Hata pale wanapopambana na miamba wanaotetea maslahi ya mataifa yao, wababe hawa hawasiti kuchukua hatua kali, ikiwa ni pamoja na kuondosha serikali inayowapinga na kuweka ya kwao. Anayetaka kujua zaidi akasome kuhusu waziri mkuu wa Iran, Mohammad Mosaddegh na mchezo aliofanyiwa na the Seven Sisterskatika miaka ya 1950.
Inaelekea tunacheza mchezo wa hatari kwa kukabidhi masuala mazito kwa watu wepesi, lakini iko siku tutakuja kujuta na kusaga meno. Madhara yake ni makubwa na yanaweza yakazua zahma ambayo tuliamini kwamba sisi, kama Watanzania, tumejijengea kinga dhidi yake.
Katika miaka ya 1970 waziri wa mafuta wa Venezuela, Perez Alfonso,  aliwahi kusema kwamba mafuta ya pateroli ni « Kinyesi cha Shetani »  na ni ukweli ulio wazi tukiangalia nchi kama Nigeria, Kongo-Brazza, Gabon, Angola na Guinea ya Ikweta, nchi zenye mafuta mengi lakini watu wake ni masikini hohe hahe na migogoro haiishi.
Hapa kwetu tumeanza kushikana mashati kabla hata Shetani hajaenda msalani. tumesikia harufu kidogo ya ushuzi wake tunatafutana. Akisha kwenda haja kubwa itakuwaje ?
Source: Jenerali Ulimwengu

No comments:

Post a Comment