WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, January 28, 2013


Gesi yetu na ya kujifunza kutoka Norway

 

ZAMANI sana kule Kilwa, Mwarabu aligundua kisiwa cha kuvutia sana; Kilwa Kisiwani. Akakitamani, na kwa hila, akamdanganya mtawala wa Kilwa akiuze kisiwa hicho kwa thamani ya shuka iliyokuwa  na urefu wa kutosha kuzunguka kisiwa chote!
Mtawala wa Kilwa akaona ni kitu cha thamani sana. Akakiuza kisiwa cha wananchi. Na katika Tanzania ya sasa wanaoitwa wawekezaji wakati mwingine hawatofautiani sana na Mwarabu yule aliyenunua kisiwa kizima kwa shuka tu.
Mikataba ya hila wanayoingia na tuliowapa dhamana za uongozi inaweza kuwa kujengewa nyumba ya fahari, gari la fahari na watoto kusomeshwa Ulaya na Marekani. Hayo tu yanaweza kutosha kumfanya Mtanzania kusaini mkataba wa mwekezaji kuvuna gesi yetu kwa miaka 25.
Kule Norway walipogundua gesi yao hawakuwa na wataalamu wa kuvuna gesi. Lakini, walihakikisha, wawekezaji waliokuja walipewa masharti magumu ikiwamo mikataba mifupi na kuhakikisha kampuni ya kigeni inaajiri raia wa Norway kwa idadi ya kuridhisha hata kwenye nafasi za uongozi wa kampuni za gesi, si vibarua tu.
Kwa mantiki hiyo, WaNorway wale walilenga, kuwa baada ya miaka 15 tu, wawe na watalaamu wao wenyewe na waanzishe makampuni yao ya kuvuna gesi na mafuta. Na leo Norway ina kampuni kubwa ya gesi na mafuta inayofahamika kimataifa, inaitwa StatsOil, imefika mpaka Kilwa, kuvuna gesi yetu. Wanatulipa nini? Ndipo hapa unakutana na ulimbukeni wetu.
Na gesi hii ya Mtwara na Lindi haitakuwa na zaidi ya miaka 100 kabla haijaisha. Juzi hapa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene kaweka wazi akiwa Arusha, kuwa hazina ya kiwango cha gesi kilicho katika miliki ya Tanzania ni asilimi 15 tu. Asilimia nyingine 85 ya gesi iliyogunduliwa iko mwambao wa bahari ya Hindi kwenye Pwani ya Tanzania, lakini, kwenye eneo la Kimataifa. Hivyo, Tanzania kama nchi haina hati miliki ya eneo hilo la bahari. Makampuni ya kigeni yana ruhusa ya kutafiti na kuanza kuvuna, kutengeneza faida na bila kuinufaisha Tanzania.
Naam, Tanzania si nchi ya kwanza kugundulika gesi katika dunia hii. Lakini, kwa ulimbukeni wetu, tuko katika hatari ya kuipoteza nafasi muhimu kabisa ya kutumia rasilimali yetu kwa manufaa ya wengi katika jamii. Tutaendelea kulumbana na kubaki masikini.
Na siku zote, historia ni mwalimu mzuri, lakini, bahati mbaya kabisa, wanadamu tumekuwa wavivu sana kujifunza kutokana na historia.
Leo tumeingia kwenye malumbano ya gesi bila wengi wetu kuwa na ufahamu wa nini hasa kinaendelea. Hakuna elimu ya kutosha iliyotolewa juu ya gesi yetu.
Leo Kampuni ya Statoil kutoka Norway ikishirikiana na Exxon Mobil imegundua gesi katika Visiwa vya Zafaran na Lavan vilivyopo Kitalu 2, Ukanda wa Pwani ya Tanzania, hususan Pwani ya Kilwa.
Mradi huo una gharama kubwa pia utafanywa na wageni ambao wana utalaamu wa miaka mingi katika biashara ya gesi duniani. Lakini, mikataba inasemaje? Na sisi watatuachia nini inapohusu utalaamu?
Haitoshi tu kutarajia wageni hao watujengee Hospitali ya kiwango cha Appolo na halafu tuwe tumeridhika. Ni yale yale ya mtawala na kipande cha shuka. Kwanza hao wakubwa wanaotibiwa Hospitali ya Appolo Kilwa watakwenda kufanya nini?
 Na tukumbushane pia juu ya kashfa ya gesi ya Songosongo kule Kilwa,  imeishia wapi?
Ikumbukwe,  kampuni ya  Pan African Energy iliyosajiliwa kwenye visiwa viwili; Mauritius na Jersey inaendelea kuvuna gesi ya Songosongo nchini Tanzania huku ikiwa imeingia mkataba wa miaka 25 na TANESCO kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli , TPDC.
Ni mkataba  wenye kuifanya kampuni hiyo kutokulipa kodi ya faida ya mapato wanayopata kutokana na mauzo ya umeme unaotokana na gesi asilia wanayovuna Songo Songo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Action Aid iliyotolewa mwezi Mei mwaka juzi, tangu Pan African Energy waanze kuvuna gesi asilia kule Songo Songo mwaka 2004, kampuni hiyo imevuna faida ya zaidi ya dola za Kimarekani milioni 60. Nusu ya faida hiyo ilipatikana mwaka 2009 na kampuni hiyo ilitarajiwa kuongeza uzalishaji. Hivyo, kuvuna zaidi gesi yetu asilia ya Songosongo.
Mpaka kufikia mwaka juzi, Pan African Energy imefanikiwa kukwepa kodi inayokadiriwa kufikia dola za Kimarekani  milioni 10. Hiki ni kiasi cha fedha kinachotosha kusomesha watoto wa Kitanzania 175,000 ( Laki moja na sabini na tano elfu) kwa mwaka kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Action Aid la nchini Sweden.
Na tujiulize, je, wananchi wa Kilwa na Watanzania kwa ujumla tunataka kujengewa hospitali ya kiwango cha Appolo au tunataka wawekezaji tuingie nao mikataba ya haki na yenye maslahi ya muda mrefu kwa Taifa na yenye kuhakikisha inatuingizia kodi ya kutosha kutujengea uwezo wa kuijenga nchi yetu wenyewe.
Na hakika, maswali ni mengi, lakini, hayo machache  yanatutaka tukae chini kama Taifa na kujadili kwa uwazi suala la rasilimali zetu na usimamizi wake kwa manufaa ya kizazi kilichopo na vijavyo. Nahitimisha.
Source: Raia Mwema: Maggid Mjengwa

No comments:

Post a Comment