WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, January 22, 2013

Leo lazima iwe bora kuliko jana, na kesho kuliko leo, la sivyo kuna tatizo


MIONGONI mwa mambo mengi yanayodhihirisha msigano baina ya taifa dogo na taifa kubwa ni upeo wa mwangalio.
Taifa dogo litakuwa na watawala na wananchi ambao wote wanaangalia vitovu vyao; wakijitahidi sana wataona ncha za vidole vyao vya miguu. Taifa kubwa litakuwa na watawala, viongozi na wananchi wanaoangalia upeo wa macho; wanaangalia makutano ya mbingu na ardhi, kisha wanainua macho na kuangalia anga.
Taifa dogo litakuwa na watu wa kufanya mambo haraka haraka, huku wakilipua, alimradi watimize ngwe. Mipango yao ni ya muda mfupi; wanachopanda ni kile watakachokula ndani ya wiki tatu, kwa hiyo watapanda mchicha na bamia na baada ya wiki nane watakuwa hawana kitu.
Watawala na viongozi wa taifa kubwa watawahimiza na kuwafundisha watu wao (na watu wao wataelewa) kufanya mambo yao kwa mipango ya muda mrefu, mipango ya kimkakati; mazao yao yatakuwa ya kudumu na yaliyofanyiwa utafiti wa muda mrefu ili kuwa na uhakika wa tija katika mavuno. Mipango yao itakuwa ya kuangalia, si tu faida ya leo na kesho na kesho kutwa, bali faida watakazokuta watoto, wajukuu, vitukuu na vilembwe, hadi miaka milioni ijayo.
Tukiangalia mataifa ya Uropa, tunalazimika kukubali kwamba haya ni matafia makubwa, na pia tunakubali kwamba yamekuwa mataifa makubwa kwa muda mrefu, ingawaje yapo baadhi yake yaliyopungukiwa na ukubwa yaliyokuwa nao huko nyuma. Hatuna budi kuona haya kwa kuona ni nini walichofanya binadamu wenzetu na kukilinganisha na upuuzi tunaofanya sisi, kana kwamba sisi si binadamu kamili.
Tunaona kwamba mababu na mabibi zao waliweza kuwaza kwa masafa marefu na kujenga juu ya msingi wa mawazo hayo, na leo bado tunayaona matunda ya mawazo hayo kila tunaponagalia majumba yaliyodumu karne kadhaa na bado ni imara na kila tunapoangalia barabara pana na imara zilizojengwa karne zote hizo zilizopita na leo bado zimesimama imara.
Tunaangalia jinsi wanavyohangaika kuboresha huduma zao za elimu, afya na huduma nyingine za kijamii (ambazo tayari ni nzuri) wakati sisi tukiua hata zile tulizokuwa nazo.
Tunaposafiri Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia na kwingineko tunaona ushahidi wa mataifa makubwa yanavyofikiri, lakini kwa sababu tumejifunga katika udogo wetu mpendwa hatupati funzo lo lote linaloweza kutusaidia kufikiri kikubwa pindi tunaporejea nyumbani. Sana sana tutapoteza muda wetu na fedha kununua vijitakataka na upuuzi mtupu ili kuwakoga wenzetu, kama vile kununua masuti ghali ambayo wala hatujui yanavyovaliwa.
Taifa kubwa litakuwa na watawala na viongozi wanaotaka kuona maendeleo ya wakati wote, na ambao hawakubali kitu cha leo kiwe duni kuliko cha jana. Kwao, maendeleo ni ile hali inayotokea wakati kitu cha leo ni bora kuliko cha jana, na cha kesho kitakuwa bora kuliko cha leo. Daima mwendo ni kuelekea mbele.
Baba atakuwa na elimu bora kuliko babu, lakini mjukuu atakuwa na elimu bora kuliko baba. Baba atakuwa na siha ya kuridhisha kuliko babu, lakini afya ya mjukuu itakuwa ni bora kuliko ya baba; hata ukubwa na urefu wa kimwili unatakiwa uende ukiwa bora zaidi kwa kila kizazi kipya kijacho. Jamii inayozaa watoto wenye maumbile madogo kuliko wazazi wao ina tatizo.
Sisi, katika udogo wetu, tunaenenda vipi?
Katikati ya miaka ya 1970 serikali iliamua kujenga barabara ya njia nne kutoka Ubungo hadi Bandarini jijini Dar es Salaam. Hiyo ndiyo leo inaitwa Nelson Mandela, iliyotufungulia maeneo kama Riverside na Tabata.
Ndiyo hiyo pia barabara kuu inayohudumia bidhaa nyingi zinazosafirishwa kwenda hadi mipakani mwetu (zikisafirishwa kwenda Zambia, Kongo, Burundi, Rwanda na Uganda) hivyo ni kitegauchumi muhimu kwa nchi yetu.
Lakini miaka 30 baadaye tunachofanya ni kwenda kuiparura barabara ile ile kwa upana ule ule, na kuipaka rangi nyeusi, huku tukishuhudia jinsi msongamano wa magari unavyozidi kughasi, kukera na kusumbua. Huu ni udogo wa mawazo unautusmbua, ingawaje kila siku tunapata kauli za kujisifia kwa ujenzi wa ajabu tulioufanya.
Tumeliacha Jiji la Dar es Salaam lioze katika sehemu nyingi katikati kabisa ya jiji. Iko mitaa inayotia kinyaa ukipita, kwa sababu ujenzi unafanywa holela, takataka zimezagaa kila mahali, na maji yametuwana yakiwa yamechanganyika na kila aina ya uchafu wa kuchefua roho. Inaelekea, pamoja na maneno yote yaliyosemwa kuhusu tatizo hili, tumeshindwa kushughulikia suala la plastiki ambazo sasa zimezagaa kila mahali, zikichafua mazingira na kuumiza ardhi yetu.
Watawala na watu wanaoangalia mbali labda wangeamua kuvunja sehemu kubwa ya jiji hili na kulijenga upya. Wangetafuta pia namna ya kulifanya lipumue kwa kusambaza huduma zinazokimbiliwa katikati ya jiji na kuzipeleka katika viunga vya mji, ambavyo vingefikika kwa urahisi kwa kujenga barabara za upana wa mita hadi 60 na zaidi.
Hapana, sisi tunataka tubanane hapa hapa, katikati ya jiji hili chafu linalonuka maji-taka. Tumeendelea kuishi katika mazingira finyu, machafu na yaliyojaa ndwele kama vile kipindupindu hadi sasa tunaelekea kukubali kwamba hivyo ndivyo tunavyotakiwa kuishi.
Rai yangu hapa ni kwamba udogo tulionao ni udogo wa kujivisha sisi wenyewe, si udogo wa kupewa na Mungu. Mataifa yaliyodhihirisha ukubwa, kadhalika, hayakuvishwa na Mungu bali yalijivisha ukubwa huo yenyewe, kwa kufikiri kikubwa na kutenda kikubwa.
Ukubwa unaohitajika ili tuondokane na udhalili huu tunao ndani yetu; tunachotakiwa kufanya ni kuutafuta, kuubaini, kuuibua na kuutumia ili na sisi tuweze kutamba mbele ya mataifa mengine kama taifa kubwa.
Niseme ukweli: Inaudhi kuendelea kuwa mdogo wakati ukijua kwamba uwezo wa kuwa mkubwa unao ila hujui namna ya kuutambua na kuutumia.
source: Raia Mwema: Jenerali Ulimwengu 

No comments:

Post a Comment