WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, January 18, 2013

DC atangaza gesi imezua balaa Mtwara


NA WAANDISHI WETU

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Wilman Ndile

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Wilman Ndile, amesema suala la gesi kwa sasa ni tishio kubwa kwa amani na utulivu kwa wakazi wa Wilaya na Mkoa wa Mtwara.

Kutokana na hali hiyo, amewataka viongozi wa asasi mbalimbali mkoani hapa kutoa elimu kuhusu gesi asilia kwa wakazi wake ili kudumisha hali ya amani na utulivu, ambavyo vinaelekea kutoweka siku hadi siku.

Alitoa kauli hiyo alipokuwa akitoa hotuba yake fupi kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Mjini Mtwara.

Alisema kwa sasa hali ya Wilaya ya Mtwara kiusalama, kisiasa na kiuchumi siyo nzuri kutokana na suala la gesi, ambalo limekuwa gumzo kila kona ya mkoa na kutishia kutoweka kwa amani na usalama.

“Kwa kweli hali iliyopo hivi sasa Mtwara siyo nzuri kiusalama. Kwani inaweza kuhatarisha maisha ya Wanamtwara. Sijui tunakoelekea. Maana kila kona unakopita hakuna mazungumzo mengine zaidi ya gesi ikiambatana na kauli mbiu yao ya ‘gesi kwanza vyama baadaye’,” alisema Ndile na kuongeza:

“Hii ni mbaya na ni hatari, kwani suala hili linaweza kuleta madhara makubwa katika siku za usoni.”

Alisema ni lazima kutenga muda maalum kwa ajili ya kuwaelimisha watu ili wapate uelewa na kutambua manufaa yatakayotokana na rasilimali hiyo na kwamba bila kufanya hivyo, hali ya utulivu na usalama haiwezi kuwapo.

“Wanamtwara ni waelewa wazuri tu endapo wataelimishwa kwa lugha iliyokuwa nyepesi na 
elimu badala ya ubabe,” alisema Ndile.

Alisema ni lazima kufanya kila linalowezekana kutenga muda maalum wa kufanya mazungumzo kati ya viongozi na wananchi ili kuweka mambo sawa.

Hata hivyo, utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya masuala ya gesi utaanza mapema wiki ijayo kwa lengo la kurejesha hali ya amani na utulivu.

Pia alisema suluhisho la suala hilo lipo katika mikono ya serikali kwani cha msingi ni kupata suluhu ya tatizo hilo ili kuiondoa jamii mahali ilipo na kurudisha imani dhidi ya viongozi wao.

YALIANZA MAANDAMANO
Desemba 27, mwaka jana, wananchi wa mkoa huo, wakiwamo wanasiasa, walifanya maandamano yaliyoratibiwa na baadhi ya vyama vya siasa, ikiwamo Chadema, NCCR-Mageuzi, Sau, TLP, APPT Maendeleo, ADC, UDP na DP, yakiwa na kaulimbiu ya ‘gesi kwanza vyama baadaye, hapa hakitoki kitu’.

Maandamano hayo yaliwashirikisha wananchi wa wilaya za mkoa huo wa Mtwara, zikiwamo Tandahimba na Newala, yalianzia katika Kijiji cha Mtawanya hadi Mtwara Mjini kupitia barabara ya kwenda Msimbati eneo, ambako gesi asilia inapatikana.  

Katika madai yao, wananchi hao walisema serikali haijaweka wazi namna gani wakazi wa Mtwara watanufaika na gesi hiyo, huku tayari Rais Jakaya Kikwete akiwa ameshazindua ujenzi wa bomba kwenda Dar es Salaam na kutaka ujenzi huo usitishwe.

Pia walisema uamuzi wa kupeleka gesi Dar es Salaam unapingana na tamko la Rais  alilolitoa kwenye ziara yake mkoani humo mwaka 2009 kwamba, mkoa huo unaandaliwa kuwa ukanda wa viwanda.  

Nyingine walitaka vinu vya kuzalishia gesi vijengwe Mtwara kwa kuwa wanayo maeneo ya kutosha ya ujenzi huo tofauti na Dar es Salaam.

MBATIA AKATALIWA
Januari 13, mwaka huu, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, alijikuta katika wakati mgumu baada ya kulazimika kufungiwa katika ofisi ya NCCR-Mageuzi Wilaya ya Mtwara Mjini kutokana na baadhi wa wananchi walioudhuria mkutano wake wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mashujaa, kutaka kumdhuru kwa madai kwamba hawakuridhishwa na hotuba yake.

Mbatia, ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais alianza kurushiwa chupa tupu za maji alipokuwa akitoka uwanjani hapo baada ya kukatisha hotuba yake kutokana na baadhi ya wananchi kupinga kauli zake kwa madai hawamuelewi.

Kauli inayodaiwa kumgharimu Mbatia ni ile ya ‘Iwapo gesi itatoka Mtwara’ ndipo wananchi hao walipoanza kupaza sauti wakisema “Hatukuelewi… hatukuelewi”.
Hata hivyo, Mbatia aliendelea kuhutubia hali iliyosababisha wananchi hao wapaze sauti zao kwa kuimba nyimbo. “Haitoki… HatokiHaitoki…”.

Hata Mbatia alipojaribu kuwatuliza wananchi hao kwa kusema ‘gesi kwanza…. Gesi kwanza” baadhi waliitikia na wengine waliendelea kusema hawamuelewi.

Hali hiyo ilimlazimisha Mbatia kukatisha hotuba yake saa 11.25 jioni na aliondoka uwanjani hapo kwa kutembea kwa miguu hali iliyotoa mwanya kwa wananchi kumrushia chupa tupu za maji. 

Mwenyekiti huyo akiwa ameambatana na wabunge wa chama hicho, Moses Machali (Kasulu Mjini) na Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini) wote wa mkoani Kigoma, walikwenda kituo cha polisi kilichopo karibu na uwanja huo na baadaye alikwenda ofisi za NCCR Mageuzi wilaya.

KAULI YA MNYIKA
Siku moja baada ya maandamano hayo; Desemba 28, mwaka jana, Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, alisema maandamano ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara kulalamikia matumzi ya gesi ni matokeo ya udhaifu wa serikali kutotaka kuwashirikisha wananchi kuhusu rasilimali na miradi muhimu ya maendeleo nchini.

Mnyika, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema) alisema maandamano hayo yaliyofanyika Desemba 29 nwaka jana, Mjini Mtwara, ni matokeo ya Bunge kutosimamia kikamilifu serikali kwa niaba ya wananchi.

Alisema serikali inapaswa kutekeleza wanachodai wananchi kwani hawakushirikishwa mapema wakati wa mchakato wa matumizi ya gesi hiyo.

WARAKA WA ZITTO
Desemba 29, mwaka jana, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), alitoa waraka na kuitaka jamii kuwasikiliza wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Zitto, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Bara, pia aliitaka serikali kufikiria upya ujenzi wa bomba la gesi kutoka mikoa hiyo hadi Dar es Salaam, kwa maelezo kwamba, itakuwa ni kupoteza fedha zinazotokana na mkopo kwa kuwa yapo matarajio ya gesi nyingine kuvumbuliwa Temeke, Dar es Salaam.

LIPUMBA APIGILIA MSUMARI
Desemba 30, mwaka jana, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema madai ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara ya kupinga serikali kulazimisha gesi, iliyoko mkoani hapa kusafirishwa Dar es Salaam, hayapaswi kupuuzwa, kwa kuwa hatua hiyo inaathiri maendeleo ya mkoa huo na Tanzania kwa jumla. 

KIKWETE ATOA HOFU
Desemba 31, mwaka jana, akitoa salamu za kuukaribisha mwaka mpya wa 2013 katika hotuba yake kwa Taifa kupitia vyombo vya habari, Rais Jakaya Kikwete, aliwahakikishia wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara, ambako gesi asilia ilipogunduliwa au popote itakapogundulika, kuwa watanufaika sawia na katu hawatasahaulika. 

Hata hivyo, wananchi hao lazima wajue kuwa gesi ni mali ya Watanzania wote.
Kauli hiyo pia ilitolewa na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

MBUNGE AAPA
Januari mosi mwaka huu, Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Asnan Murji, alisema yupo tayari kufa au kupona kwa ajili ya kutetea maslahi ya wananchi wake wanaopinga mpango wa kutaka kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Murji alitoa matamshi hayo akiunga mkono msimamo wa umoja wa vyama vya siasa, walioandaa maandamano ya amani kupinga hatua hiyo inayotaka kuchukuliwa na serikali.

PINDA MTWARA
Januari 13, mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliwasihi wakazi wa mikoa ya Kusini kuwa wavumilivu na kuruhusu mradi wa kusafirisha gesi kutoka mikoa hiyo kwenda Dar es Salaam ufanikiwe kwa kuwa una faida kubwa kwao.

KAULI YA TPDC
Wakati huo huo, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limeeleza kwamba ni asilimia 16 pekee ya gesi itakayotoka Mtwara kwenda Dar es Salaam na kwamba kiasi kingine chote kitasindikwa mkoani humo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Yona Kilaghane, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akiwasilisha taarifa ya shirika hilo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC).

Alisema bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam litakuwa na matoleo ambayo yatatoa gesi Mtwara Mjini, Lindi na Mkuranga.

Alisema kitaalamu gesi inayopatikana kwenye kina kirefu cha bahari inapaswa kusindikwa nchi kavu na kwamba kuna maeneo manne yamependekezwa kwa ajili kujengwa viwanda vya kusindika gesi.

Kilaghane alisema hali ya upatikanaji wa gesi kwa sasa ni futi milioni 80 kwa siku, lakini bomba linalojengwa litakuwa na uwezo wa kusafirisha gesi futi za ujazo milioni 700 kwa siku.

Alisema serikali imeamua kujenga bomba lenye uwezo huo kwa kuwa mahitaji ya gesi yanaongezeka kila siku.

Wabunge walihoji mikataba ya ujenzi wa bomba hilo na kutaka kuiona, lakini TPDC ilieleza kwamba isingeweza kuitoa kwa kuwa iko wizarani kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi.

Aidha, POAC imeiagiza TPDC kuwasilisha orodha ya majina ya wanafunzi wanaofadhiliwa na fedha hizo pamoja na kozi wanazosoma kabla ya  Januari 21, mwaka huu.

Mjadala kuhusu upatikanaji wa gesi mkoani Mtwara umezua mgawanyiko mkubwa, lakini taarifa za serikali zinaonyesha kwamba gesi inayopatikana katika Mkoa wa Mtwara pekee ni asilimia 14, wakati inayopatikana mkoani Lindi ni asilimia saba na Pwani asilimia moja wakati inayopatikana katika kina kirefu cha bahari ni asilimia 78 na kwamba, gesi nyingi inayotumika haitoki katika mikoa ya Mtwara na Lindi pekee.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment