WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, January 30, 2013

‘Mafisadi Zbar wawajibishwe’



Rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,Dk Ali Mohammedi Shein. 

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein ametakiwa kuchukua hatua madhubuti za kuwawajibisha watendaji wa Serikali wenye kufanya ubadhirifu wa fedha na kuisababisha Serikali hasara.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika, Baraza la Wawakilishi, Omar Ali Shehe alitoa ushauri huo wakati akifanya majumuisho ya maoni na michango ya wajumbe wa baraza hilo yaliyotolewa wakati wa kuchangia ripoti ya kamati hiyo.
Shehe alisema, Dk Shein anatakiwa kuwa jasiri na kujiamini katika uchukuaji wa hatua kama anavyofanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ambaye amewawajibisha viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa fedha serikalini.
“Bahati nzuri Mheshimiwa Kikwete anafuata sera za Chama Cha Mapinduzi na Dk Shein pia anafuata sera na kanuni za chama hicho kwa hivyo namwomba sana Dk Shein afuate na aige mfano anaouchukua Mwenyekiti wake,” alisema.
Wakitoa maoni yao wawakilishi walitaka Serikali kuchukua hatua kutokana na fedha nyingi za Serikali kupotea bila ya wahusika kuchukuliwa hatua licha ya ripoti hizo kutoa mapendekezo kadhaa.
Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni, Mahmoud Mussa Abdallah (CCM), alisema anakubaliana na ripoti hiyo iliyowasilishwa lakini bado kunahitajika kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wahusika na kuona vyombo vya sheria vitakavyolishughulikia suala hilo kuwa makini katika kuifanyia kazi ripoti hiyo.
Alisema Zanzibar inafuata utawala bora na haitakuwa busara kuona kazi kubwa iliyofanywa na kamati hiyo  ikaachwa bila ya kuchukuliwa hatua kwa watendaji waliotajwa katika ripoti hiyo.
Mwakilishi huyo alisema ni kweli ndani ya Shirika la Umeme Zanzibar kumekuwa na matatizo na waliofanya hivyo hawakutumwa na vyama vyao kwani ndani ya CCM inakataza wala rushwa na wezi na ni vyema Serikali ikawachukulia hatua za kisheria wahusika wote.
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF), Ismail Jussa Ladhu, alisema Serikali bado haijaonyesha umakini na hivyo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wana haki ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Serikali kutokana na kutokuwana hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahusika wa ubadhirifu wa mabillioni ya fedha.
Alisema wajumbe wa baraza hilo waone kuwa, wanaendelea kufanya kazi ya kuwatumikia zaidi wananchi kwa kuelezea mambo wanayoyataka yakiwemo kufichua mambo maovu yanayotokea.
Jussa alisema wakuu wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) wapo wenye kutumia huduma ya umeme bila ya kulipia jambo ambalo gharama zao hulipishwa wananchi wanyonge. Hiyo inaweza kuwa ni hatari kwa taifa huku akitahadharisha kuwepo kwa matabaka.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni, Salmin Awadh Salmin (CCM), akitoa maelezo yake alisema anasikitishwa na Ofisi ya Mdhibiti wa Serikali kuona imeshindwa kubaini ubadhirifu huo uliotokea katika shirika hilo.
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment