WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, January 24, 2013

Karume wawili watofautiana


Na Salma Said, ZNZ

Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume, ameomba kupatiwa hati halisi (Original) ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambayo imetiwa saini na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume.


Ombi hilo la Karume limekuja kufuatia utoaji wake wa maoni mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, makamo Mwenyekiti Assa Rashid na wajumbe wnegine aliyokutana nayo juzi nyumbani kwake Mjini Unguja.

Karume alisema yeye hana hati ya Muungano na hajawahi kuiona na iwapo Tume hiyo inayo hati hiyo basi angeomba kupatiwa kwani ni wazanzibari wengi wanahitaji kuiona hati hiyo ambayo ni mkataba kati ya nchi mbili zenye mamlaka kamili kila moja na zilizoungana mnamo mwaka 1964 kila nchi ikiwa huru.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya tume hiyo, kimesema Karume mbali ya kutaka kupatiwa hati ya Muungano lakini pia alisema anaunga mkono kuwepo kwa Muungano wa Mkataba ambao kila nchi itakuwa na mamlaka yake kamili na kisha kufuatia huo na mfungamano wa mkataba ambapo alisema Zanzibar kwa takriban miaka 50 sasa imekuwemo katika Muungano lakini imekuwa hainufaiki kiuchumi ndani ya Muungano huo.

Aidha Karume alisema yeye yupo tayari iwapo kutakuwepo na kipindi cha mpito kutoka Muungano huu uliopo na kuingia wa Maktaba pale alipoulizwa na Mjumbe wa Tume hiyo, Salim Ahmed Salim ambaye alionesha khofu yake na uzoefu wa chaguzi zinazofanyika nchini kwamba zinakuwa na machafuko.Karume alisema hakuna machafuko yoyote yatakayoweza kutokezea katika kipindi hicho cha mpito na iwapo Rais aliyekuwepo madarakani hataweza kusimamia na hatajiamini kwa hilo basi yeye anaweza kuchukua nafasi hiyo ili aweze kusimamia hilo na akaahidi kwamba hali itakuwa shuwari na kuivusha Zanzibar katika machafuko kama alivyoweza kusimamia Maridhiano kati ya vyama vikuu vya CCM na CUF mwanzo hadi mwisho wake.

Karume ambaye amekuwa rais kwa miaka 10 Zanzibar amesema amepata uzeofu mkubwa sana katika kipindi cha uongozi wake akiwa madarakani ambapo ameishuhudia Zanzibar ikidhoofika kiuchumi wakati upande wa pili wa Muungano ukinufaika zaidi.

Alisema ni wakati mwafaka kupitia katiba mpya watu kuwa wawazi na kusema ukweli kwa kubainisha kero na matatizo yote ya Muungano ili hatua za lazima zichukuliwe katika kuwaletea wananchi katiba iliyo nzuri na yenye usawa wa nchi mbili zilizoungana na zenye hadhi sawa.

“Karume alisema waziwazi kwamba kwa kipindi cha miaka 10 ameshuhudia mengi sana katika suala zima la maslahi ya Zanzibar, lakini pia alisema sasa ni zama mpya za ukweli na uwazi na kwa hali iliyofikia sasa hakuna njia nyengine zaidi ya kila nchi - Zanzibar na Tanganyika - kurejesha mamlaka yake (sovereignty) kitaifa na kimataifa na kisha nchi hizo mbili kushirikiana kupitia Muungano wa Mkataba kati yao, hivyo ndivyo alivyosema Mheshimiwa Karume” kilisema chanzo chetu cha habari.

Hata hivyo Karume aliwaambia wajumbe wa tume hiyo kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliotiwa saini na Mwalimu Nyerere na Mzee Karume ulikuwa na heshima hapo zamani na ukiheshimiwa sana lakini kumekuwepo na dharau fulani ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi na baadhi ya watendaji jambo ambalo linadhoofisha Muungano huo na kusababisha malalamiko makubwa miongoni mwa pande mbili hizo.
Katika hatua nyengine Balozi Ali Karume alitofautiana na kaka yake kwa kukataa Muungano wa Mkataba akisema Muungano wa serikali mbili kama ulivyo unatosha na pia alikataa kupendekeza Rais wa Zanzibar kuwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akisema nafasi ilivyo ibaki kama ilivyo.

“Mimi siungi mkono mkataba kwa sababu mkataba unaweza kuchezewa kama alivyosema Mwalimu Nyerere lakini katiba haiwezi kuchezewa na mtu na kama atatokea Rais akachezea katiba kitachomfika atakijua mwenyewe, lakini suala la pili mimi hoja ya Rais wa Zanzibar kuwa Makamo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siliungi mkono naona bora ibaki hivyo hivyo kama ilivyo sasa asiwe Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu huwezi kujua Rais wa Tanzania akifa? Na upinzani ukija kuchukua nafasi jee? Alihoji Balozi Karume.

Akizungumza na Mwananchi muda mfupi baada ya kumaliza kutoa maoni hapo katika ofisi ya tume hiyo Maisara Mjini Unguja, Balozi Karume alisema katika maoni yake ametaka urais wa Tanzania uwe kwa zamu ndani ya katiba mpya.

Akitetea mfumo uliopo wa serikali mbili Balozi Karume alisema ameridhishwa na mfumo huu uliopo na haoni kam akuna tatizo la mfumo bali ni tatizo la viongozi wenyewe kuwa shupavu katika kutekeleza majukumu yao ndani ya serikali ya Muungano.

“ Katiba maoni yangu mimi nimesema kinaganaga Zanzibar itambuliwe kikatiba kwamba ni nchi kama zamani ilivyokuwa ikitambuliwa, na isemwe Zanzibar ni nchi na pia Tanganyika kwani Tanganyika sio nchi? kwa nini isitamkwe hivyo tutengeneze katiba ieleze wazi Zanzibar kwa sababu haiwezekani Zanzibar isiitwe nchi wakati watu walipindua na watu chungu zima kufa kwa hivyo kufutwa Zanzibar hilo halikubaliki na wazanzibari hawatakubali, lakini pia itaondosha wawe wenye mawazo potofu kuwa Zanzibar sio nchi” alisema Balozi Karume.

Katika suala jengine ambalo amechangia katika maoni yake ni nafasi ya Urais wa Tanzania ambapo amependekeza kuwepo na usawa wa kupishana iwapo mwaka mmoja atateuliwa Rais kutoka Bara basi afuatiwe na Rais kutoka Zanzibar na hilo amesema ni kwa kila chama isiwe chama kimoja cha CCM tu.

No comments:

Post a Comment