WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, January 18, 2013

Mwalimu Nyerere na uchumi tulioukalia



"UCHUMI mnao, lakini mmeukalia!” Utotoni nilipata kusikia redioni kauli hii ya Mwalimu Julius Nyerere. Tulipokuwa shuleni tulifundishwa na hata kuimba kwamba ili tuendelea tunahitaji vitu vinne; watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.
Wakati tumeumaliza mwaka 2012 na kuingia mwaka mpya wa 2013 Watanzania, na kama taifa, tunahitaji kuwa na visheni katika masuala ya maendeleo. Tuangalie hapa suala la umasikini na mchango wa elimu katika kuondokana na hali hiyo.
Tukirejea kwenye kauli ya Mwalimu Nyerere hapo juu,  na yale tuliyofundishwa shuleni,  ni dhahiri kwamba, watu tunao, tena wengi sana. Ardhi tunayo, tena kubwa sana. Na labda hivyo viwili nilivyovitaja ndio mtaji mkubwa tulio nao.
Huo ndio utajiri wa masikini, lakini hauonekani. Huenda kinachokosekana ni siasa safi na uongozi bora katika kuuendeleza mtaji tulio nao. Kuna Mtanzania mwenzetu aliyebainisha kuwa mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe. Labda nyongeza hapa ni kuwa; mtaji wa nchi ni watu wake wenyewe.
Nchi kupitia vyanzo vyake vya mapato, siasa safi na uongozi bora na zaidi utawala bora, vina wajibu wa kujenga misingi ya jamii bora. Jamii bora ni ishara ya kuwapo kwa taifa bora.
Taifa bora ni taifa lenye nguvu. Hilo litafanikiwa kama dola itaweka kipaumbele katika kuwaendeleza watu wake. Muhimu na la kwanza kabisa ni kuwekeza katika elimu. Huko ni kuuendeleza mtaji muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Angalia hapa, wasichana hawa wenye kupata mimba na kufukuzwa shule ndio sehemu ya makabwela tunaotaka kuwawezesha. Hawa ndio wazazi wa kesho.
Kuwapa nafasi ya pili katika maisha yao angalau tu wamalizie elimu yao ya shule ya msingi ni mojawapo ya njia za kuwawezesha wanawake hawa ili nao waje kuwa walezi bora wa watoto wao ambao pia ni taifa la kesho.
Wasichana wenye kupata mimba shuleni, wengi wao hujutia hali zao. Si wengi kati yao wenye kupenda kukatisha masomo yao. Hakuna mwenye kuona raha ya kukaa nyumbani, halafu kurudi tena shuleni huku tayari akiwa na mtoto wa kumtunza.
Hebu tujikite zaidi kwenye elimu. Ni ukweli, kuwa Serikali kwa kupitia mpango wake wa MMEM (Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi) imefanikiwa katika ujenzi wa madarasa mapya katika sehemu mbalimbali. Lengo pia ni kuwashirikisha wananchi katika masuala ya elimu.
Lakini,  kuna ugumu mkubwa katika hili, kwani wengi wa wananchi ambao Serikali inataka kuwashirikisha,  nao pia wana kiwango kidogo kabisa cha elimu ikiwamo ujinga wa kutokujua  kusoma, kuandika na kuhesabu.
Ili mpango wa MMEM uwe na mafakinio ya muda mrefu, kunahitajika pia kuwapo mpango mwingine wa kuimarisha elimu ya watu wazima . Wazo hapa ni kuwapo kwa Mpango wa Kuendeleza Elimu ya Watu wa Wazima (MKEWAWA).
Visheni ya Serikali ya kuondoa umasikini ifikapo mwaka 2025 haiwezi kufanikiwa endapo hakutakuwapo visheni ya kuondoa ujinga wa kutokujua kusoma na kuandika sambamba na kampeni ya kuondoa umasikini.
Kwa vile zaidi ya asilimia 80 ya watu wa nchi hii wanaishi vijijini na kwamba kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi wetu, kamwe hatuwezi kupiga hatua za haraka za maendeleo endapo idadi kubwa ya watu wetu na hususan waishio vijijini watazidi kuzama kwenye bahari ya ujinga wa kutokujua kusoma na kuandika.
Kuufuta ujinga wa kutojua kusoma na kuandika miongoni mwa watu wetu iwe ndio hatua ya kwanza katika kampeni za kuondoa umasikini. Hapa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi ingeweza kushiriki kikamilifu katika Mpango wa Kuendeleza Elimu ya Watu Wazima kwa kutoa mchango mkubwa katika kuendesha kampeni za kufuta ujinga na kuwaendeleza wananchi kielimu katika hatua ya utu uzima.
Itakumbukwa kuwa, huko nyuma Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima imeshiriki katika kampeni mbalimbali za kitaifa, baadhi yake ni; Kupanga ni Kuchagua (1970), Uchaguzi ni wako (1970), Wakati wa Furaha (1971), Mtu ni Afya (1973), Chakula ni Uhai (1975) na Misitu ni Uhai (1978).
Tuna mfano mzuri wa kampeni ya Kisomo cha Ngumbaru, ya mwaka 1970 iliyoendeshwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuitikia wito wa Rais, Julius Nyerere.
Mwalimu Nyerere alikuwa na visheni kuhusiana na Elimu ya Watu Wazima. Itakumbukwa, Mwalimu alipata kuutangaza mwaka 1970 kuwa mwaka wa Elimu ya Watu Wazima. Mwalimu alibaini, kuwa hatuwezi kuendelea kama nchi, endapo watu wetu wengi wana ujinga wa kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Katika hotuba ile ya mkesha wa mwaka mpya, Mwalimu alianza kwa kukumbushia ahadi muhimu ya mwana –TANU; kwamba “Nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa manufaa ya wote”.
Mwalimu alisisitiza, nitamnukuu; “Hatuwezi kusubiri hadi watoto wetu walio shuleni wamalize elimu yao ndipo tupate maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Ni jukumu la wale raia wa nchi hii ambao tayari wameshakuwa watu wazima kuianza kazi hii. Pamoja na kuzungumzia sana suala la elimu na elimu ya watu wazima, lakini bado hatujajipanga kwa shambulizi kubwa dhidi ya ujinga,” mwisho wa kumnukuu.
Bila shaka hotuba ile ya Mwalimu inafaa kuwa dira ya kutuongoza katika mikakati yetu ya kuendeleza elimu ya watu wazima.  Heri ya Mwaka Mpya!
source Raia mwema Maggid Mjengwa

No comments:

Post a Comment