WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, January 19, 2013

Migongano ya kikatiba ilizaa Azimio la Arusha





“WALE wenye bahati ya kupata elimu, wanao wajibu wa kulipa jasho ambalo wengine wamelitolea. Ni sawa na mtu aliyepewa chakula chote katika kijiji chenye njaa, ili apate nguvu za kwenda kuhemea katika sehemu zilizo mbali. Mtu huyo akikipokea chakula hicho, na halafu asiwaletee msaada ndugu zake, basi yeye ni msaliti.” (Mwalimu Julius Nyerere).
Tamko hilo la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, liliwalenga Wasomi na Vijana wa Taifa hili juu ya wajibu wao kwa jamii nzima. Juu ya Vijana, Mwalimu aliwahi kuelezea aina ya vijana aliotaka kuona. Alisema alitaka vijana jeuri na wenye kujiamini. Si vijana kina ndiyo Bwana! Vijana wenye ujasiri wa kuhoji mfumo wa jamii usioshabihiana na matakwa na matarajio ya jamii. Vijana waasi wa mifumo kandamizi!
Katika hili Mwalimu alisema: “Ni kazi bure, na kwa kweli ni ubatili mtupu kuwa na Taifa lenye silaha (nyenzo za maendeleo) za kisasa, lakini vijana wake ni waoga.”
Maneno haya ya Mwalimu kwa vijana yalijenga jeuri na kujiamini kwa vijana wa Kitanzania miaka hiyo ya 1960 hadi kung’atuka kwake mwaka 1985. Lakini ni jeuri hiyo hiyo aliyowajengea vijana iliyomtoa jasho baadaye pale wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu walipogomea mpango wake wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mwaka 1966 na kulazimika kuwafukuza chuo, Oktoba, 1966.
Mmoja wa viongozi wa wanafunzi hao jeuri ni Waziri wa sasa wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, ambaye Mwalimu, kwa kuona namna alivyosimamia mgomo huo kijasiri, aliamua kumcharaza viboko kabla ya kumruhusu arejee chuoni tena.
Ilikuwa hivi: Mapema Februari 1966, Serikali ilichapisha muswada kwa madhumuni ya kuanzisha programu ya JKT kwa lazima kwa vijana wote waliomaliza elimu ya kidato cha Sita na vyuo vya elimu ya juu, kikiwamo Chuo Kikuu pekee cha Dar es Salaam.
Mpango huo, ulioendeshwa na kusimamiwa na wakufunzi wa kijeshi kutoka Israeli, uliwataka vijana kutumikia JKT kwa miaka miwili, ambapo miezi sita ilikuwa kwa mafunzo ya kijeshi kambini, na miezi 18 ya kutumikia Jeshi nje ya kambi kama watumishi wa umma, na kukatwa asilimia 60 ya mshahara kama mchango kwa Taifa.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilitoa wasomi wake wa kwanza mwaka 1964, ambao walionekana tishio kwa nafasi za vigogo madarakani kwa sababu ya elimu yao. Ni vigogo hao walioasisi wazo la programu hiyo ya JKT kwa vijana.
Kabla ya programu hii, JKT iliyoanzishwa mwaka 1964, ilikuwa kwa vijana wa kujitolea tu. Hata hivyo, hadi Oktoba 1966, ni vijana 25 tu wa kujitolea ndio waliokuwa wamejiunga. Na mpango huo ulipochukua mkondo wa kuwaingiza wasomi kwa lazima, muswada wake haukupokelewa vyema na jamii ya wasomi nchini na baadhi ya wabunge.
Wabunge wasomi kama kina Nicholaus Kuhanga na wengine, wakati wakijadili muswada huo, walisema wazi kuwa: “Kudai kwamba kuwakata vijana asilimia 60 ya mishahara yao ni ujamaa, ni uongo; wabunge na viongozi wa Serikali wanasahau kwamba ni wao hao hao wanaomiliki majumba yenye thamani kubwa na magari ya kifahari, kitu ambacho ni kinyume cha ujamaa. Kwa hiyo, wanapashwa kuonyesha kwanza kwamba wao ni wajamaa kabla ya kuwataka vijana hawa masikini kuwa wajamaa.” (Hansard, Septemba 22 – Oktoba 11, 1966 ukurasa 249).
Muswada huo ulizua ukinzani mpana katika jamii hadi maofisini, ambapo kuliripotiwa kisa kimoja wakati wa mjadala bungeni, juu ya mabishano makali ya maofisa wawili; mmoja msomi na mwingine asiye msomi, wakiapizana.
Yule asiyesoma akisema: “Kusoma si hoja, ukiwa na digrii mtatufanya nini wakati tuna majumba, magari, vipusa (warembo) na madaraka tunayo?” (Hansard, kama hapo juu).
Mara tu muswada huo ulipopita, wanafunzi waliwasilisha serikalini madai yao ya kutaka muda wa JKT upunguzwe kutoka miaka miwili hadi miezi sita, na makato ya asilimia 60 ya mishahara yaondolewe. Yalipokatiliwa madai yao, waliona kwamba Serikali haikuwa na nia njema kwao; saa ya machafuko ilikuwa inajongea taratibu.
Ziara za mara kwa mara za viongozi wa Serikali chuoni hapo kuzungumza na wanafunzi, hazikubadili hisia za wanafunzi hao. Mambo yalitibuka zaidi pale Naibu Waziri wa Ulinzi na JKT wa wakati huo, Richard Wambura, alipowahutubia wanafunzi, Oktoba 18, 1966; katika hotuba ambayo ilitafsiriwa kuwa mpango huo wa JKT ulikuwa wa hila, kwa lengo la kuwaonea na kuwanyanyasa vijana kwa kuwa tu wao ni wasomi.
Baada ya hotuba hiyo, wanafunzi waliitisha mkutano wa dharura, ambapo ziliundwa kamati mbili. Moja ya kwenda kuonana na Rais (Julius Nyerere) kuelezea malalamiko yao, na ya pili; kwenda Polisi kuomba kibali cha kufanya maandamano.
Kamati iliyokwenda kuonana na Rais ilitoa taarifa kwa wanafunzi hao kwamba Mwalimu hakuwa na uhakika juu ya kile kilichokuwa kikiendelea. Aliyatupilia mbali malalamiko yao. Na ile iliyokwenda Polisi, ilitaarifu juu ya kukataliwa kibali. Oktoba 21, 1961, wanafunzi waliitisha kikao kingine cha dharura; wakaazimia kuandamana bila kibali cha Polisi, kwenda Ikulu kukabiliana uso kwa uso na Mwalimu Nyerere.
Waliandaa mabango yenye ujumbe mbalimbali. Kwa kutaja baadhi tu, mabango hayo yalisomeka: “Tumechoka kutumikia wabenzi (mafisadi). “Afadhali wakati wa Ukoloni.” “Kumbuka ya Indonesia.” “Atokomezwe Kawawa na mpango wake.” Na mengi mengine.
Hili la “Kumbuka ya Indonesia,” liliikumbusha Serikali namna Serikali ya Rais Suharto wa nchi hiyo, ilivyopinduliwa kwa maandamano ya wanafunzi. Lakini hili la “Afadhali wakati wa Ukoloni,” kuna taarifa zisizothibitishwa kwamba halikuwa na ridhaa ya wanafunzi, na kwamba lilipandikizwa tu na watu wa Usalama wa Taifa ili kuchokoza hasira ya Mwalimu Nyerere aweze ‘kuwaadabisha’ waandamanaji.
Bila ya wanafunzi hao kujua, huko Ikulu, Oktoba 22, 1966, Mwalimu aliitisha kikao cha dharura cha Baraza la Mawaziri, ili pamoja na mambo mengine, kuamua namna ya kukabiliana na waandamanaji watarajiwa. Iliazimiwa kwamba maandamano yaongozwe na askari polisi kuingia Ikulu hiyo Oktoba 22, 1966.
Ilivyotokea ni kwamba maandamano hayo hayakuwahusisha vijana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pekee, bali walijiunga wengine wengi kutoka Chuo cha Uganga cha Muhimbili, Chuo cha Ualimu Chang’ombe, Chuo cha Biashara tawi la Dar es Salaam (CBE) na Shule ya Sekondari Aghakhan.
Pale Ikulu, waandamanaji hao walilakiwa na Mwalimu, Makamu wa Pili wa Rais, Rashid Mfaume Kawawa na Mawaziri kadhaa. Kisha, Mwalimu alimkaribisha msemaji wa waandamanaji kutoa malalamiko yao. Msemaji huyo akatoa masharti yao kwa lugha ya Kiingereza fasaha, tena kwa ukali, akisema:
“Serikali inajaribu kuutupa mzigo wa kugharamia mpango huu (JKT) mabegani mwa wanafunzi masikini…au tulipwe haki zetu zote za mishahara, ama wale wote wanaopata mishahara ya juu nao watumbukizwe katika utaratibu huu ili uonekane kweli kuwa ni wa kujitolea na si wa kunyonywa.”
Kabla ya kuhitimisha tamko la wanafunzi, aligonga nyundo iliyomsitua Mwalimu, kesha akaendelea: “Kwa hiyo, Mheshimiwa, kama utaratibu huu pamoja na mawazo ya viongozi wa juu hayakubadilika, hatukubali mpango wa JKT kwa moyo. Miili yetu inaweza kwenda, lakini mioyo yetu itabaki nje ya mpango huu.” Waandamanaji wenzake wale wakamshangilia sana na kumpigia makofi.
Kisha akahitimisha tamko hilo la wanafunzi kwa kishindo, akasema: “Vita baina ya wanasiasa na watu wenye elimu vitaendelea daima…Aksante.” Hapo akawa amemchokoza Mwalimu.
Mwalimu alianza kujibu risala, kwanza kwa pole pole na kwa sauti tulivu. Alisema: “Nilielewa hili. Nimeyaelewa malalamiko yenu. Sisi Serikali tumepata ujumbe wenu. Natafuta njia ya kueleza kidogo. Maneno yenu tuliyowaambia viongozi wenu, yamewafikia.” Mwalimu alitokwa na maneno hayo huku akiangaza macho huku na kule.
Baadaye sauti ilianza kupanda kidogo, na akasema: “Sasa mimi nimeyakubali masharti yenu. Naweza kuwahakikishia kwamba sitamlazimisha mtu yeyote. Mnayosema ni sawa. Hata miili yenu ikienda (JKT), mioyo yenu haitakuwa huko…sintampeleka hata mmoja katika JKT ambaye moyo haupendi (makofi kutoka kwa waandamanaji)…maana huko si gerezani! Lakini hata hivyo, mpango wa JKT utaendelea kuwa wa lazima kwa kila mwanafunzi ambaye hatimaye atafanya kazi serikalini. Kwa hiyo, ni juu yenu kuamua…”
Mwalimu aliendelea: “Mnayosema juu ya mishahara, ni ya kweli, ni mikubwa mno (makofi na shangwe). Mimi na ninyi tumo katika kundi la wanyonyaji. Je; hayo ndiyo mambo nchi hii iliyopigania? Je; juhudi yote tuliyofanya ni kwa sababu ya kuneemesha kikundi cha wanyonyaji huku juu?” Alihoji hayo Mwalimu kwa sauti kali.
Kisha akawaeleza juu ya mapinduzi yanayotakiwa. Akasema: “Siku nitakayoweza kumlipa mfanyakazi wa Tanzania mshahara wa Shilingi mia tano kwa mwezi, tutakuwa tumefanya mapinduzi makubwa sana…hapo tutaweza kusimama juu ya Mlima Kilimanjaro na kutangaza Mapinduzi ya Tanzania.”
Ili kuthibitisha kwamba alikuwa hatanii juu ya mishahara mikubwa, Mwalimu akasema: “Mshahara wangu mnaujua ni kiasi gani? Shilingi elfu tano kwa mwezi. Ni mkubwa mno!” Hapo akapandisha sauti, akasema: “Mshahara wangu naupunguza kwa asilimia ishirini kuanzia sasa hivi…nchi hii yahovyo; mishahara minene mno,” alifoka Mwalimu.
Kisha akarejea kwenye hoja ya siku hiyo. Akasema: “Mimi nimeyakubali maneno mnayosema (wanafunzi waandamanaji). Na ninyi, mimi nawaomba mwende nyumbani kwenu. Rashid (Kawawa), ni jukumu lako kuhakikisha kwamba wanakwenda kwao hawa.”
Mwalimu alikuwa amewafukuza wanafunzi wote 415. Muda huo huo wakazingirwa na askari polisi, wakaanza kushughulikiwa kwa kipigo kikali na kudhibitiwa.
Oktoba 28, 1966, Chama cha Wanafunzi (USUD), kupitia barua iliyotiwa sahihi na Kaimu Rais wa chama hicho, kilimwomba Mwalimu atumie hekima yake kuwasamehe wanafunzi waliofukuzwa. Barua nyingine ya Oktoba 30, 1966, iliweka bayana kwamba malalamiko ya wanafunzi hayakutendewa haki kwa kueleweka vibaya, na kwamba wanafunzi hao walitaka kupindua Serikali.
Hatimaye, Julai 1967 Mwalimu alikubali kuwarejesha wanafunzi 392 kati ya 415 waliokuwa wamefukuzwa. Wanafunzi 23 hawakurejeshwa kwa madai ya kuwa ndio waliokuwa viongozi wa mgomo, kati yao hao akiwamo Waziri wa sasa wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta.
Hawa walitakiwa kwanza waombe radhi kwa Mwalimu mwenyewe uso kwa uso, wakionyesha kujuta kwao kumethibitika kuwa na manufaa kwa jamii. Walifanya hivyo, na baadaye walirejeshwa miezi kumi baadaye baada ya wenzao hao 392 kurejeshwa.
Pamoja na kufukuzwa kwa wanafunzi hao, Mwalimu hakuweza kuipangua hoja yao juu ya vigogo wa Serikali kujineemesha kwa jasho la wanyonge wa nchi hii, na hivyo akachukua hatua hima ya kupunguza mishahara ya viongozi wote nchini.
Kwa kuwafukuza wanafunzi hao, Serikali ilikuwa inajitafutia sifa na umaarufu rahisi wa kwamba ilikuwa inatekeleza matakwa ya wananchi, wakati ukweli ulikuwa ni kinyume chake, tabia ambayo inaendelea hadi leo.
Profesa T. O. Ranger, katika barua aliyomwandikia Msaidizi wa Rais, Mama Joan Wickens, yenye Kumb. C3/SA.13 ya 2/3/1967, kumwomba amshawishi Mwalimu awarejeshe wanafunzi hao 23, alisema wazi kwamba haikuwa halali kwa wanafunzi hao kutumika kama chambo kwa Serikali iliyokuwa imepoteza dira na iliyojaa na kudhibitiwa na mafisadi, wasiojali maslahi ya umma.
Ukweli huo ulijidhihirisha pale Mwalimu Nyerere alipoyatafsiri kwa vitendo, madai ya wanafunzi kwa kutangaza Azimio la Arusha, Februari 5, 1967, kama dira ya sera za uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujenzi wa jamii yenye usawa, tofauti na ile iliyokuwa ikijengeka mwaka 1966.
Azimio la Arusha na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, vilipokelewa kwa nderemo na vifijo na jamii ya wasomi kama mkombozi wa wanyonge. Kuanzia hapo, na hatimaye Tanzania kuamua kufuata siasa za mrengo wa Kisoshalisti, wanafunzi vijana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, walifunga fungate ya uswahiba na Serikali iliyokuja kukatwa na sera za soko huria kupitia Azimio la Zanzibar mwaka 1992.
Historia hujirudia. Yale ya mwaka 1966 yamerejea tena nchi tayari. Kama Tanzania sasa ni masikini kuliko ilivyokuwa kabla ya Uhuru, kuna tofauti gani kati ya sasa na wakati wa ukoloni? Kama matabaka nchini yameruhusiwa kujijenga, kuna tofauti gani kati ya enzi za Wabenzi wa 1966 na mafisadi wa sasa?
Jamii yetu imewekeza kwa vijana kwa kujinyima, ili hatimaye wapate nguvu ya kuhemea maendeleo ya nchi kwa manufaa ya wote. Lakini ilivyo sasa, vijana hawa wanagawana na vigogo mafisadi kila walichohemea kabla hakijamfikia mwananchi. Wamegeuzwa (vijana) vipeperushi vya wakubwa! Huu ni usaliti kwa jamii! Kile ambacho vijana makini wa mwaka 1966 walikataa kwa nguvu na kupata ushindi mkubwa, vijana wa leo wanakisujudia. Wanalisaliti Taifa!
source:Raia Mwema Joseph Mihangwa

No comments:

Post a Comment