WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, December 31, 2012

Urais 2015: Chadema sasa vipande viwili



SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kumtangaza Dk Willibrod Slaa kuwa ndiye mgombea wa urais mwaka 2015 kwa tiketi ya chama hicho, makada wa chama hicho wamegawanyika baadhi wakimponda na wengine kumuunga mkono.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya makada wa chama hicho walisema mwenyekiti wao amekosea kumtangaza mgombea kabla ya wakati, huku wanaomuunga mkono wakisema hajakosea kwa sababu hatua hiyo itasaidia kuondoa makundi ndani ya chama hicho.
Juzi, Mbowe akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Karatu mkoani Arusha, alisema Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa atapewa fursa ya kuwania tena urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015, huku mwenyewe akijiweka kando kuwania nafasi hiyo
Hata hivyo, Dk Slaa alipoulizwa iwapo ana nia ya kuwania nafasi hiyo alihoji: “Kwani mwaka 2010 nilijitangaza mwenyewe,? Iwapo wanachama wa Chadema watanipendekeza nitafikiria kufanya hivyo.” Mwasisi wa chama hicho Edwin Mtei, Wajumbe wa Kamati Kuu; Profesa Mwesiga Baregu na Dk Kitila Mkumbo, Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa Bavicha John Heche na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema walitoa maoni yanayopingana kuhusu kauli hiyo ya Mbowe.
Wanaounga mkono
Mtei alisema anaunga mkono kauli ya Mbowe akisema kiongozi huyo hajakosea kumtangaza Dk Slaa kuwania urais mwaka 2015.
“Ninaunga mkono Dk Slaa kuwania tena nafasi ya urais mwaka 2015. Mwenyekiti amemtangaza baada ya kupata baraka ya vikao vya chama,” alisema Mtei.
Ingawa Mtei hakuwa tayari kusema ni kikao gani kilichopitisha jina la Dk Slaa kuwania nafasi hiyo, alisisitiza: “Kuna vikao vya Kamati Kuu vimefanyika hivi karibuni, vinaweza kuwa vimefanya uamuzi huo. Mwenyekiti hawezi kuzungumza jambo bila baraka za vikao vya chama.”
Hata hivyo, kauli hiyo ya Mtei inapingana na ile aliyoitoa Oktoba 6, mwaka huu baada ya Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini kutangaza kutogombea tena ubunge badala yake kusema anataka kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Mtei alisema hatua ya Zitto kutangaza kuwania urais mapema kungesababisha  mzozo na mpasuko  ndani ya chama hicho.
Mtei alisema amekuwa akimshauri Zitto mara kwa mara kuhusu hatua yake hiyo akimtaka kuwaunganisha wana Chadema na siyo kuwagawa au kuwavuruga.
“Hakuna shida kuonyesha hisia, lakini unatengeneza mzozo mkubwa sana ukitangaza sasa. Mimi nimeshamshauri sana Zitto, ahakikishe anakiunganisha chama na siyo kukigawa wala kukivuruga.”
Alisema mbunge huyo kutangaza kutogombea tena ubunge na badala yake kujipanga kuwania urais mwaka 2015 kumekuja mapema mno na kuonya kuwa itaibua mzozo ndani ya Chadema.
Mtei ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu enzi za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, alisema kwamba wakati mwafaka ukiwadia, Chadema kitaamua ni nani mwenye sifa za kugombea urais  huku akisema kina utaratibu wake wa kuwapata wagombea mbalimbali wa uongozi.
Hata hivyo, Zitto jana alikataa kuzungumzia suala hilo akisema: “Nimesikia hata mimi kwenye vyombo vya habari ila sina cha kuzungumza kuhusu hilo.”
Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Heche alisema kauli hiyo Mbowe siyo yake binafsi, bali ni ya wananchi.

“Ni kauli na maoni ya Watanzania wanaomwamini Dk Slaa kuwa anaweza kumudu kuliongoza taifa hili kama walivyoonyesha kwa kumpigia kura nyingi kuliko mgombea yeyote wa upinzani katika nafasi ya urais (mwaka 2010),” alisema Heche.
Heche alisema ingawa ndani ya Chadema kuna viongozi wengi wenye uwezo wa kuliongoza taifa, nyota ya Dk Slaa bado inang’ara.
Msimamo wa Heche uliungwa mkono na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambaye alisema ni sahihi Dk Slaa kugombea urais mwaka 2015.
Lema alisema katika historia ya chaguzi za vyama vingi nchini, hakuna mgombea wa upinzani aliyewahi kupata kura nyingi kama Dk Slaa mwaka 2010 akadai kwamba ndiyo maana hivi sasa CCM kinafanya kila njama kumdhoofisha.
Lema alisema hatua ya kumtangaza Dk Slaa kuwa mgombea wa urais mwaka 2015, itaondoa harakati za chinichini zilizokuwa zikifanywa na watu ndani na nje ya Chadema kuwagombanisha viongozi wakuu wa chama hicho, hasa Mbowe na Dk Slaa.
Wanaopinga
Wakati Mtei akieleza kuwa Mbowe amepata Baraka za chama, Profesa Baregu alisema kutangazwa kwa jina la Dk Slaa kuwania urais ni maoni binafsi ya mwenyekiti huyo.
“Hayo ni maoni yake, lakini vikao vya chama ndivyo vyenye uamuzi wa mwisho kuteua jina la mgombea urais na havijakaa,” alisema Profesa Baregu.
Alipoulizwa maoni yake  kuhusu sababu za Mbowe kumtangaza mgombea urais sasa kabla ya wakati, Profesa Baregu alisema: “Mbowe atakuwa amefanya hivyo kwa sababu watu wengi walikuwa wanadhani kwamba yeye pia anawania nafasi hiyo ya urais.”
“Hivyo ili kuweka mambo sawa ameamua kutangaza mapema kuwa hatawania urais na kwamba Dk Slaa ndiye anayefaa kuwania nafasi hiyo,” alisema.
Profesa Baregu alisema haoni tatizo kwa wanachama wa Chadema kutangaza nia mapema kwa sababu hiyo ni haki yao kwa mujibu wa katiba... “Hata kama watu wengi watatangaza nia ya kuwania urais, siyo jambo baya katika ujenzi wa demokrasia, lakini uamuzi wa mwisho ni wa vikao vya chama.”
Kauli ya Profesa Baregu kuhusu vikao iliungwa mkono na Dk Mkumbo ambaye alisema kwamba anachojua vikao vya chama ndivyo vyenye uamuzi wa mwisho kuhusu uteuzi wa wagombea wa ngazi ya urais.
Dk Mkumbo alionyesha shaka kama kweli Mbowe alimtaja Dk Slaa kuwa ndiye atakayewania nafasi hiyo akisisitiza: “Ninachofahamu ni kwamba yeye ametangaza kuwa hatagombea nafasi hiyo.”
Mwananchi

No comments:

Post a Comment