WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, December 16, 2012

Mgimwa: Serikali haikurupuki



Waziri  wa  Fedha, Dk.  William Mgimwa  amesema Serikali  haiwezi  kukurupuka kutoa  maamuzi  kuhusu  madai ya  kuwepo kwa  Watanzania waliohifadhi fedha  katika benki za nchini  Uswiss.

Alisema ndiyo maana Serikali  imetoa  fursa  kwa  kila Mtanzania  kujitokeza na  kutaja  jina  ama  majina ya watu wanaotuhumiwa.



Dk. Mgimwa alitoa taarifa hiyo jana wakati   akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kuhutubia kwenye mahafari ya kwanza ya wahitimu wa kozi ya Mipango na Maendeleo vijijini  ngazi ya cheti katika tawi la kanda ya  Ziwa (Mwanza).

“Ni kweli  madai hayo  yapo, Lakini  Serikali  hata  siku moja haiwezi kukurupuka  na kutoa maamuzi  ikiwemo kukamata watu  hovyo hovyo  pasipo  kufuata sheria, kanuni pamoja na taratibu za Kamataifa,” alisema  Dk Mgimwa  ambaye  alikuwa  mgeni rasmi  kwenye mahafari hayo.

Alizitaja baadhi ya taratibu hizo kuwa ni  kupatikana kwa majina pamoja na ushahidi wa majina ya   watuhumiwa, malalamiko hayo kupitiwa na kitengo cha upelelezi wa kimataifa (Financial Intelligency  Unit) na Serikali ya Uswiss kuwa tayari kuthibitisha kwamba ni kweli fedha hizo zimehifadhiwa nchini humo kwa nia ovu.

Dk Mugimwa alisema kwa mujibu wa sheria, siyo kila fedha zinazohifadhiwa nje ya nchi ni fedha  haramu.

“Ndiyo maana sasa hivi tuna mpango wa kuanzisha utaratibu wa kutunza fedha nje ya nchi kwa ajili ya akiba ya kigeni  kwa kipindi cha miezi minne wakati tunapopata dharura” alisema.
Alikanusha madai ya waandishi wa habari kwamba  huenda serikali inaogopa kuwakamata na  watuhumiwa ndiyo maana hakuna hatua yoyote  iliyokwishachukuliwa.

“ Siyo kwamba tumenyamaza ama tunaogopa  kuwakamata watuhumiwa na kuwashukulia hatua  za kisheria, hapana. Kwa mfano, hadi sasa  tunawasiliana na Uswiss (serikali) ambayo wengi   wanasema ndiko ziliko fedha; kinachotakiwa na ambacho ofisi yangu inakifanya sasa hivi  ni kufuata  taratibu za kimataifa,” alisema na kuongeza kuwa ni mapema mno kuilaumu Serikali ya Tanzania.

Alifafanua kwamba kwa kulitambua hilo,  ndiyo maana  Serikali  imetoa  mwanya kwa kila Mtanzania anayedhani kwamba anao ushahidi wa kutosheleza   kuwasilisha majina ya watuhumiwa kwa njia ya siri  ili yafanyiwe kazi.

Hata  hivyo,   wakati akihutubia  kwenye  mahafari hayo, Dk Mgimwa  aliwataka  wahitimu  hao kuwa mfano wa kuigwa kwa kutofanya  kazi  kinyume  na maadili ya  kazi .
Aliuahidi  uongozi  wa   chuo hicho kwamba  ofisi yake itakuwa bega kwa bega katika kukabiliana na changamoto kadhaa  zinazokikabili chuo hicho.

Awali, Mkuu   wa chuo hicho, Costantine  Lifuliro   alimweleza  Dk Mgimwa   kwamba  chuo  kinakabiliwa na upungufu wa  vitendea kazi.

Alivitaja vitendea kazi hivyo kwamba ni pamoja na vitabu  kwenye maabara, upungufu wa kompyuta   fedha  kwa ajili ya ujenzi   wa  chuo  kwa vile hadi sasa    chuo hicho kinatumia majengo ya  kanisa la Africa  Inland  Church Tanzania(AICT).

Alisema   jumla  ya  wanachuo 323   wamehitimu  mafunzo  ngazi ya cheti.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment