WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, December 9, 2012

Tafsiri Yangu Jumapili hii - Taifa Lisilo Na Utambulisho Wake...!



                                                    
Na: Maggid Mjengwa,

Ndugu zangu,
Utamaduni ni utaratibu wa maisha ikiwa ni pamoja na sanaa za maonesho, muziki asilia, ngoma za asili, tamthilia, lugha, sanaa za ufundi, filamu na chakula. Utamaduni ni utambulisho wa mtu husika. Kama huwezi kuuthamini utamaduni wako, basi, umeshindwa kujithamini mwenyewe. Ni nani basi atakayekuthamini?
Tuna kila sababu ya kujikita katika kurejesha heshima, hadhi, moyo na juhudi za kukuza utamaduni wetu unaotishiwa kumezwa na tamaduni za kighaibu hususan zile za kimagharibi. Tutumie utandawazi unaoambatana na sayansi na teknolojia kama nyenzo na fursa ya mafanikio ya jitihada za kuendeleza, kukuza, kusambaza na kuuza utamaduni wetu.

Tuuthamini, kuuendeleza na kuukuza utamaduni wetu.
Leo hii ukiangalia muziki unaopigwa kwenye redio zetu, filamu zinazonyeshwa na hata kuigizwa na Watanzania wenzetu. Ukiangalia namna ya mavazi tunayovaa, vyakula tunavyokula na hata lugha tunayozungumza. Vyote hivyo havitoi taswira ya utamaduni halisi wa Mtanzania. Maeneo ya mijini ndiyo yanayoelekea kumezwa zaidi na tamaduni za kighaibu.
Tuna haja ya kutafakari kwa kina juu ya utamaduni tunaoujenga sasa. Itakumbukwa, miaka ile ya mwanzoni mwa uhuru wetu, masuala ya utamaduni yaliwekwa chini ya Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana. Wizara hii ilianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1962. Kunako Desemba 10, mwaka 1962, Mwalimu Nyerere aliweka bayana majukumu ya Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana, Mwalimu alitamka yafuatayo;
" Mabadiliko makubwa niliyoyafanya ni kuanzisha Wizara mpya ya Utamaduni wa Taifa na Vijana. Nimefanya hivyo kwa kuamini kuwa Utamaduni ni kitu muhimu na ni roho ya taifa lolote liwalo.

Taifa lisilo na utamaduni ni sawa na mkusanyiko wa watu walikosa hari na moyo wenye kuwafanya kuwa taifa. Moja ya dhambi kubwa ya wakoloni ni ile hali ya kutufanya tuamini kuwa hatuna utamaduni wetu wa asili; au kwamba yote tuliyokuwa nayo hayakuwa na thamani yeyote-kitu ambacho tulipaswa tukionee aibu badala ya kuwa chanzo cha kujivunia.

Baadhi yetu, hususan wale tulioelimishwa na Wazungu tunanajaribu kuwathibitishia wakoloni waliotutawala kwamba "tumestaarabika" ikiwa na maana tumeachana na yale yote yenye kutuunganisha na utamaduni wetu wa asili. Kwamba tumejifunza kuiga utamaduni wa Kizungu. Malengo ya vijana wetu hayakuwa kuwa Waafrika walioelimika bali kuwa Wazungu Weusi." Hayo ni maneno ya Mwalimu Nyerere mwaka 1962.

Bila shaka, Mwalimu Nyerere alikuwa ni mfano wa viongozi waliothamini na kuuenzi utamaduni wetu ikiwemo lugha ya Kiswahili. Leo tunashuhudia jinsi jamii yetu ilivyovamiwa na tamaduni za kighaibu. Ni dhahiri kuwa utamaduni unaimarika kwa kuiga yaliyo mazuri kutoka tamaduni nyingine.
Lakini , katika jamii yetu, tamaduni za kighaibu hususan kutoka Ulaya na Marekani zaelekea kukumbatiwa zaidi na wanajamii na hivyo basi kuhatarisha kuufifisha na pengine kuuangamiza utamaduni wetu.

Vijana wetu wanaona fahari zaidi kuimba na kucheza nyimbo na miziki ya kighaibu. Wanaona aibu kuimba nyimbo za Kiswahili. Nyimbo za makabila yetu kwa mfano Kinyamwezi, Kizaramo na nyinginezo za asili. Vijana wetu wanaona fahari kuongea Kiswahili kwa lafidhi ya Kiingereza. Vijana wetu wengi wa siku hizi hawajawahi kusikia au hata kujaribu kucheza Gombe Sugu, Mganda, Mangala, Konge, Nyang'umumi, Kiduo, au Lele Mama. Hizi ni baadhi tu ya ngoma zetu za asili. Vijana wetu wengi hawajawahi kusikia au hata kujaribu kupiga vyombo vya muziki vya asili kama vile Marimba, Kilamzi, Ligombo au Imangala.

Na tuangalie ni jinsi gani tutaweza kuuhifadhi, kuuendeleza na kuuimarisha utamaduni wetu. Hivi leo kuna wanaozungumza au kuandika kwa Kiingereza mahali ambapo asilimia 90 ya wasikilizaji au wasomaji ni wazungumzaji wa Kiswahili. Hiyo ni hali ya kutojiamini. Ni kubaki katika hali ya utumwa wa fikra. Je, wenye kufanya hivyo wana malengo ya kuwaonesha "wakoloni" au "Wafadhili" wa semina kwamba wao "Wamestaarabika"? Au wanafanya hivyo ili kuwaridhisha Wafadhili tu? (Rejea kauli ya Mwalimu Nyerere mwaka 1962 hapo juu). Kwa nini waandaaji wa semina wasitumie wakalimani kuwatafsiria wasio wazungumzaji wa Kiswahili ambao ni asilimia kumi tu ya kadamnasi. Hilo pia lingetengeneza ajira kwa baadhi ya Watanzania. Tubadilike.

0788 111 765, 0754 678 252 http://mjengwablog.com

No comments:

Post a Comment