WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, December 16, 2012

HEBU TUJIKUMBUSHE MAKALA HII YA JENERALI ULIMWENGU



Tusiwe watu wa ‘fasta fasta’, tunayo miaka bilioni ya kuishi hapa

Makala yangu iliyopita ilijadili umuhimu wa kuwa na mtazamo wa mbali, na kufanya mipango yetu kwa kuamini kwamba taifa letu litakuwapo baada ya sisi tuliopo kutoweka.
Hii ina maana ya kuachana na mtindo wa kulipua na kufanya kazi kwa njia za zimamoto. Ina maana ya kupanga miradi mikubwa ndani ya programu pana zinazoangalia upeo wa karne kadhaa zijazo.
Kila nikitathmini utendaji wetu, na hasa utendaji wa wakuu wa Serikali, sioni mtazamo wa aina hiyyo. Ninachoona ni kufanya mambo ‘ad hoc,’ haraka haraka, kwa ajili ya leo au kesho tu, halafu tutaangalia. Tunalipua, hatuna mtazamo wa kimkakati, kana kwamba muda si mrefu ujao tutakuwa hatupo tena.
Kutokana na hali hii, tumezalisha ‘viongozi’ wengi wanaodhani kwamba kuchapa kazi maana yake ni kupiga kelele majukwaani, kutoa amri kwa watendaji kupitia kauli za majukwaani na kupitia televisheni.
Leo hii, kila ‘kiongozi’ anashindana na mwingine kwa kujaribu kutoa amri nyingi kuliko mwingine. Matokeo yake ni kwamba hatuna mipango ya muda mrefu wala mipango iliyoratibiwa kuhusisha nchi nzima na sekta zote. Kila amri inajitegemea na kila ‘kiongozi’ ana mipango yake.
Hii ndiyo staili ninayoiita u-Mrema kutokana na staili aliyoianzisha Augustine Mrema alipokuwa waziri aliyehusika na mambo ya usalama wa raia.
Naamini kwamba Mrema alichukua staili ya kutoa matamko mengi hadharani ambayo mengi yalikuwa ni amri kwa watu aliowataka wafanye hili au lile, kwa sababu hakuwa na uwezo wa kutambua ni vipi Serikali inatakiwa kufanya kazi, akidhani kwamba waziri mchapa kazi ni yule anayekwenda mwenyewe kukamata walanguzi wa pombe na wafanya magendo ya kahawa.
Kinachotusumbua leo, ni kwamba Mrema alifanikiwa mno katika juhudi zake za kupata umaarufu, kwani wananchi wa kawaida ambao nao hawajui ni jinsi gani Serikali inatakiwa ifanye kazi yake, walimuona kama shujaa.
Wananchi wa kawaida waliziona zile amri za ‘siku saba’ kama ushahidi wa waziri anayefanya kazi yake bara bara. Wala hawakuhoji ni kwanini mara kadhaa aliwataka wafanyabiashara walioonekana kama wasio waaminifu wamfuate kijijini kwake Moshi.
Wananchi pia hawakuhoji ni kwanini Mrema alikuwa na ujasiri wa kuwalaumu mawaziri wenzake hadharani kwa kusema kwamba walikuwa wanamzuia kufanya kazi yake kikamilifu kwa kuwa walikuwa si waaminifu kwa wananchi.
Bila shaka walikuwapo mawaziri walioona kwamba utendaji kazi serikalini haukupaswa kuwa jinsi Mrema alivyokuwa akifanya, na bila shaka walisema hivyo katika vikao vya Baraza la Mawaziri, lakini wakaonekana kama wasio na maana.
Katika utaratibu wa Serikali inayoendeshwa kama Serikali, ilitakiwa Rais Ali Hassan Mwinyi (wakati huo wa Mrema) amuondoe serikalini mapema asubuhi kwa kukiuka utaratibu wa Serikali.
Badala yake akampandisha cheo na kumfanya Naibu Waziri Mkuu, huku akiendelea kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, mamlaka makubwa mno mikononi mwa mtu aliyekuwa ametia fora katika kuvuruga utaratibu wa utendaji serikalini. Sababu zake ni nini? Nitajaribu kueleza.
Utawala unaokabiliwa na malalamiko mengi ya wananchi bila kuwa na maelezo ya kuridhisha, utakumbatia kila aina ya ubabaishaji alimradi unashabikiwa na wananchi, kimsingi kwa sababu ushabiki wa wananchi unaonekana kuujengea uhalali, na Mrema alionekana hivyo.
Wala hakuwa wa kwanza, kwani hata Edward Sokoine alikuwa na muonekano huo wakati wa kile kilichojulikana kama ‘Uhujumu Uchumi.’ Maana yake ni nini? Mfumo uliochoka na ulioshindwa kutafuta majibu sahihi kwa maswali ya wananchi, utaegemea juhudi za kiimla za mtendaji mmoja mmoja, kama Sokoine chini ya Mwalimu Nyerere na Mrema chini ya Ali Hassan Mwinyi, na hawa tunaowashuhudia chini ya Rais Jakaya Kikwete.
Maana yake ni kwamba ni rahisi zaidi kuachia watu wawili au watatu wakapita wakifoka na kutoa amri, badala ya kujenga mifumo ya utekelezaji iliyosimama juu ya misingi ya kisera na kisheria, ambayo inasumbua akili, inahitaji usimamizi makini na inahitaji uratibu ulio makini wa sekta zote zinazohusika na zinazoingiliana. Hiyo ni kazi ngumu zaidi kuliko kutoa amri za kiimla.
Lakini ni staili dhaifu na isiyo endelevu, haina mashiko ya kiutekelezaji, haina uwezo wa kuenea kote nchini na inatoweka mara tu anapoondoka madarakani waziri au mkuu yeyote aliyeianzisha. Ni moto wa kifuu unaowaka sehemu ulipowashiwa, lakini usiosambaa sehemu nyingine yo yote, na baada ya muda mfupi tu kitakachosalia ni majivu baridi.
Wale wanaopendelea staili hii wanapaswa wajiulize, iwapo waziri ametembelea wilaya moja ambako amekuta matatizo ya utendaji mbovu na akaona jawabu ni kutoa amri ya kumsimamisha mtendaji au kusitisha zoezi fulani, je; ni wilaya ngapi anaweza kujua zinaendeshawa vipi, zina matatizo yapi, na ni ngapi anaweza kuzitembelea katika kipindi cha miaka mitano, na ni amri ngapi anaweza kutoa na kufuatilia utekelezaji wake?
Tatizo linalojitokeza katika wilaya moja linaweza kuwa ni ishara kwamba kuna matataizo ya aina hiyo hiyo katika wilaya zote nchini. Watu wetu wanazo tabia zinazofanana, mazoea ya utendaji yametufanya tujenge utamaduni unaoshabahiana, na mara nyingi tunaambukizana udhaifu kama vile wizi, ubadhirifu, uzembe na kutokujali.
Hivyo, matatizo yetu yanaweza kupatiwa majawabu ya jumla iwapo tutaketi na kuyajadili kama nchi na kuyatafutia dawa badala ya kutegemea amri za kiimla.
Ukoloni ulikuwa ni mfumo wa hovyo, wa nchi moja kuitawala nyingine, lakini pamoja na maovu yao yote, wakoloni walituachia utaratibu wa utendaji serikalini ambao uliwafaa wao wakati wakitutawala na ungeweza kutufaa sisi pia, tukifanya marekebisho kidogo. Cha kustaajabisha, ni kwamba yale maovu ya wakoloni tumeyakumbatia, wakati yale machache mazuri tumeyatupilia mbali.
Hebu tuirejee, tuiangalie mifumo yetu ya utawala, tuirekebishe. Tusifanye ‘fasta fasta’ kwani bado tupo hapa kwa karne kadhaa zijazo, miaka milioni kadhaa. Tunakimbilia wapi; tunakimbilia nini

Source: Raia mwema

No comments:

Post a Comment