WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, December 27, 2012

MAGGID MJENGWA MWANDISHI BORA WA HABARI ZA JAMII WA MWAKA 2012



  • HII KULINGANA NA MAPITIO YALIYOFANYWA NA BLOG YA UKADIRIFU NA MUNGUPAMOJANASI.
Mwanazuoni mmoja aliwahi andika kuwa “I know Mjengwa personally and have always known him to be fair and honest when it comes to news reporting, never even shying from his sometimes very  opinionated columns released in the press”.

Kama umeshawahi kupata na kusoma makala mbalimbali za mwandishi Maggid mjengwa katika magazeti ya Raia Mwema, na Kwanzajamii  kwa kweli utakubaliana na mimi kuwa Ndugu Magid amekuwa ni mwandishi ambaye amesaidia sana kuelimisha jamii katika hoja mbali mbali za maendeleo hata pale hoja zake zilipokuwa zikipingwa na watu wengine lakini aliendelea kusimama katika ukweli kwa faida ya Jamii ya Tanzania na mwisho wa siku ukweli unabaki kuwa ukweli.
Makala zake zimetumiwa na blogs nyingi katika kuhabarisha jamii ya Tanzania waishia popote pale duniani.
Amekuwa ni mwandishi ambaye amekuwa akiandika na kujishughulisha sana na maisha ya jamii za kawaida na wakati na kukosoa utendaji wa serikali katika mazingira yeyote yale bila hata kuuma uma akiwa anasimamia ukweli.
Amekuwa anajitahidi sana kuelimisha jamii bila kusimamia upande wowote wa siasa hata kama anajijua ni mpenzi wa mwanasiasa au chama gani.
Hebu tuangalie baadhi tu ya nakuu zake ambazo zimetokana na kazi zake mbalimbali:

BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI: TAFSIRI YA MAGGID MJENGWA ( MAKALA, RAIA MWEMA).

“Kijana, hatukuandika bei, maana, gharama ya ukweli mzima ni uhai wako. Je, uko tayari kulipa?” Kijana yule akatimua mbio. Nyuma aliacha vumbi. Hakuwa tayari kulipa gharama ya ukweli mzima. Yumkini ukweli utakaousema mwanadamu waweza usiwafurahishe wachache, walakini, ukawa wenye kuleta tija, furaha na matumaini kwa walio wengi. Mimi nitasena hapa ukweli wangu, kuwa Baraza jipya la mawaziri ni mabadiliko ya sura ya Baraza lakini si mabadiliko ya mfumo uliosababisha udhaifu wa kiutendaji ikiwamo ‘madudu’ yale tuliyoyaona bungeni hivi karibuni.”
“Ushauri kama huu unafundisha tu si wanasiasa hata jamii kuelewa kuwa hata kama kesho  CUF au CHADEMA wakiingia madarakani kwa mfumo huu huu, nao, kwa kiasi kikubwa, watafanya hivi hivi. Ndio maana ya kusisitiza, kuwa, tulilo nalo sasa ni tatizo la kimfumo ambalo ndiyo chimbuko la utendaji mbovu wa kuanzia mawaziri na walio chini yao. Ni mfumo unaomfanya waziri, awajibike zaidi kwa chama chake badala ya taifa kwa ujumla wake”.
Gulio la mafisadi makala ya Raia mwema/ Spika Makinda ‘amechemsha’ Raia Mwema 217
“Tulipo sasa ni kwa baadhi ya viongozi wetu kuigeuza nchi yetu kuwa gulio la mafisadi. Kwamba kila mwenye uwezo atafute mtaji. Awahi nafasi ya uongozi itakayomsaidia kuingia gulioni. Huko ni mahala pa kufanya biashara, si kuwatumikia wananchi. Kwa bahati mbaya, hata rasilimali zetu wanazipeleka gulioni. Ili kuinusuru nchi yetu, sote kwa pamoja. Bila kujali itikadi zetu za vyama, tuna lazima ya kulifunga gulio hili Sasa”.
Miaka 51 ya Uhuru na maneno ya Mkapa makala Raia Mwema 272
 “Kuwapo kwa amani na usalama katika nchi, hujengeka katika misingi ya haki na usawa, misingi ya kuaminiana. Misingi ya kuheshimu haki na uhuru wa raia kutoa mawazo yao. Ni lazima kuwapo misingi imara ya demokrasia. Wananchi ni vema wakawaamini viongozi wao, na viongozi pia ni vizuri wakawaamini wananchi wao. Na ili viongozi waaminike, ni lazima wawe wakweli na wawazi na Wawe waadilifu”.
Haya ni mambo ya msingi kabisa kuyatafakari. Hii ni nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Ni lazima tuaminiane. Tulio wengi tuna mapenzi ya dhati na nchi yetu. Kama taifa, miaka 51 ya Uhuru inatutaka tutafakari kwa kina juu ya mustakabali wa taifa letu”.

Mgomo wa madaktari na Muhimbili kukosa nyuzi za kushonea kwenye upasuaji! 225
 “Maana, haitakuwa busara kuliacha suala hili likapita kama yanavyopita mengine ilihali limegharimu maisha ya Watanzania. Na kubwa zaidi kwa sasa, ni kwa pande zote katika mgogoro huu kutambua; kuwa kwa sasa mvutano unaoendelea hautatoa mshindi, ni kwa vile, katika kilichotokea na kinachoendelea kufanyika sasa, sote, kama Taifa, tumeshindwa”.
“Huu ni wakati wa kutanguliza busara na hekima. Tufanye yote, lakini, njia mujarab ya kutanzua mgogoro huu uliopo sasa ni mazungumzo katika mazingira ya kuheshimiana, basi. Kinachoonekana sasa ni kwa baadhi ya viongozi kuwa mbali na umma. Viongozi kuwa mbali na hali halisi.  Baadhi ya kauli wanazotoa zinadhihirisha umbali huo kati yao na wanaowaongoza”.   
Tanzania ina vyote kasoro Watanzania Toleo la 218
“Nimepata kuandika huko nyuma (Juni 16, 2004) kuwa Tanzania ina vyote, kasoro Watanzania. Niliandika; kuwa Tanzania ni nchi nzuri sana. Ni nchi ya kujivunia. Kwamba Tanzania ni nchi kubwa sana kwa eneo. Ni nchi yenye rasilimali nyingi; ardhi yenye rutuba, mito, maziwa, milima, mabonde, bahari na vivutio vingi vya asili. Hata hivyo, Tanzania ni moja ya nchi masikini sana duniani. Kwa nini? Ndiyo, kikubwa kinachokosekana Tanzania ni Watanzania. Tanzania tunayoijenga sasa ni mkusanyiko tu wa watu wa makundi mbalimbali wenye kwenda kwa staili ya 'kila mtu na lwake'. Idadi ya Watanzania wenye uzalendo na mapenzi kwa nchi yao inazidi kupungua. Ubinafsi umekithiri, na ubinafsi mbaya zaidi ni ule wenye kufanywa na viongozi.”

" Bila Utawala Bora, bila kuwa na demokrasia, bila kuheshimu Haki za Kibinadamu,  mafanikio ya kiuchumi hayatawezekana."
“Hakika hakuna uchumi unaokua bila uwepo wa utulivu wa kisiasa. Kina Jaji Warioba wahakikishe wanaleta Katiba itakayohakikisha, mbali ya mambo ya mengine, inatupa  Tume Huru Ya  Uchaguzi”

CCM Kama Barcelona! ( Makala, Raia Mwema)


“CCM nayo inaamini, siku zote, kuwa kuna njia moja tu ya kuendesha siasa katika nchi hii, na njia hiyo ni ya CCM”!
Hakuna busara nyingine yeyote kwa sasa bali ni kwa CCM kuruhusu na kuendesha kwa salama mchakato wa mabadiliko makubwa yanayotakiwa na umma. Mabadiliko hayaepukiki. Ni hali ya dunia kwa sasa. Ni kama wimbi la maji ya bahari. Limeshajikusanya. Kwa CCM chaguo ni moja tu, kuenenda na wimbi hilo la mabadiliko au kukubali kufunikwa nalo.

Hilo la mwisho laweza kuharakisha kifo cha CCM. Ni jambo baya, maana, hata kama Watanzania watachagua upinzani ifikapo 2015, nchi yetu inahitaji chama imara cha upinzani, na CCM inaweza kuvaa viatu hivyo”. 
“Nchi yetu inapita sasa katika kipindi kigumu tangu tupate uhuru wetu. Ni kipindi kinachowataka viongozi, na hususan viongozi wa kisiasa, kutanguliza hekima na busara badala ya jazba, chuki na visasi. Hayo matatu ya mwisho ni mambo maovu yenye kuambukiza kwa haraka”.
“Kamwe tusiruhusu jazba, chuki na visasi vitawale siasa zetu. Hii ni  nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Hakuna mtu, kikundi  au chama cha siasa chenye haki zaidi ya kuongoza nchi hii kuliko wengine wote”.
Mwandishi Ni Mjumbe, Hauawi- Makala Ya Maggid Mjengwa Raia Mwema September 7 2012
“Hii ni nchi yetu. Tutafanya makosa makubwa kuwaachia viongozi wa kisiasa pekee, jukumu la kulinda maslahi ya nchi yetu.  Tunapita sasa katika kipindi kigumu tangu tupate Uhuru.

Dunia imebadilika, na nchi yetu inapitia kwenye kipindi cha mabadiliko. Hakuna  mtu au chama cha siasa kinachoweza kuyazuia mabadiliko  haya. Kufanya hivyo ni kutuletea machafuko na kuvunja amani yetu. Tuna jukumu la kufanya tunayoweza, na kwa kutanguliza busara, kuipitisha salama nchi yetu katika kipindi hiki cha mabadiliko. Maana, tukiingia kwenye machafuko, basi, hakutakuwa na mshindi, maana, sote tutashindwa”.


Dhana ya uandishi wa habari:

Mwandishi Maggid Mjengwa ameendelea kusimamia ukweli kuwa vyombo vyetu vya habari vimekuwa vya kishabiki bila utumiaji wa taaluma ya kiuandishi, na tabia ya vyombo vya habari hususan magazeti kuibuka na vichwa vya habari vinavyoashiria moja kwa moja uchochezi. Maggid alitoa mfano kwamba “inaweza kutokea mtu mmoja ama mwislam au mkristo amefanya jambo la kukashifu dini nyingine. Sasa badala ya kuandika fulani kafanya hiki na kile, magazeti yanaibuka na vichwa vya habari tena kwenye kurasa za mbele vyenye mwelekeo wa kujumuisha kundi zima la dini fulani. Utasikia "Waislam wafanya fujo", au "Wakristo wakasirishwa". Aina hii ya uandishi italipeleka Taifa pabaya;


ukombozi wa waandishi

“Huko nyuma nimepata kuanzisha mjadala wa umuhimu wa kuwepo kwa ruzuku kwa vyombo vya habari ili navyo viweze kupata nguvu ya kuendesha shughuli zao ikiwamo hata uwezo wa kuwasafirisha wanahabari wao kwenye matukio badala ya gharama hizo za usafiri kutegemea ‘ bahasha’ za wanasiasa na wamiliki wa makampuni ya biashara, ambao , masharti yasiyoandikwa ya wao kutoa bahasha zao, ni namna wanahabari hao watakavyoripoti habari za kuwapamba na itakazowafurahisha watoa bahasha”.

“Naam, wanahabari unganeni. Huu si wakati wa kulilia huruma za watawala ikiwamo wanasiasa. Huu ni wakati wa kupambana kudai ruzuku ya Serikali kwa vyombo vya habari. Ni ruzuku, pamoja na mauzo ( kama ni magazeti) na matangazo ndivyo vitakavyo wafanya muwe huru. Vinginevyo, mtaendelea kuachana na jukumu la kuutumikia umma wa Tanzania na badala yake mtabaki kuwatumikia wanasiasa, wafanyabiashara na makampuni makubwa”.

Hatari ya siasa kuchanganyika na dini Raia Mwema 260
Watanzania tuliwashuhudia baadhi ya viongozi wa kidini; Uislamu na Ukristo, wakitumia nyumba za ibada, si kwa kazi ya kiroho, kazi ya kuhubiri yaliyo mema kwa mwanadamu, bali walifanya kazi ya siasa. Kazi ya kuhutubia mambo ya siasa na kutoa maelekezo ya kisiasa ya moja kwa moja.

Hayo yamefanyika misikitini na makanisani. Ni hatari! Jambo hili linaiweka rehani amani ya nchi yetu. Linahatarisha umoja wetu wa Kitaifa. Maana, makanisani na misikitini wanakusanyika Watanzania wa itikadi tofauti za kisiasa, na wengine ni watoto, hawajawa tayari kupokea hotuba za kisiasa, bali watoto wako tayari kupokea mahubiri na mafundisho ya kiroho.

Naam, ni ukweli sasa, kuwa dini imejichanganya na siasa. Na huu si mseto mwema kwa nchi yetu.

Udhaifu wa JK - Tafsiri ya Maggid Mjengwa



“Kuna hoja mezani juu ya udhaifu wa JK, imetokea Bungeni.  Yumkini, kama mwanadamu, JK ana mapungufu na udhaifu wake, nani asiye na mapungufu na udhaifu? Lakini, tukimzungumzia JK kama taasisi ya ’ Urais’, namwona Rais anayejipambanua na waliomtangulia. Ni  kwa kujitahidi kufanya yale yalo nafuu na yenye manufaa kwa nchi yetu  kwenye mfumo dhaifu uliopo.   
 
Wanadamu tunapaswa kuhukumu dhamira ya mtu na si matokeo. Bado namwona JK kama kiongozi mwenye dhamira njema kwa nchi yetu. Nauona ujasiri ndani ya JK. Ni ujasiri wa kufanya yale ambayo, hata ndani ya chama chake hayakupata fanyika”

“Maana, katika jamii, mabadiliko yanapaswa yaendane pia na fikra mpya . Na jamii huingiwa na mashaka na kukosa imani pale fikra mpya zinapotekelezwa na watu wale wale ambao hawataki kabisa kuwaruhusu wengine  kushiriki uongozi wa nchi. Watu ambao bado miongoni mwao wanaamini kuwa tofauti za kifikra ni jambo baya. Kwamba upinzani ni uadui, ni uhaini. Kwamba wapinzani ni wa kuwakatakata na kuwatupa.  Sasa, katika hali ya sasa utawachinja wangapi ukawamaliza? Ni fikra za kiwendawazimu”.

 KATIBA NA UKOMO WA MALI 
“Kiongozi anayefahamu jinsi watu mitaani na vijijini wanavyoathirika na vitendo vya ufisadi hatopata kigugumizi kukemea na kulaani ufisadi kila anapopata fursa ya kufanya hivyo”.
“Tuna baadhi ya viongozi wenye utajiri wa ajabu kushinda hata hao wafadhili wanaotupa misaada. Yote hii inatokana na ubinafsi na uchoyo wa viongozi hawa. Wako tayari nchi inunue vifaa vibovu vya mamilioni ya dola za Marekani ili mradi wao wamehakikishiwa 10% yao. Katiba iweke wazi, kuwa kutakuwapo na ukomo wa kiwango cha fedha ambacho kiongozi wa kuchaguliwa au mtumishi wa umma anaweza kutoa kama zawadi kwa jamii.  Kinyume chake iwe ni kosa la jinai. Naam, Katiba mpya itusaidie kuwafanya viongozi wetu wafukuzie zaidi maendeleo ya wananchi kuliko mikate yao. Inawezekana”

kwa niaba ya Blogs za ukadirifu na mungupamojanasi tunakutakia kila la kheri katika mwaka 2013; uwe ni mwaka mwingine kwako ambao utaendeleza utashi wako na uwezo wako wa uandishi kwa faida ya Jamii ya Tanzania; KEEP IT UP;

No comments:

Post a Comment