WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, December 5, 2013

Tunakaribia hitimisho la Tume ya Katiba

warioba_3e352.jpg
Muda uliotolewa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kumaliza kazi yake ya kutayarisha Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya na kuikabidhi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sasa unakaribia ukingoni.
Baada ya Rais Kikwete kuiongezea Tume hiyo muda wa mwisho wa wiki mbili hivi karibuni, sheria inaitaka Tume hiyo iwe imewasilisha Rasimu hiyo kwa mamlaka husika katika kipindi cha siku 60, ambazo zinamalizika mwishoni mwa mwezi huu.
Itakumbukwa kwamba mara ya kwanza Tume hiyo iliongezewa muda wa siku 45 mwezi Oktoba, mwaka huu. Kwa kuwa sasa imeongezewa wiki mbili, maana yake ni kwamba itakuwa imeongezewa jumla ya siku 59. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 iliyounda Tume hiyo inasema Rais wa Jamhuri ya Muungano anaweza kuiongezea Tume hiyo muda usiozidi siku 60.
Hivyo, kisheria siku ya mwisho ya kukabidhi Rasimu hiyo ni Desemba 30 na Rais hana tena mamlaka kisheria ya kuiongezea muda Tume hiyo nje ya siku hizo 60.Kwa maana hiyo, Tume lazima ifanye kazi usiku na mchana kuhakikisha inamaliza kazi zake katika muda huo.
Kwa kuwa Bunge Maalumu la Katiba linakutana mwanzoni kabisa mwa mwaka ujao kuijadili Rasimu hiyo na kufanya marekebisho yatakayowezesha kupatikana kwa Rasimu ya Tatu ya Katiba kabla haijapigiwa Kura ya Maoni, hakuna tena uwezekano wa kuiongezea Tume muda zaidi, hata kama Bunge lingekuwa tayari kukutana kwa dharura kuifanyia marekebisho Sheria hiyo ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013.(P.T)
Hiyo ndiyo changamoto kubwa inayoikabili Tume hiyo hivi sasa. Sote tunajua kuwa, mara ya kwanza iliomba kuongezewa muda na kupewa siku 45 baada ya kutingwa na kazi ya kuratibu na kuchambua maoni ya wananchi waliojitokeza kwa wingi kutoa maoni kuliko ilivyotarajiwa.
Mara hii imeomba muda zaidi na kupewa wiki mbili, baada ya mjumbe wa Tume hiyo, Dk Sengondo Mvungi kuvamiwa na kujeruhiwa vibaya na majambazi na baadaye kufariki dunia.
Kifo cha ghafla cha Dk Mvungi kilisababisha kusitisha kazi za Tume, kwani kwa zaidi ya wiki mbili ndiyo iliyokuwa ikiratibu shughuli zote za matibabu yake ndani na nje ya nchi na baadaye maziko.
Alikuwa kitovu na mmoja wa mihimili mikubwa ya Tume, kiasi kwamba yeye kama mwanasheria wa kipekee na nguli katika masuala ya katiba ndiye aliyekuwa akitegemewa na Tume katika utayarishaji wa Rasimu zote mbili za Katiba Mpya. Tume siyo tu ilitikiswa na kifo hicho, bali pia ilighadhabishwa na upotevu wa kompyuta yake iliyoporwa na majambazi ikiwa na kumbukumbu muhimu kuhusu mchakato huo wa Katiba Mpya.
Hiyo ndiyo hali ya kusikitisha inayoikumba Tume hiyo. Hapana shaka kwamba kuiongezea muda Tume hiyo hakukutokana na uzembe kwa upande wake, bali mazingira yaliyojitokeza bila kutazamiwa na kuathiri kazi zake kwa namna moja ama nyingine.
Kwa vile bado ni mapema mno tangu kifo cha Dk Mvungi, hatutarajii wajumbe wake kuwa na hali ya utulivu kisaikolojia kutokana na kumpoteza mwenzi wao huyo.
Hata hivyo tunawasihi wapige moyo konde na kurudi kazini ili waweze kuwasilisha serikalini Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya muda uliopangwa. Matumaini yetu ni kwamba wananchi wote watawaunga mkono.

source: mjengwa blog

No comments:

Post a Comment