WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, December 9, 2013

Dk. Slaa: Nakwenda Kigoma Mjini,nikipigwa risasi mipango ya Mungu

 
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amesema wanaodai asikanyage Kigoma Mjini wanapoteza muda wao kwani hatishwi wala haogopi na hata ikitokea amepigwa risasi na kufa Mwenyezi Mungu atakuwa ameridhia hivyo.
Ametoa  msimamo huo jana wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Malumba Jimbo la Kasulu Mjini kwenye mkutano wa hadhara.

“Kama ni kutishiwa maisha mimi si mara kwa kwanza, lakini hata ikitokea nimepigwa risasi Mwenyezi Mungu atakuwa ameridhia, binadamu hawezi kufa kama Mungu hajaruhusu, sasa unaogopa nini?,” Alisema na kuhoji Dk. Slaa.

Dk. Slaa ambaye alikuwa akijibu watu walioandamana juzi Kigoma Mjini na kumtisha asikanyage Kigoma, alisema hawezi kuacha kutetea wanyonge eti sababu kuna watu wanataka asikanyage Kigoma.

“Hao wanaofanya hivyo hawawatakii mema Watanzania wanyonge, naomba wajue Dk. Slaa haogopi, mlinzi wangu siyo hawa wenye bunduki mlinzi wangu ni Mungu ambaye yupo juu,” alisema.

Dk. Slaa alisema wanaodai asikanyage Kigoma mjini watambue nchi hii hakuna mwenye hakimiliki bali kila mtu ana haki ya kufika mahali popote.

Alisema toka mwaka 2011, amekuwa akitembea vijijini, wilaya, majimbo na mikoa na kwamba tatizo watu wanahisi amekwenda Kigoma kwa sababu ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ambaye mwezi uliopita alivuliwa nafasi ya Unaibu Katibu Mkuu wa Chadema kwa tuhuma za kukisaliti Chama.

Kwa upande wake, Ofisa wa Chadema wa Sera na Utafiti, Mwita Waitara, alisema Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kigoma, amtafute na kumkamata mtu aliyetangaza katika maandamano ya jana Kigoma mjini kwamba atamuua Dk. Slaa akikanyaga Kigoma mjini “OCD wa Kigoma asiseme viongozi wa Chadema makao makuu badala yake amtafute aliyetishia kumuua Dk. Slaa hadharani,” alisema.

Alisema Chadema inafahamu njama zote hizo zinafanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwamba vitisho hivyo haviwezi kumzuia Dk. Slaa kwenda Kigoma Mjini.

Dk. Slaa leo ataendelea na ziara yake katika Mkoa wa Kigoma kwa kutembelea Jimbo la Buhigwe, kesho atatembelea Jimbo la Kigoma Kaskazini na kesho kutwa Kigoma Mjini.

AWASHUKIA POLISI
Katika hatua nyingine, Dk. Slaa amewashukia polisi kwamba waache ushabiki wa kisiasa na kama wanaona siasa inalipa, wavue magwanda (sare) na kupanda kwenye majukwaa ya kisiasa.

Alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara na wananchi wa vijiji vya Kitanga na Kwaga vilivyopo Jimbo la Kasulu Vijijini.
”Polisi acheni kutumika katika siasa na kama mnataka siasa vueni magwanda yenu mpande jukwaani ili tupambane kuliko hivi sasa mnavyotumiwa na Chama tawala,” alisema.
Dk. Slaa alisema baadhi ya askari wamekuwa wakiwabambikizia kesi na kuwapa mateso makubwa viongozi na wanachama wa Chadema wa mikoa ya Kanda ya Magharibi ili kuwapunguza nguvu.

Alisema mfano katika kijiji cha Kwaga, viongozi 15 wa serikali ya kijiji hicho wamekamatwa na kufunguliwa kesi ya mauaji na kwamba polisi watambue kuwa wanapofanya vitendo hivyo wanajenga chuki kwa wananchi.

Dk. Slaa alisema polisi lazima watambue kuwa nchi ilipata uhuru ili kila mtu aishi kama Mungu alivyomuumba maana Mungu hakumuumba mtu ili apate matatizo.

Alisema kumekuwa na unyanyasaji mkubwa wa wanachama na viongozi wa Chadema ambao wengine wamejeruhiwa kwa kuwekewa `spoko' za baiskeli na chupa sehemu za siri.

Alikumbushia kuwa hata bomu lililopigwa Arusha wakati wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani, Chadema ina ushahidi lilirushwa na polisi.

Alisema kutokana na unyanyasaji huo, Chadema itawawekea mawakili viongozi na wanachama wote waliofunguliwa kesi za kubambikiziwa kutokana na masuala ya kisiasa.

Aidha, alisema kuanzia sasa polisi watakaobainika kunyanyasa raia, watafunguliwa kesi kama wao na si kama Jamhuri kwa sababu Jamhuri haikumtuma kutesa watu.

Katika hatua nyingine, alisema Chadema inajipanga kuwa na mabalozi wake nchi nzima ili kila mwanachama anayepata tatizo lolote liwe la kifamilia linalohitaji usuluhishi, aende kwa balozi wa Chadema.

Wakati huo huo, jana jioni Dk. Slaa alishindwa kuhutubia kwa muda wa dakika 20 baada ya vijana takribani 10 wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Zitto, kuingia katika uwanja wa Kigwanamo mjini Kasulu wakiwa na mabango na kupiga kelele wakisema `Zitto, Zitto,. Zitto....

Hata hivyo, polisi waliwatawanya kwa mabo ya kutoa machozi na Dk. Slaa akaendelea kuhutubia. Lakini bada ya muda mfupi, mkutano huo haukuedelea kutokana na mirindimo ta mabomu hayo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment