WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, December 22, 2013

Tambwe amfunika Okwi, Yanga majanga matupu


Nahodha wa Simba, Haruna Shamte akinyanyua juu kombe baada ya kuifunga Yanga 3-1 katika mchezo wa Nani Mtani Jembe. P

Dar es Salaam. Mshambuliaji Amis Tambwe ameitibua sherehe ya utambulisho wa Emmanuel Okwi baada ya kupachika  mabao mawili wakati Simba ilipoichakaza Yanga 3-1 katika mchezo wa ‘Nani Mtani Jembe’ jana kwenye Uwanja Taifa, Dar es Salaam.
Mrundi Tambwe  alifunga mabao mawili huku Awadh Juma akifunga bao moja kwa Simba kabla ya Okwi kufunga bao la kufutia machozi kwa Yanga.
Tambwe aliwainua mashabiki wa Simba dakika ya 13 baada ya kupokea pasi nzuri ya Said Ndemla akiwa peke yake na kupiga shuti pembeni kwa kipa Juma Kaseja.
Baada ya Simba kupata bao mashabiki wa Yanga walikaa kimya hali iliyomfanya mwenyekiti wao Yusuf Manji kusimama na kuwataka washangilie huku akionyesha vidole vitano. Jambo lililowafanya mashabiki wa Simba kuanza kuzomea kwa nguvu.
Tambwe alipatia Simba bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 43 baada ya Ramadhani Singano kuchezewa vibaya na David Luhende, kabla ya kuhitimisha kwa bao la tatu dakika ya 60, akitumia vizuri uzembe wa Kaseja kupachika bao la tatu.
Manji aliinuka kwenye kiti chake na kwenda kumkumbatia Zaccaria Hanspope na kuondoka uwanjani hali iliyowafanya mashabiki wa Simba kumzomea.
Okwi aliingia akitokea benchi na kuifungia Yanga bao la kufutia machozi dakika ya 79, akimalizia vizuri krosi ya Haruna Niyonzima.
Mashabiki wa Simba walikuwa wakiwakejeli wenzao wa Yanga kwa kuwaambia waendelee kusajili wachezaji wa Simba faida yake wameiona.
Baada ya kukabidhiwa kombe mashabiki wa Simba walizunguka nalo, na wengine wakisukuma gari la Hanspope huku wakiimba ‘Okwi, Okwi, Okwi..’
Katika mchezo huo Yanga walionekana kuwa na presha na kucheza zaidi kibinafsi kuliko kitimu kulinganisha na wapinzani wao Simba.
Yanga waliondoka kabisa mchezoni baada ya bao la Simba na kuwaacha viungo Mkude, Henry Joseph, Chombo wakifanya watakalo katika kuanzisha mashambulizi ya vijana hao wa Msimbazi.
Beki wa Yanga, Luhende alikuwa na bahati ya pekee kwa kukosa kupewa kadi nyekundu baada ya kumkwatua kwa nyuma winga Simba, Singano na kusababisha penalti iliyofungwa na Tambwe.

Beki Kelvin Yondani alipewa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Singano dakika ya 74 na mwamuzi Ramadhan Ibada.
Kocha wa Simba, Zdravko Lugarusic alikuwa kivutio uwanjani hapo kutokana na mambo yake na kushindwa kutulia sehemu moja katika muda wote wa mchezo.
Pamoja na kutompa kadi nyekundu mwamuzi wa mchezo huo, Ibada kutoka Zanzibar alishindwa hata kumwonyesha kadi ya njano Luhende kwa kitendo chake hicho.
Simba iliwapumzisha Joseph, Ndemla, Chanongo, Tambwe na kuwaingiza Singano, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Uhuru Seleman wakati Yanga katika kipindi cha pili iliwatoa Haroub, Kiiza, Kavumbagu na kuwaingiza Simon Msuva, Okwi, Hassan Dilunga.
Mabadiliko hayo hayakuweza kuwasaidia Yanga walioshindwa kabisa kuelewana huku wachezaji wake wakionekana wakicheza bila ya malengo na kupoteza kasi yao ya kawaida.
Mashabiki wa Yanga baada ya kufungwa bao la tatu kutokana na uzembe wa Kaseja waliinuka kwenye viti na kuanza kuondoka.
Pia, Jerryson Tegete aliyekuwa amekaa benchi baada ya bao hilo alimwinua kipa Deo Munishi  kumtaka aende kudaka, lakini kocha Brandts alikataa kufanya mabadiliko hayo. Mashabiki wanne wa Yanga walizimia na kuondolewa na machela uwanjani, huku wengine wakizingira basi la wachezaji wao na kuwashutumu kwa kucheza chini ya kiwango.
Yanga waliingia uwanjani saa na robo, huku mshambuliaji wake Okwi akizunguka uwanja wa mzima kuwapungia mashabiki waliofurika uwanjani hapo.
Mashabiki wa Yanga waliamka kwa shangwe kwa kitendo hicho cha Okwi kuwapungia, wakati wale wa Simba wengi walikaa kimya na wachache walimpigia makofi.
Vikosi
Yanga: Juma Kaseja, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub, Athuman Idd, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngassa, Hamis Kiiza.
Simba: Ivo Mapunda, Haruna Shamte, Issa Rashid, Joseph Owino, Donald Msoti, Johas Mkude, Henry Joseph, Haruna Chanongo, Hamis Tambwe, Said Hamis, na Awadh Juma

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment