WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, December 16, 2013

Nenda shujaa Mandela


Maofisa wa Jeshi la Afrika Kusini wakipiga saluti baada ya kushusha kaburini mwili wa Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela katika ibada ya mazishi iliyofanyika Qunu,
Qunu: Yametimia. Saa 6:45 kwa saa za Afrika Kusini (sawa na saa 7:45 za Afrika Mashariki) ni muda ambao pengine hautasahaulika katika historia ya nchi hiyo, kwani wananchi wake walishuhudia ukomo wa maisha ya Rais wao wa kwanza mzalendo, Mzee Nelson Mandela.
Ukimya ulitawala katika makaburi ya familia ya Mandela, Qunu, katika Jimbo la Eastern Cape, wakati mwili wa Mandela ukiwa umewekwa ndani ya jeneza lililotengenezwa kwa mbao na kwa ustadi mkubwa lilipokabidhiwa kwa viongozi wa mila za Kabila la abaThembu kwa ajili mazishi.
Mwili huo ulishushwa kaburini katika tukio la mazishi ambalo halikuwa wazi kwa waombolezaji wengine, isipokuwa kwa familia ya Mzee Mandela, Rais Jacob Zuma na viongozi wa kimila katika jamii hiyo ya Waxosa ambako Mandela anatoka. Hata hivyo, mazishi hayo yalionyeshwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni ya SABC.
Kwa mujibu wa mila na desturi za kabila hilo alipaswa kuzikwa mchana wakati jua likiwa utosini, muda ambao kama angekuwa hai, kivuli chake kingekuwa kifupi kuliko muda mwingine.
Mwili wa Mandela ulikabidhiwa kwa viongozi wa kimila na Majenerali wa Jeshi la Afrika Kusini (SANDF) baada ya kumpa kiongozi huyo heshima kubwa, sawa na ile ambayo hupewa kiongozi ambaye hufariki akiwa madarakani.
Kabla ya kukabidhi mwili huo, waliondoa bendera ya Taifa ya Afrika Kusini ambayo ilikuwa imefunika jeneza pamoja na vifaa vingine, ili kutoa mwanya kwa jeneza hilo kufunikwa kwa ngozi ya chui kama mila zinavyotaka.
Bendera na vifaa vilivyoondolewa vilikabidhiwa kwa familia ya Mandela.
Ni watu 450 tu kati ya zaidi ya 5,000 walioshiriki katika ibada ya mazishi, ambao walipata kibali cha kwenda makaburini na majina yao yalisomwa mmoja baada ya mwingine.
Mara baada ya mwili wa Mandela kukabidhiwa, Askofu Don Dabula, alifanya sala ya mwisho na alipohitimisha anga la Qunu lilishamiri sauti za helikopta tatu za kijeshi ambazo zilikuwa zimening’iniza bendera za Afrika Kusini.
Helikopta hizo zilifuatiwa na ndege nyingine sita ambazo zilikuwa zimerushwa zikitengeneza umbo la pembe tatu, matukio ambayo yalifanywa kwa heshima ya kiongozi huyo.
Kulikuwa na ukimya na wakati ndege hizo zikitokomea, baragumu lilipigwa wakati ambao mazishi rasmi ya Mandela yalikuwa ya kianza kwa taratibu za kimila.
Mapema Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma alisema wiki iliyopita imekuwa ni wiki ya uchungu, kwani kwa siku tisa za maombolezo watu wameomboleza kwa ukimya, vilio na nyimbo ikionyesha kuwa walifurahishwa na kumpenda Mzee Mandela.

Rais Zuma, Mjane wa Mandela, Graca Machel, Mtalaka wake, Winnie Medikizela pamoja na watoto, wajukuu, vitukuu na wanafamilia wengine, walikuwa wameketi viti vya mbele wakati taratibu zote za mazishi zilipokuwa zikiendelea.
Ibada ya mazishi
Ulikuwa ni wakati mgumu kwa familia ya Mandela ikiongozwa na Graca, Medikizela, watoto wake; Makaziwe, Zenani na Zindziswa, wajukuu; Mandla na Ndaba pamoja na ndugu jamaa na marafiki ambao walijawa na huzuni wakati wa ibada hiyo.
Vilio na nyimbo za maombolezo vilisikika tangu asubuhi wakati wa mchakato wa kuelekea kuanza kwa taratibu za mazishi na hali ya huzuni ilizidi miongoni mwa waombolezaji na wageni waalikwa kadiri muda wa mazishi ulivyokaribia.
Baadhi ya waandishi wa habari wa Afrika Kusini, polisi na wanajeshi, waliweka majukumu yao kando na kuomboleza hasa wakati mmoja wa marafiki wakubwa wa Mandela, Ahmed Kathrada alipokuwa akisoma wasifu ambao ulihitimishwa kwa maneno ya uchungu.
“Wakati Walter (Sisulu) alipofariki dunia, nilipoteza baba na sasa Mandela amefariki nimepoteza kaka, sijui ni nani nitakayemwendea,” alisema Kathrada ambaye alifungwa gerezani pamoja na Mandela kwa miaka 26.
Mishumaa 95 ambayo ni idadi sawa na miaka aliyotimiza Mandela, iliwashwa wakati wa ibada ya mazishi nyumbani kwake Qunu alikokulia, katika Jimbo la Estern Cape, umbali wa kilometa zaidi ya 1,000 kutoka Johannesburg.
Mandela alizaliwa katika Kijiji cha Mvezo eneo la Transkei, Julai 18, 1918 akiwa mtoto wa Nongaphi Nosekeni na Henry Gadla Mandela, ambaye alikuwa mshauri muhimu katika utawala wa abaThembu na alipewa nafasi ya kuwa Chifu wa Mvezo alipokuwa kijana.
Mazishi hayo yanahitimisha siku kumi zilizotangazwa na Rais Zuma kwa ajili ya maombolezo baada ya kufariki dunia Desemba 5, 2013 saa 02:50 usiku, nyumbani kwake Mtaa wa Laa Na:12, Houghton, Johannesburg.
Miongoni mwa wageni mashuhuri alikuwamo, Rais Jakaya Kikwete aliyeongoza ujumbe wa Tanzania ukimjumuisha Mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere.
Mama Maria alishangiliwa sana pale alipotambulishwa na Mmoja wa Waongozaji; Cyril Ramaphosa na baadaye Rais Kikwete.

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment