WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, December 9, 2013

Hakuna mahali pa kukanyaga’ msibani kwa Mandela

s b0103
.
Makazi ya Rais wa Kwanza mzalendo wa Afrika Kusini yaliyopo katika Mtaa wa Laa namba 12, Houghton ambako ndiko alikokuwa hadi alipokutwa na mauti, ni kama hapaingiliki kutokana na wingi wa watu, magari na vyombo vya habari kutoka sehemu mbalimbali duniani ambavyo vimeweka kambi katika eneo hilo, usiku na mchana kufuatilia safari ya mwisho ya kiongozi huyo.(HD)

Anga la mtaa huo na sehemu za jirani, limehanikizwa na sauti nyingi za nyimbo zikiongozwa na Wimbo wa Taifa wa Afrika Kusini 'Nkosi Sikeleli Afrika' (Mungu Ibariki Afrika), ukifuatiwa kwa zamu na nyimbo za kidini na zile za asili ambazo zinasifu ushujaa wa Mandela.

Katika lango la kuingia kwenye makazi hayo ya Mandela, kuna maombolezo ya aina yake kwani yameambatana na kitu ambacho kwa macho kinaonekana kama shamrashamra kwa nyimbo za sifa na kufurahia kile Waafrika Kusini wanachokiita kazi nzuri ya kutukuka ya Mandela aliyoifanya katika umri wa miaka 95 ya uhai wake.
Mwandishi wetui alitembelea makazi hayo ya Mandela jana na kushuhudia umati mkubwa wa watu wakifika nje ya nyumba yake kwa ajili ya kuomboleza; wakiweka mashada ya maua, mishumaa na kadi zenye ujumbe wa pole kwa familia yake.
Miongoni mwa waliokuwapo katika eneo hilo ni Mtanzania, Christer Mwageni na watoto wake; Sabina na Faraja.

Mwageni alisema: "Kwa jinsi hali ilivyo, huwezi kukwepa kuwa mwombolezaji, mimi na wanangu tulikuja hapa kutembea tu kwa siku tatu hivi lakini tumejikuta tukishiriki msiba na hata kama tungekuwa hatutaki kushiriki, uhalisia unatulazimisha".

"Kweli tuna mengi ya kujifunza, inaonekana msiba huu wa Mzee Mandela umewaunganisha zaidi Waafrika Kusini, maana wote bila kujali rangi wala kingine chochote, wanaonekana kuomboleza kwa dhati kutoka mioyoni kabisa."

Katika eneo hilo la Houghton, ulinzi umeimarishwa na polisi wako kila kona na wamekuwa wakiwaelekeza waombolezaji na watu wengine njia sahihi za kufuata hadi kuyafikia makazi ya Mzee Mandela kutoka na barabara nyingi za kuingia katika eneo kufungwa na nyingine kugeuzwa maegesho ya magari ya waombolezaji.

Kwa ujumla, pilikapilika ni nyingi, lakini katika lango kuu la kuingia makazi ya Mandela, ulinzi ni mkubwa na hakuna anayeruhusiwa kulikaribia isipokuwa wanafamilia, vingozi wa Serikali na watu wengine wenye shughuli maalumu.Soweto, Mandela Square

Hali kama hiyo ipo katika makazi yake ya zamani Mtaa wa Vilakazi Na: 8115, Orlando Magharibi, Soweto ambako kuna pilikapilika nyingi zinazoyahusisha makundi ya watu kutoka ndani na nje ya Afrika Kusini.Mandela aliishi katika Mtaa wa Vilakazi kabla ya kukamatwa na kuwekwa kizuizini na alirejea katika nyumba hiyo miaka 27 baadaye alipoachiwa huru na kuishi humo kwa siku kumi na moja kabla ya kuhamia katika nyumba ya aliyekuwa mkewe, Winnie Mandela katika eneo hilohilo la Soweto.

Kama ilivyo Houngton, katika eneo hilo pia ulinzi umeimarishwa na baadhi ya njia zimefungwa kutokana na wingi wa watu na magari. Vyombo vya habari kutoka kila pembe ya dunia navyo vipo vikiendelea kufuatilia maombolezo hayo.

Katika nyumba ya Soweto ambayo sasa ni makumbusho ya Mzee Mandela, idadi kubwa ya watu wanafurika kujifunza historia ya kiongozi huyo na nje vipo vikundi vinavyoimba nyimbo za maombolezo na kumsifu Mandela kwa ushujaa wake.
Eneo la tatu ni Mandela Square lililopo katika Jiji la Sandton, Johannesburg ambako kuna sanamu kubwa ya kiongozi huyo yenye urefu wa mita sita kwenda juu, 

likimwonyesha katika hali ya kucheza muziki. Iliwekwa katika eneo hilo, Machi 31, 2004.
Katika eneo hilo, pia ulinzi umeimarishwa na askari wanalazimika kusimamia jinsi watu wanaovyoingia na kutoka. Watu wamekuwa wakisimama katika msitari mrefu kupata fursa ya kupiga picha katika sanamu hiyo yenye uzito wa tani mbili na nusu (kilo 2,500).
Pembezoni mwa sanamu hiyo, kama ilivyo Houghton na Malakazi, limetengwa eneo maalumu kwa ajili ya watu wanaoomboleza kuweka maua, nembo, nyaraka na mishumaa.

Maombolezo ya kifo cha Mandela yanaingia katika siku ya nne leo na yataendelea hadi Jumapili ijayo ya Desemba 15 wakati kiongozi huyo atakapozikwa kijijini kwake Qunu, 

Mthatha Mkoa wa Eastern Cape

source: mjengwa blog

No comments:

Post a Comment