WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, December 21, 2013

Mawaziri wanne wang’oka


Dk Emmanuel Nchimbi 


Dar es Salaam / Dodoma. Ripoti ya Kamati ya Maliasili, Ardhi na Mazingira iliyowasilishwa jana asubuhi bungeni mjini Dodoma, imewang’oa madarakani mawaziri wanne ambao wizara zao zilishindwa kusimamia vizuri utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Kung’oka kwa mawaziri hao kulitangazwa bungeni jana usiku na Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyeeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ametengua uteuzi wao baada ya kuwasiliana naye kwa mashauriano akiwa nchini Marekani kwa matibabu.
Mawaziri waliong’olewa kutokana na ripoti ya kamati hiyo iliyoongezewa shinikizo na michango ya wabunge wengi ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa  Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
Waziri wa  kwanza kutangaza kujiuzulu alikuwa ni Kagasheki huku uamuzi wa mawaziri watatu kujiuzulu ukitangazwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Kagasheki alitangaza kujivua wadhifa huo sa 2:09 usiku alipokuwa akichangia majumuisho ya ripoti ya kamati hiyo iliyowasilishwa na mwenyekiti wa kamati hiyo James Lembeli ambaye ni Mbunge wa Kahama (CCM).
Katika maelezo yake Kagasheki alisema: “…Mimi ni mtu mzima nimesikia hisia nzito sana kwa waliyoyasema wabunge.  Rais Kikwete aliponiteua ilikuwa ni kwa furaha yake na operesheni hii, yaliyotokea yametokea hali ya wanyama huko si nzuri;
Mimi mwenyewe nimewasikia na nachukua fursa hii kuteremka ngazi hii ya uwaziri na nitachukua taratibu za kawaida kuijulisha sehemu inayohusika(Rais).
Baada ya Kagasheki kutangaza hatua hiyo, Spika aliwaita mawaziri Dk Nchimbi na Nahodha kuchangia hoja hiyo, hata hivyo hawakuwepo ndipo alipoitwa Dk Mathayo na kutoa maelezo yake.
Katika maelezo yake Dk Mathayo alisema kuwa ripoti hiyo haikumtendea haki kwani kamati ya Lembeli haikumwita kumhoji na kwamba hata ripoti nzima haikueleza kuhusika na kashfa hiyo. Hata hivyo akihitimisha hoja hiyo Lembeli alisema Dk Mathayo ameshindwa kusimamia mapendekezo tisa, yakiwemo matatizo    ya wafugaji aliyopewa na Rais Jakaya Kikwete Januari 18, 2006 alipoteuliwa kushika nafasi hiyo.
Akitoa maelezo ya kutenguliwa kwa uteuzi wa mawaziri hao, Waziri Mkuu Pinda alisema: “Niliona nimtafute mkuu wa nchi (Rais Jakaya Kikwete), nilimpa picha yote ya kinachoendelea, alikubali ushauri wa Bunge; ..amekubali kuchukua ya uamuzi wa kutengua uteuzi wao(mawaziri).”
Akihitimisha mjadala huo wa ripoti ya kamati yake, Lembeli alisema: “...Katibu Mkuu na watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii nao wawajibishwe kutokana na kuhusika kwao na unyama uliotokea kwenye mpango wa Operesheni Tokomeza Ujangili. Rushwa iliyopo ndani ya wizara hiyo ni kubwa inakusanywa kwa kutumia simu, hivyo Serikali izichunguze simu zao kuanzia leo.”
Awali hali ya hewa ndani ya kumbi wa Bunge jana ilichafuka baada ya wabunge kuchangia kwa hisia kali, wakitaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kujiuzulu sambamba na mawaziri wengine watatu.
Mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu ni wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
Mbunge wa Longido, Lekule Laizer (CCM), alienda mbali zaidi na kutaka Bunge livunjwe endapo Waziri Mkuu na mawaziri hao watatu watakataa kujiuzulu kwa lengo la kung’ang’ania madaraka.
Michango ya wabunge hao ilitokana na ripoti ya kamati ndogo ya uchunguzi ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira chini ya Mwenyekiti wake, James Lembele iliyowasilishwa bungeni jana.
Ripoti hiyo inayohusu Operesheni Tokomeza Ujangili (OTU), ilibainisha kuwapo mauaji ya watu 13 na askari sita, utesaji wa kutisha wa watuhumiwa, ubakaji, rushwa na uporaji wa mali za wananchi.
Hata hivyo pamoja na kamati ya Lembeli kumtaka Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David apime kama bado anastahili kuongoza wizara hiyo, wabunge walimsafisha.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), alisema hakuna jinsi ya kuonyesha namna wabunge walivyokasirishwa na vitendo hivyo zaidi ya Serikali nzima kwa maana ya Pinda kujiuzulu.
“Naomba Waziri Mkuu uchukue ‘political responsibility’ (uwajibikaji wa kisiasa) na siyo kwamba kwa kufanya hivyo anahusika la hasha… Kama hachukui hatua Bunge libebe dhamana hiyo,” alisema.
Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia alisema ripoti hiyo ya Lembeli imetaja kuwapo baadhi ya wabunge wanaotuhumiwa kwa ujangili na kuhujumu OUT akitaka kamati iwataje ndani ya Bunge.
“Bungeni kazi yetu, sisi Wabunge ni kuisimamia Serikali kwa hiyo wale wabunge waliotajwa kwenye ripoti watajwe ili nao wawajibike ili Bunge letu liwe na nia thabiti ya kuisimamia Serikali,” alisema Mbatia.
Wabunge waliochafua zaidi hali ya hewa kutokana na michango yao ya hisia kali dhidi ya Pinda ni Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.
Lugola alisema makosa ya operesheni hiyo yalianza mapema wakati operesheni ya kijeshi ilipopelekwa kwa raia na kusema; “Hainiingii akilini kwamba aliyekuwa ana command (kutoa amri) ni mwanajeshi.”
“Wakati operesheni hii ikitokea wanawake wanabakwa na watu wawili…Watu wameteswa, mwanaume mwenzetu amelazimishwa kufanya mapenzi na mti Waziri Mkuu ulikuwa wapi haya yakitokea?” alihoji.
Lugola aliongeza; ”Kwa utaratibu wa nchi yetu tumekupa kila aina ya usafiri kuanzia helikopta, ving’ora kila wakati vinalia ulikuwa wapi Waziri Mkuu wakati mambo haya machafu yanatokea?”
Alisema Vuai hawezi kupona katika suala hilo kwa kuwa wanajeshi ndiyo waliobaka, kuua na kujeruhi na ndiyo walioua mifugo kwa risasi na kwamba atapona katika Bunge hilo mbele ya haki hatapona. Vivyo hivyo alisema Dk Nchimbi hawezi kupona katika kashfa hiyo kwa vile askari polisi ndiyo walioua, kubaka, kuwapa watu vile na kuua mifugo akisema; ”Utaponea wapi Dk Nchimbi?”
Lugola alisema pamoja na ripoti ya kamati kumnukuu Kagasheki akidai alinyang’anywa mamlaka yote katika utekelezaji wa OTU, akihoji ni waziri wa namna gani aendelee kukalia kiti cha uwaziri.
“Nimeisoma ripoti hii hakuna mahali Dk Mathayo alipohusika anataka kutolewa kafara… Mifugo yake imeuliwa hahusiki na sera yeye anahusika na wafugaji waliouawa pamoja na mifugo,” alisema Lugola.
Hata hivyo Lugola alisema Dk Mathayo anahusika na uzembe kwa kuwa wafugaji imeuawa, mifugo imeuawa na kuhoji waziri huyo alikuwa wapi wakati hayo yakitokea ndani ya Tanzania.
“Naendelea kumshauri Rais kama tunaitakia mema nchi hii na kama tunataka CCM kiendelee kuaminiwa na Watanzania, Rais amfukuze Waziri Mkuu mara moja,” alisisitiza mbunge huyo.
Aliongeza kusema; “vv       Mawaziri wake hao hawawezi kukwepa hili, watu wanachukua ‘political responsibility’ kwani Maige (Ezekiel) alichukua Twiga porini?” alihoji na kuongeza kusema;
“Kama tunataka tuwe na Bunge lenye viwango, Bunge lisilokuwa na ‘double standard’ (upendeleo) na nyinyi watu wameua watu na nyinyi lazima muondoke ndiyo tutajenga heshima ya nchi hii,” alisema.
Lugola alenda mbali na kusema endapo Rais atashindwa kumfukuza Pinda katika wadhifa wake huo, yeye atakuwa wa kwanza kupeleka hoja bungeni ili wabunge wapige kura ya kumng’oa Waziri Mkuu.
Kwa upande wake, Msigwa alisema wabunge wanapopendekeza Waziri Mkuu aachie ngazi hawana chuki naye, lakini kwa madudu yaliyotokea chini ya usimamizi wake ni lazima awajibike.
“Na kama mnatuheshimu, mheshimiwa Waziri Mkuu ungekuwa unatayarisha makaratasi saa hizi unaandika barua za kujiuzulu, tukufanyie sherehe ya kukuaga na nyie wa chini yake mfuate,” alisema.
Msigwa alienda mbali zaidi na kumnyooshea kidole Vuai kwamba ana rekodi mbaya kuanzia Zanzibar na kwamba dhambi ya damu ya mauaji ya raia huko Pemba inamlilia na kumfuata hadi Bara.

“Hata sisi tunasema hamkuhusika ‘direct’ (moja kwa moja) lakini hapa tunazungumzia uhai wa watu na watu waliokufa siyo wanachama wa CCM wala wa vyama vya upinzani…Tutangulize utaifa,” alisema.

Mbunge huyo alisema siku zote cheo ni dhamana na kwamba wasingependa Chadema itakapochukua nchi iwapeleke mawaziri hao Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, iliyopo The Heague nchini Uholanzi, kwa kuwa hawatapona.

Lekule ndiye aliyepigilia msumari wa mwisho aliposema endapo Bunge litamaliza mkutano wake huo bila kuwapo mawaziri watakaowajibika, basi Rais alivunje Bunge ili ufanyike uchaguzi mwingine.

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment