WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, December 11, 2013

Kili Stars yafa, lakini kiwango

 
Mshambuliaji wa Tanzania Bara, Mbwana Samata akiwatoka mabeki wa Kenya, Joackins Atudo (kulia) na Aboud Omar kwenye Uwanja wa Nyayo jana. Kili Stars ililala 1-0.
Licha ya timu ya Taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) kumiliki mpira kwa dakika zote 90, imeshindwa kutinga fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji baada ya jana kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Kenya (Harambee Stars).
Baada ya kupata bao hilo la dakika ya nne, mabeki wa Harambee Stars walihakikisha Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu hawagusi mpira kwa kuwathibiti vilivyo, huku wakicheza mashambulizi ya kushtukiza.

Kwa matokeo hayo sasa Kili Stars itashuka uwanjani Alhamisi kucheza dhidi ya Zambia (Chipolopolo)  kuwania nafasi ya mshindi wa tatu baada ya Wazambia hao nao kukubali kipigo cha mabao 2-1 katika nusu fainali nyingine iliyofanyika jana wakicheza dhidi ya Sudan.

Chipolopolo na Kili Stars awali zilikuwa kundi moja na mechi iliyozikutanisha zilitoka sare ya bao 1-1.

Harambee ilipata bao lake pekee kipindi cha kwanza kupitia kwa Clifton  Miheso katika dakika ya nne baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Ivo Mapunda aliyeshindwa kulimiliki shuti la Francis Kahata.

Dakika mbili baada ya bao hilo, nusura Kenya waandike la pili, lakini Miheso akiwa amebaki yeye na Ivo, shuti lake lilikosa macho baada ya kupaisha, huku dakika ya 22, Kipa Dancan Ochieng wa Harambee akifanya kweli kwa kupangua mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Mrisho Ngasa.

Kama Amir Kiemba angekuwa makini katika dakika ya 55, angeweza kuipatia Kili Stars bao la kusawazisha, lakini alichelewa kuruka kuunganisha krosi ya Erasto Nyoni.

Ulimwengu kipindi cha pili aliachia shuti kali ambalo liligonga 'posti' ya bao, na kurudi uwanjani, hiyo ikiwa nafasi nyingine ya Kili kushindwa kusawazisha.

Nafasi pekee kwa Kili Stars tena, ilikuwa dakika ya 88 baada ya Samatta kuwatoka mabeki wa Harambee lakini shuti lake halikuwa na macho baada ya kupaa juu ya lango.

Awali mechi hiyo ilikuwa ipigwe Uwanja wa Machakos majira ya saa saba mchana, lakini mvua kubwa ilinyesha na kusababisha dimba hilo kujaa maji na baada ya mwamuzi wa mchezo huo, Thiery Nkurunzinza kutoka Burundi na wasaidizi wake kuukagua, alitoa taarifa kwamba haufai kwa mchezo huo ndipo uongozi wa Cecafa ukatangaza rasmi kuhamishia Uwanja wa Nyayo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment