WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, December 9, 2013

Wabunge waache itikadi za vyama kwenye masuala mazito ya kitaifa

Maoni ya Katuni
 Bunge la Jamhuri ya Tanzania ni bunge la Watanzania wote bila kujali tofauti za itikadi za vyama wanavyoviwakilisha,  ijapokuwa zipo hoja za msingi zinazohusu vyama vyenyewe.
 
Lakini pia zipo hoja nzito ambazo zinagusa maslahi ya taifa ambapo wabunge wanatakiwa wazijadili kwa maridhiano na kuachana na masuala ya vyama.
 
Mwishoni mwa wiki hii,  Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwataka wabunge kujenga umoja wa kushirikiana bila kuingiza itikadi zao za vyama wanapojadili masuala mazito na ya msingi kitaifa, ili kuweza kutengeneza na kuibua masuala yenye maslahi kwa Watanzania.
 
Kutokana na malumbano yaliyojitokeza wakati wa kujadili Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2013, ambao Waziri Mkuu Pinda alisisitiza kuwa haujakiuka Katiba kama ilivyokuwa ikidaiwa, alisema muswada huo ulitungwa kwa kauli moja na mamlaka iliyopewa Bunge.
 
Kauli hiyo ya Waziri Mkuu Pinda ilitolewa wakati akifunga mjadala wa muswada wa sheria ya kura ya maoni, akisisitiza kuwa Bunge  hilo ni la Watanzania, akasema ni vyema yanapokuwapo masuala mazito, yajadiliwe na wabunge wote kwa kuangalia zaidi maslahi ya nchi kuliko umuhimu wa vyama ambavyo wabunge wanavyoviwakilisha.
 
Wabunge wengi wamekuwa na mwelekeo wa kujenga na kutetea hoja zinazolinda sera na maslahi ya vyama vyao, wanasahau kwamba baadhi ya hoja kama hii ya sheria ya kura ya maoni ya Katiba Mpya ni suala nyeti la kitaifa, ambalo kimsingi linatakiwa kujadiliwa kwa mtazamo wa maridhiano thabiti.
 
Pinda aliwakumbusha wabunge kuwa wapo bungeni kwa ajili ya maslahi ya Watanzania, na si kwa ajili ya kuwakilisha vyama vyao. 
 
Aidha, maneno ya kupeana vijembe ndani ya bunge ni katika kunogesha mazungumzo, ila visivuke mipaka na kuharibu misingi yenyewe iliyowaweka.
 
Kwa ajili ya kuweka msimamo wa maamuzi ya pamoja ndani ya Bunge, Waziri Mkuu alisema anatamani kwa siku zijazo za Bunge, liwe mfano wa kutengeneza kikundi kimoja kitakachokuwa na uwakilishi wa vyama vyote vilivyopo Bungeni, na kuzungumzia maudhui ya mijadala na miswada inayowasilishwa bungeni na kutoka na mtazamo mmoja wenye manufaa kwa wananchi.
 
Tunakubaliana kwa dhati na ushauri alioutoa Waziri Mkuu Pinda, tunaamini bunge letu lipo kwa ajili ya kutengeneza taratibu na sheria zitakazokuwa na tija kwa Watanzania wote. 
 
Tunaelewa pia wajibu wa wabunge katika kuikosoa na kuielekeza serikali kwa namna ya kupeleka huduma bora za maendeleo kwa wananchi. 
 
Wabunge wakijenga umoja wa kukubaliana katika masuala ya msingi, migongano ya kimaslahi na malumbano yasiyokuwa na maslahi kwa wananchi yataisha. 
 
Matukio ya misuguano ya hivi karibuni miongoni mwa wabunge  yameweka sura mbaya kwa wananchi. 
 
Ni wakati muafaka sasa kurejesha imani ya Bunge hili kwa wananchi kwa kufanya mijadala na maamuzi yenye tija kwa taifa.
 
Kama ambavyo alisema Waziri Mkuu Pinda huko bungeni kuwa kwa kauli moja walikubaliana kuwa, kwa mamlaka ya Bunge waliweza kutunga Sheria yoyote kwa maslahi ya taifa, na kwamba wote wanafahamu kuwa suala la muswada wa sheria ya kura ya maoni ni jema na limezingatia taratibu zote za nchi.
 
Kinachotakiwa ni kuhakikisha mambo yanasonga mbele. Haipendezi kuona miswada muhimu ikiendelea kukwamishwa kutokana na malumbano yanayozingatia itikadi za vyama jambo ambalo litaturejesha nyuma na kuchelewesha maendeleo ya wananchi. 
 
Kinachotakiwa ni wabunge kushikamana na kufanya maamuzi ya pamoja kwa maelewano thabiti ili nchi isonge mbele.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment