WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, December 22, 2013

Maalim Seif Hamad awapa somo Chadema Na Romana Mallya


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka viongozi wa Chadema kutafakari upya kwa kuyaunganisha makundi yaliyopo ndani ya chama hicho ili waweze kuelekeza nguvu ya mapambano kwenye vyama vingine.
 
Hamad ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho alisema hayo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Tanganyika Parkers, Kawe jijini Dar es Salaam.
 
Mkutano huo pamoja na mambo mengine ulilenga kuwaeleza wanachama mambo mawili ambayo ni mchakato wa katiba mpya pamoja chaguzi zinazotarajiwa kufanyika ndani ya CUF.
 
Akizungumzia migogoro ndani ya vyama vya upinzani, Hamad alisema imekuwa ikiwakatisha tamaa Watanzania ambao wana kiu ya chama mbadala hivi sasa.
 
Alitoa wito kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuyaunganisha makundi yote waliyonayo ili washindane na vyama vingine.
 
Akielezea kuhusu mchakato wa chaguzi ndani ya CUF, Hamad alitaka wanachana kuhakikisha hawawapi nafasi mapandikizi ambao wamekuwa wakivuruga vyama.
 
Aliwaeleza wanachama kuwa, ili kuwapata viongozi bora lazima waachane na majungu, fitna wao kwa wao na makundi.
 
Kuhusu Katiba mpya, Hamad amemuunga mkono Rais Jakaya Kikwete kuwa, kabla ya bunge la Katiba kuanza kuwe na mkutano utakaowashirikisha wadau wote ambao utawezesha kuondoa tofauti zilizopo.
 
Alisema kwenda kwenye bunge la katiba huku kila mtu akiwa na msimamo wake, itasababisha kupatikana katiba isiyo ya Watanzania.
 
Alisema kuingia katika bunge bila kikao hicho kutafanya katiba itakayopatikana kuwa ya CCM kwa sababu wabunge wake ni wengi.
 
Katika hatua nyingine, Hamad ameitaka serikali kuhakikisha Watanzania wote wenye sifa hasa vijana kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.
 
Aliongeza kuwa Watanzania wengi hawana vitambulisho vya kupigia kura na wengine ndio wametimiza umri wa miaka 18.
 
Alisema serikali kwa namna yoyote inatakiwa kuangalia namna watakavyowawezesha  kupata haki hilo.
 
Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi ndani ya chama hicho, Abdul Kambaya alisema kuwa tatizo la nchi sio usalama wa Taifa, polisi bali ni utaratibu unaowaongoza.
 
Aliwaeleza wananchi kuwa wakitaka kuondoa matatizo hayo njia pekee ni kuing’oa CCM madarakani.
 
Naibu Katibu wa Jumuiya ya Vijana ya CUF (Juvicuf), Hamidu Bobali, alisema wabunge waliochukua fedha za safari bila kwenda walikokutakiwa wanatakiwa kufikishwa mahakamani.
 
“Tumeshtushwa na kauli ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwa, wabunge hao warejeshe fedha hizi, tunadhani adhabu ni kufikishwa mahakamani kwa sababu hizi ni kodi za Watanzania wanyonge,” alisema.
 
Jana, Mwenyekiti wa chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba katika kikao cha baraza kuu la uongozi wa Taifa, alitoa ushauri kwa Chadema kuwa sio muda muafaka wa kuendeleza migogoro badala yake washirikiane katika kuandaa katiba ya Wananchi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment