WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, December 19, 2013

Tume ya Katiba kukabidhi rasimu ya pili Desemba 30

 
 
Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba.

Dar es Salaam.Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakabidhi rasimu ya pili ya Katiba kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, Desemba 30, mwaka huu.

Makabidhiano hayo yatafanyika katika hafla itakayofanyika katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam baada ya Tume kumaliza kazi yake ya kuiandaa.

Rasimu hiyo ya pili inatolewa ikiwa imepita miezi saba tangu tume hiyo ilipotoa rasimu ya kwanza ya ambayo ilijadiliwa katika Mabaraza ya Katiba yaliyokaa kuanzia Julai 12 mpaka Septemba 2 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Ibara ya 20 (2) ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, mara baada ya Rais kukabidhiwa rasimu hiyo, itachapishwa katika Gazeti la Serikali na kwenye magazeti mengine ndani ya siku 31.

Pia katika kipindi hicho, Rais anatakiwa kuitisha kikao cha Bunge Maalumu la Katiba kwa ajili ya kupitisha rasimu iliyopendekezwa. Kutokana na hali hiyo, kuna uwezekano mkubwa kuwa Bunge la Katiba litaanza vikao vyake Februari, 2013.

Taarifa ya Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashid iliyotolewa jana ilieleza kuwa Tume hiyo itakabidhi rasimu hiyo kwa Marais Kikwete na Dk Shein katika hafla itakayohudhuriwa na viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, taasisi za kidini, asasi za kiraia na wananchi wa kawaida.

Tume hiyo ilitakiwa kumaliza kazi ya kuandaa rasimu ya pili Desemba 15 mwaka huu lakini Rais Kikwete aliiongezea siku 14 zaidi hadi Desemba 30, mwaka huu.

Hatua hiyo ya Rais Kikwete kuiongezea muda tume hiyo ilikuwa ya pili. Mara ya kwanza iliomba kuongezewa muda wa siku 45, kuanzia Novemba Mosi hadi Desemba 15, mwaka huu. Kabla ya kuomba kuongezewa muda mara ya kwanza, ilitakiwa kukamilisha kazi yake Novemba 30.

Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaelekeza Tume hiyo kufanya kazi kwa miezi 18 licha ya kuwa inampa Rais mamlaka ya kuiongezea muda usiozidi siku 60.

Hatua ya Rais kuiongezea muda kwa mara ya pili, ilitafsiriwa kama kutoa fursa kwa wajumbe wake kujipanga upya baada ya kifo cha mwenzao, Dk Sengondo Mvungi kilichotokea Novemba 12, mwaka huu huko Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa baada ya kujeruhiwa kwa mapanga.

Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 3, 2012 kwa kukusanya maoni ya wananchi, iliandaa rasimu ya kwanza iliyotolewa Juni 4, mwaka huu.
Mambo yanayosubiriwa kwa hamu
Baadhi ya mambo yaliyopendekezwa na tume hiyo katika rasimu ya kwanza ambayo yanatarajiwa kuibua mjadala iwapo yatabaki kama yalivyo, kuondolewa au kuongezwa katika rasimu ya pili ni pamoja na muundo wa Muungano.

Baada ya Tume kupendekeza mfumo wa Muungano wenye Serikali Tatu, watu wa kada mbalimbali walitoa maoni tofauti.

Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba alitetea kuwa katika mazingira ya sasa, mfumo wa Serikali Tatu haukwepeki kwa maelezo kuwa utasaidia kuondoa hofu ya Zanzibar kumezwa kama ilivyojengeka kwa Wazanzibari wengi na wananchi wengine wa Tanzania Bara.

Mambo mengine yaliyomo katika rasimu ya kwanza yaliyozua mjadala ni pamoja na mawaziri kutokuwa wabunge, kufutwa kwa viti maalumu, wabunge kugombea ubunge kwa awamu tatu pekee.

Mengine ni kuhojiwa kwa matokeo ya urais mahakamani, kufutwa kwa nafasi ya waziri mkuu, kupendekeza waziri yeyote mwandamizi ateuliwe kukaimu nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa Rais na Makamu wake hawapo nchini kutokana na sababu zozote zile.

Pia ilipendekezwa jumla ya wabunge wawe 75, kwa maana 50 watoke Tanzania Bara, 20 Tanzania Visiwani na watano watoke kundi maalumu ambao watateuliwa na Rais.

Katika rasimu hiyo, pia imependekezwa kusiwepo na uchaguzi mdogo, isipokuwa kama nafasi yake ni ya mgombea binafsi. Kama ni ya chama cha siasa, basi nafasi hiyo ijazwe na mtu kutoka chama chake.

Kuhusu madaraka ya Rais, tume hiyo ilipendekeza yabaki kama yalivyo, kwa uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu, pia ashirikiane na taasisi na vyombo vingine katika uteuzi.

Kuhusu Tume ya Uchaguzi, rasimu hiyo ya kwanza ilipendekeza jina la Tume ya Uchaguzi ya Taifa (Nec), libadilishwe na kuwa Tume Huru ya Uchaguzi.

Pia ilipendekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu (Supreme Court). Ilisema majaji wa Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani watateuliwa na Rais, baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment