WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, October 21, 2013

‘Uncle J’ Nyaisanga afariki dunia



Marehemu Nyaisanga ameacha watoto watatu ambao ni  Samuel, Noela na Beatrice. 

Morogoro/Dar es Salaam. Mtangazaji mkongwe nchini, Julius Nyaisanga ‘Uncle J’ (53), alifariki dunia jana mkoani Morogoro baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kisukari na moyo.

Meneja wa Matangazo wa Kituo cha Abood Media ya Morogoro, Abeid Dogoli alisema Nyaisanga alifariki dunia jana saa moja asubuhi katika Hospitali ya Mazimbu, Manispaa ya Morogoro alikokuwa amelazwa.

Nyaisanga alikuwa miongoni mwa wakuu wa idara katika Kituo cha Televisheni cha Abood Media.

Dogoli alisema kuwa taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwa marehemu Kihonda na kwamba wanatarajia kumsafirisha kwenda nyumbani kwao mkoani Mara kwa maziko ingawa taarifa zaidi zitatolewa kama kutakuwa na mabadiliko.

Akizungumzia kifo hicho, mke wa mtangazaji huyo, Leah Nyaisanga alisema hali ya mumewe ilibadilika ghafla kwa kuzidiwa ambapo juzi aliwahishwa katika Hospitali ya Mazimbu ambako alifikwa na mauti.
Marehemu Nyaisanga ameacha watoto watatu ambao ni  Samuel, Noela na Beatrice.

Naye Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Aziz Abood ambaye familia yake ndio wamiliki wa Kituo cha Abood Media, alisema kuwa amepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo wa meneja huyo aliyekuwa mchapakazi.

Nyaisanga aling’ara Radio Tanzania

Dar es Salaam (RTD) na Redio One.
Nyaisanga ni kati ya watangazaji waliong’arisha tasnia ya utangazaji nchini Tanzania na hata nje ya nchi.
Alianzia kazi RTD, pia aliwahi kufanya kazi katika Kampuni ya IPP akiwa kama mtangazaji na baadaye Mkurugenzi wa Radio One.

Pia alifanya kazi na Sauti ya Ujerumani (Deutsche Welle), Sauti ya America, Redio Japan na Ghana.

Alianza kujizolea sifa kwenye iliyokuwa Radio Tanzania Dar es Salaam na sasa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwenye miaka ya 1970.

Nyaisanga alikuwa mahiri zaidi katika vipindi vya burudani na kujizolea mashabiki wengi na alijijengea jina zaidi katika vipindi vya RTD kama Klabu Raha Leo Show, Misakato, Bendi Zetu, Top Ten Show, Disco Show na kusoma taarifa ya habari.

Pia alikuwa anatumika katika vipindi vingi vya idhaa ya biashara ya RTD kama Karibu Vijana, Chai Bora na kipindi cha BP.

Nyaisanga alikuwa na sifa ya kutangaza kwa mbwembwe na hata kuanzisha misemo mingi kama `ngoma za kuruka majoka’(break dance na robot), `ngoma za kufoka foka’ (rap), ngoma za kuruka misumari (reggae), ngoma laini (muziki wa taratibu) na `nyuzi nyuzi bin nyuzi’ (pale gitaa linapopigwa vizuri kwenye wimbo).

Watu waliokuwa karibu na Nyaisanga wanaeleza kuwa alianza utangazaji akiwa bado kijana mdogo baada ya kuhitimu masomo yake ya sekondari nchini Kenya ambako ndiko kipaji chake kilichomoza kwa mara ya kwanza.

Wakati sauti yake ilipoanza kusikika kwa mara ya kwanza katika mawimbi ya RTD mwishoni mwa miaka ya 1970, Nyaisanga alikuwa tayari ametengeneza ramani iliyoonyesha mwelekeo wa maisha yake ya utangazaji.

Alikuwa mpole
Kwanza alikuwa ni mtu mtulivu, lakini aliyependa kutaniana na kila mtu aliyejuana naye.

Pia alikuwa anasifika kwa urefu wake na mwendo wake wa madaha uliofanya ajizolee umaarufu. Kutokana na urefu wake alivuma kwa jina la utani la `Super Tall’ ingawa lile la `Uncle J’ ndiyo lilitamba zaidi.

Pia msanifu za gazeti hili, Joseph Kapinga ambaye familia yake iliwahi kumpangisha nyumba ya kuishi Nyaisanga katika maeneo ya Mwenge kijijini anasema kuwa kile anachoweza kumwelezea mwandishi huyo alikuwa muungwana na alipenda kusaidiana na wenzake.

“Kwa kipindi cha miaka mitano aliyokaa kwenye nyumba yetu, Nyaisanga hakuwahi kukorofishana na sisi, wakati wote alilipa kodi yake kwa wakati na sijawahi kusikia akikwaruzana na majirani zake,” alisema na kuongeza.

“Nakumbuka mara nyingi tulikuwa tunakaa naye kupata viburudisho kwenye maeneo ya Maryland na pale ilipokuwa zamani Baa ya Igongwe,” alisema Kapinga.

Watangazaji wenzake wanavyomzungumzia
Mikidadi Mahmoud `Brother Micky’
Mtangazaji mkongwe Mikidadi Mahmoud alisema kuwa alianza kumfahamu Nyaisanga wakati wakiwa RTD na baadaye walikuwa pamoja Radio One.

“Hizi taarifa zimenishtua kweli hasa ukizingatia kuwa mwenyewe hapa ni mdhaifu sasa na hizi taarifa naona hali yangu inazidi kuwa mbaya. Nimeshtuka sana. Nyaisanga nilimpokea Redio Tanzania na baadaye tumefanya naye kwa kipindi kirefu kabla ya kuachana tukiwa Redio One,” alisimulia Mikidadi.

Alisema kuwa Nyaisanga alikuwa mtangazaji mwenye uwezo wa hali ya juu na wakati wote alifanya kazi kwa kujituma huku akizingatia maadili ya kazi. Pamoja na kushiriki vipindi vingi vya burudani na taarifa za habari, Mikidadi anakumbuka kipindi kimoja ambacho anasema kuwa kilizusha gumzo kubwa kutokana na kuendeshwa vizuri na Nyaisanga.

“Unajua Nyaisanga alikuwa anaujua vizuri muziki hasa wa Congo na wa hapa kwetu nyumbani, nakumbuka wakati tukiwa Redio Tanzania kulikuwa na kipindi nadhani kilikuwa kinaitwa `Top Ten Band’ yaani bendi 10 bora. “Tulikuwa tunazitembelea bendi huko ziliko na kukirusha kipindi, sasa huyu jamaa alikuwa hodari kweli maana ndiye aliyekuwa anaongoza, alikimudu vizuri sana,” alisema na kuongeza:

 “Hizi FM redio zinahitaji vijana wenye kipaji na mimi wakati nilipoombwa kusimamia uanzishwaji wa Redio One sikutaka kufanya makosa, nikamchagua Nyaisanga kwa kuwa tayari nilijua uwezo wake. Nikamchagua pia Charles Hillary na Blandina Mugenzi tukaanzisha redio hiyo ambayo ipo hadi sasa.”

Masoud Masoud
Masoud Masoud alisema kuwa pamoja na  Nyaisanga kuwa mtangazaji wa redio, pia alikuwa amebobea katika kuchezesha disko (DJ).

Alikumbushia jinsi yeye na Nyaisanga walivyokuwa wakichezesha muziki wa disko katika klabu mbalimbali za usiku jijini Dar es Salaam. 

“Nakumbuka wakati nikiwa upande wa magazeti kwenye Kampuni ya IPP, mwaka 1996, Nyaisanga aliniita niende studio kuzungumzia kitu fulani kuhusu muziki, nilimkuta Taji Liundi akiendesha kipindi hicho. Kusema kweli siku hiyo nilimfunika Taji, basi tangu siku hiyo ikaamuliwa kile kipindi mie ndiye niwe nafanya,” alisema Masoud.

Aboubakary Liongo 
Liongo alimfahamu Nyaisanga kwa mara ya kwanza  wakati alipokuwa RTD.

Alisema kuwa wakati anaendelea kuomboleza kifo cha Nyaisanga jambo kubwa analoendelea kulikumbuka ni kuhusu alivyosaidiwa naye kutoka Radio Tanzania na kwenda kujiunga na Redio One.

Alieleza kuwa Nyaisanga ndiye aliyempokea yeye pamoja na mwenzake Pascal Mayalla wakati walipojiunga na RTD kwenye miaka 1990.

“Nyaisanga alikuwa kaka yetu mkubwa sana, nakumbuka mimi na Pascal wakati tunajiunga pale RTD,  Nyaisanga alitupokea vizuri na alitusaidia kwa mambo mengi. Lakini jambo lingine ambalo lazima nimshukuru yeye ni namna alivyonishawishi kwenda Redio One. Yeye ndiye aliyekuja kumwomba baba yangu ili nihamie Redio One,” alisema Liongo.
Imeandikwa na Lilian Lucas na George Njogopa.

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment