WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, October 21, 2013

Kama zali, ngoma droo


Kipa wa Simba, Abel Dhaira (kushoto) akiwania mpira na nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana. Timu hizo zilitoka sare ya 3-3. Picha na Michael Matemanga. 

Dar es Salaam. Bahati yao! Ndicho unachoweza kusema baada ya Simba kufanikiwa kulazimisha sare ya 3-3 dhidi ya  Yanga jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mabingwa watetezi Yanga, walianza kwa kasi mchezo na kupata mabao matatu katika kipindi cha kwanza kupitia Mrisho Ngassa na mawili ya Hamis Kiiza, lakini Simba waliamka kipindi cha pili na kusawazisha mabao hayo kupitia Betram Mwombeki, Joseph Owino na Gilbert Kaze.

Katika uchunguzi uliofanywa na Gazeti hili kabla ya mchezo huo ulibaini Simba wamekuwa wakifunga mabao mengi kipindi cha kwanza na Yanga wenyewe wameruhusu mabao mengi kipindi cha pili.

Yanga waliuanza mchezo kwa kasi na dakika ya nne, ambapo katika dakika ya 14 winga Ngassa aliwainua mashabiki wa Yanga baada ya kufunga bao akiunganisha krosi ya Kiiza iliyompita beki wa Simba, Kaze.

Katika dakika ya 35, mpira wa kurusha wa Mbuyu Twite uligongwa na Kavumbagu na kumkuta Kiiza aliyeusukumia wavuni mpira huo kirahisi.Pia katika dakika ya 45, Kavumbagu aliwatoka mabeki wa Yanga na kupitisha krosi fupi kwa Kiiza aliyefunga bao la tatu kirahisi.

Kocha wa Simba, Abdallah Kibaden atajutia uamuzi wake wa 4-4-2 kwa kuwaanzisha Chanongo, Singano, walioshindwa kurudi katikati kuwasaidia Humoud na Mkude kulinda kutokana na kuzoea kucheza kama winga.

Yanga walikuwa imara zaidi katikati ya uwanja wakiwa na viungo watatu Athuman Idd, Frank Domayo na Haruna Niyonzima pamoja na Kavumbagu aliyesaidia hivyo kuwafanya kuwa wanne na kuwafunika kabisa Mkude na Humoud.

Hata hivyo kipindi cha pili katika dakika ya 47 Kibaden aliwapumzisha Chanongo na Humoud na kuwaingiza Said Hamis Ndemla na William Lucian walioimarisha safu ya kiungo na kuirudisha Simba mchezoni.

Mshambuliaji Mwombeki aliipatia Simba bao la kwanza katika dakika ya 53, baada ya mabeki wa Yanga, Nadir na Yondani kufanya uzembe wa kumkaba Amis Tambwe na kutoa nafasi kwa mfungaji .

Dakika ya 57, Owino aliipatia Simba bao la pili akiunganisha kwa kichwa kona ya Singano kufanya matokeo kuwa 3-2.

Baada ya hali hiyo, kocha wa Yanga, Brandts alimtoa Kiiza na kumwingiza Simon Msuva, ambapo katika dakika ya 64 Ngassa alpiga shuti la karibu lililopanguliwa na kipa Abel Dhaira.

Yanga imeendeleza udhaifu wa kuruhusu mabao katika kipindi cha pili kwani kati ya mabao saba waliyofungwa msimu huu kabla ya jana, waliruhusu kuanzia katika dakika ya 49 mpaka 90, ndicho kilichotokea, baada ya Kaze kumalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Cholo katika dakika ya 83 na kuiandikia Simba bao la kusawazisha.

Akizungumza baada ya mechi kumalizika, kocha wa Simba, Abdalah Kibaden aliwasifu wachezaji wake kwa kucheza kwa kujituma na kufanikiwa kusawazisha.
Naye Brandts alisema wachezaji wake walicheza kizembe kipindi cha pili hasa sehemu ya kiungo.

Yanga iliwasili uwanjani saa 8:33, kupitia mlango wa kawaida, wakati watani zao Simba waliingia saa 8:35 kwa kupita geti lililopo upande Kaskazini walipo mashabiki wao.

Katika mchezo wa awali wa timu za vijana, Simba B na Yanga B zilimaliza kwa kutoka sare 1-1.

Vikosi

Simba: Abel Dhaira, Nassor ‘Cholo’ Masoud, Haruna Shamte, Kaze Gilbert, Joseph Owino, Jonas Mkude, Abdulhalim Humoud/ Lucian William, Ramadhani Singano, Amisi Tambwe, Betram Mwombeki/ Zahoro Pazi na Haruna Chanongo/ Said Hamisi.

Yanga: Ally Mustapha ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Athuman Idd, Mrisho Ngassa, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza/ Simon Msuva na Haruna Niyonzima.
source: mwananchi

No comments:

Post a Comment