WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, October 21, 2013

Kwanini Diamond tajiri, Gurumo masikini?

 
MWAKA 2005 nilikuwa nikipanda daladala na Naseeb Abdul (Diamond) katika kituo cha Shule Tandale Magharibi jijini Dar es Salaam. Wakati huo, sikuwa hata na wazo kwamba atakuja kuwa mtu maarufu katika muziki hata kushughulisha watu kutaka kujua zaidi kuhusu maisha yake.
 Wakati nikipanda naye daladala moja nikielekea kazini nilimuona kijana mdogo anayepotea, kwani alikuwa na nywele za rangirangi, nguo za kubana huku amevaa suruali chini ya kiuno maarufu kwa jina la ‘Kata K.’
Mkononi ameshikilia ‘CD’ za muziki huku midomo yake ikitikisika kutokana na kufuatisha muziki anaousikiliza kupitia spika za masikioni ‘ear phones’.
Baada ya hapo nikaanza kuona wimbo wake wa kwanza kwenye video, ‘Nenda Kamwambie’ kilikuwa kibao kizuri kilichompa umaarufu, ndipo alipoanza kunivutia kusikiliza nyimbo zake. Baada ya video ile sikumuona tena kituoni kama ada yetu, nikaanza kusikia anaendesha gari aina ya Toyota Celica.
 Kutoka mwaka 2006 mpaka sasa ni mfululizo wa mafanikio aliyoendelea kuyapata kijana huyu aliyezaliwa Septemba 28, 1988 mpaka kuwa mwanamuziki wa kwanza Tanzania kulipwa pesa nyingi kutokana na shughuli hiyo.
 Kutokana na utafiti uliofanywa na tovuti inayozungumzia masuala ya vijana www.teentz.com inasemekena ‘Diamond Platnamz’ anapata kiasi cha Sh Mil 16 kwa matamasha mawili anayofanya katika mwezi. Mbali ya mikataba minono aliyoingia na makampuni mbalimbali yanayonufaika kwa taswira ama sauti ya mwanamuziki huyo kijana, Diamond anaingiza fedha nyingi kila anaposafiri nje ya Tanzania na bara la Afrika kufanya matamasha ya muziki.
 Wakati Diamond, ambaye hajatimiza hata miaka kumi kwenye tasnia ya muziki kuna mtu mmoja anaitwa Muhidini Gurumo, amejishughulisha na muziki kwa takriban miaka 45 lakini kila alipokutana na swali hili kutoka kwa wanahabari kuwa kwa kipindi chote hicho muziki umemsaidia nini, jibu lake ni: “Bado hakuna ninachoweza kujivunia kupitia muziki, hali ya maisha ni ngumu.”
 Gurumo ambaye alizaliwa 1940 alianza muziki mwaka 1959 akiwa na bendi ya Kilimanjaro Chacha Band. Sasa ni takriban miaka 45, umri wa baba mwenye wajukuu lakini alichofanikiwa ni kujenga nyumba mbili na kupata shamba moja. Gari lenyewe alizawadiwa na Diamond mwaka huu baada ya kulalamika sana kwenye vyombo vya habari.
 Nini Tatizo
 Maalim Gurumo (Kamanda), analalamika kuwa wanamuziki wa kizazi kipya wanasifiwa sana na vyombo vya habari. Akisisitiza kuwa hawana ubunifu, nyimbo zao hazina athari katika jamii na hudumu chini ya mwaka mmoja zinapoteza taswira.
 Lakini amesahau kuwa wanamuziki wa sasa wengi wamejiajiri, kipindi hicho bendi nyingi zilimilikiwa na kampuni, taasisi ama mtu ambaye anapenda sanaa hiyo ya muziki.
 Lakini sasa wanamuziki wameamka, wanajimiliki wenyewe pesa wanazopata zinaingia mifukoni mwao.
 Mathalan tangu Diamond aanze kuimba ameshaingia zaidi ya mikataba kumi tofauti ambayo ilimnufaisha yeye kama Diamond, matamasha yake yanamnufaisha yeye, kikundi anachomiliki anakilipa kiasi wanachokubaliana kutokana na uwezo wa mwanakikundi.
Mwaka jana, 2012, Diamond aliingia mkataba na kampuni ya I-View Studios wa kusimamia kazi zake zote kwa miaka miwili. Huu ni mkataba ambao umemjengea heshima kubwa sana. Ingawa kiasi cha malipo kilifanywa siri lakini inaonekana ni mkataba mnono.
 Kampuni nyingine ya One Touch, ilifunga naye mkataba wa kuwa wasemaji wake. Yaani kila anachotaka kufanya ama kuzungumza kwenye jamii, ikiwa kuna kampuni inataka kufanya naye mazungumzo ya kibiashara, One Touch Company ndio watakaofanya kazi hiyo.
 Hilo tu linamfanya Diamond awe na uwezo mkubwa wa kupata fedha kutokana na muziki. Mara nyingine msanii anashindwa kujua thamani yake, anaweza kutaja kiasi kidogo cha fedha katika ‘dili’ kubwa. Lakini kwa kupata mtu wa kukusimamia kwenye mazungumzo ya kifedha lazima uwe tajiri.
 Aidha, bendi ambazo Maalim Gurumo amehama kutokana na sababu za kimaslahi hazipungui kumi, alianza na Kilimanjaro Chacha Band, Kilwa Jazz Band, NUTA Jazz Band, Mlimani Park, Safari Sound Ochestra, Rufiji Jazz, na nyingine nyingi kabla ya kumalizia muziki kwenye bendi kongwe ya Msondo Ngoma Music Band.
 Kote huko alizunguka kwa kutumia kichwa kitupu kujadili thamani ya sauti yake, hakuwa na mshauri wa masuala ya muziki ambaye atamwambia kutokana na thamani yako usikubali kuhama bendi hii ili kuenda bendi nyingine bila kupewa kiasi fulani cha fedha.
 Aliweza kuitwa baa akawa anakunywa bia na nyama choma huku anajadili mustakabali wa maisha yake na mkurugenzi wa bendi pinzani na anayofanyia kazi.
 Katika mazungumzo yake na wanahabari Maalim Gurumo aliwahi kutamka kuwa anatamani siku zirudi nyuma ili anufaike na muziki wake. Lakini nakataa, hata awe vipi kutokana na mfumo anaoutumia hawezi kuwa tajiri kama Diamond.
 Leo hii, Maalim Gurumo akiandaa tamasha na kuingiza Sh Mil 50, basi atakachoambulia ni asilimia  10 ya mapato ambayo ni Sh Mil 5, ambacho kitakuwa ni kiasi kikubwa kuwahi kukipata kwa tamasha moja tangu aanze kuimba.
 Lakini siku hiyohiyo Diamond akialikwa katika tamasha hilo la Gurumo ataondoka na Sh Mil 8 taslimu bila kupungua senti. Bado tofauti ipo kubwa.
 Aidha, mbali ya mapato ya stejini lakini Diamond ana mikataba minono na makampuni ya simu ambayo yanatumia nyimbo zake kama miito ya simu, ana mkataba mwingine mnono na kampuni ya Vodacom, ana mkataba na kampuni ya vinywaji baridi ya Coca Cola hata kufikia kujiita Coke Boy.
 Tukiwakusanya wanamuziki wa zamani kuanzia Mbaraka Mwinshehe mpaka kufikia Maalim Gurumo, bado hawawezi kufikia mafanikio ya muda mfupi aliyoyapata kijana mdogo Naseeb Abdul ‘Diamond’ ambaye hata ladha ya ndoa hajaionja kutokana na umri wake kuwa mdogo.
 Wakati Gurumo akijisifia nyumba mbili alizojenga kwa tamu, Diamond ana nyumba zaidi ya mbili ambapo moja amemjengea mama yake yenye thamani inayofikia zaidi ya Sh Mil 50.
 Pengine Gurumo ni mwanamuziki bora zaidi kuliko Diamond lakini mwenziye amemzidi kwenye ujanja wa kutafuta fedha
source: Raia  Mwema 

No comments:

Post a Comment