WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, October 16, 2013

Rais Kikwete ateta na viongozi wa vyama pinzani

1623604_orig_fd7fd.jpg

Rais Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Vyama vya upinzani na wasaidizi wao waandamizi muda mfupi kabla ya kuanza mazungumzo kuhusu rasimu ya katika ikulu jijini Dar es Salaam leo. Kutoka kushoto mbele Isaack Cheyo UDP, James Mbatia NCCR Mageuzi, Professa Ibrahim Lipumba CUF, Freeman Mbowe CHADEMA, Philip Mangula CCM, na Bibi Nancy Mrikaria aliyemwakilisha Mwenyekiti wa TLP Mhe.Agustine Lyatonga Mrema.Waliosimama Nyuma kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu CUF Bwana Julius Mtatiro,Mhe. Tundu Lissu CHADEMA, Bwana Martin Mng'ong'o NCCR Mageuzi ,Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Uratibu na Bunge William Lukuvi, Mhe.Habib Mnyaa CUF, Mbunge wa Ubungo Kwa tiketi ya CHADEMA Mhe.John Mnyika, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu Mhe.Steven Wassira na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Mathias Chikawe. (picha: Freddy Maro/IKULU).

TAARIFA KWA UMMA KUTOKA KURUGENZI YA MAWASILIANO IKULU

MKUTANO kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni umemalizika Ikulu, Dar Es Salaam, muda mfupi uliopita leo, Jumanne, Oktoba 15, 2013 kwa pande hizo mbili kukubaliana kama ifuatavyo:

Moja , kwamba vyama vyote vya siasa nchini vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha Sheria ya Kurekebisha

Sheria ya Mabadiliko ya Katiba viwasilishe mapendekezo yao haraka Serikalini ili ifatutwe namna ya kuyashirikisha mapendekezo hayo katika marekebisho ya Sheria hiyo.

Pili, kwamba vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba Mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano wa jinsi kwa pamoja vitakavyosukuma mbele mchakato huo kwa maslahi mapana ya nchi yao na mustakabali wa taifa. Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimepewa jukumu la kuratibu jambo hilo ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini.

Viongozi wa vyama vyama vya siasa waliokutana na Mheshimiwa Rais Kikwete ni Mheshimiwa Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF; Mheshimiwa Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA na Mheshimiwa James Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.

Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Mheshimiwa Philip Mangula, Mheshimiwa Isaack Cheyo ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa Chama cha UDP Mheshimiwa John Cheyo na Mheshimiwa Nancy Mrikaria ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa TLP Mheshimiwa Augustine Mrema. Waheshimiwa John Cheyo na Mrema wako nje ya nchi.

Wengine ambao wameambatana na wenyeviti wao ni Mheshimiwa H. Mnyaa na Bwana Julius Mtatiro wa CUF, Waheshimiwa Tundu Lissu na John Mnyika wa CHADEMA na Bwana Martin Mng'ongo wa NCCR-Mageuzi.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
15 Oktoba, 2013

No comments:

Post a Comment