WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, October 14, 2013

Kumbukumbu ya miaka 14 ya Mwalimu Nyerere leo


Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere
Wakati leo ikiwa ni  kumkukumbu ya miaka 14 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere , wadau mbalimbali wamemzungumia kiongozi huyo wakisema baadhi ya mambo aliyoyasimamia yametelekezwa.
Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Sayansi na Utawala toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, amesema kama nchi, tuna mambo ambayo tunaweza kusema tumeendelea kumuenzi na ambayo tumeshindwa.

“Kwanza ni muhimu kuelewa kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa ni zawadi kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla wake kwa aina ya uongozi aliyoutoa na misingi aliyoijenga kwa taifa,” alisema.

Alisema misingi aliyoiweka na ambayo imeendelea kuzingatiwa na awamu za uongozi zilizofuata ni ile ya usawa, umoja na mshikamano huku amani ikiendelea kulindwa.

Dk. Bana alisema pamoja na kuendelea kuenzi hayo mambo ya msingi, bado kuna maeneo ambayo tumepotoka na hasa katika masuala ya uchumi na kutolea mfano  kwa viwanda vingi ambavyo mwalimu alivijenga ambavyo vilikuwa vikitoa fursa ya ajira kwa Watanzania vimeuzwa.

Alisema katika nchi kama Tanzania, dola ilipaswa kusimamia uchumi wa nchi na si kuacha mikononi mwa sekta binafsi.

“Sekta binafsi ambayo inaweza ikatupeleka mbele ni ile ya vyama vya ushirika aliyoianzisha na kuilinda Mwalimu Nyerere. Vyama vya ushirika ndiyo vilivyopaswa kuwa sekata binafsi vinavyoshiriki kwenye umiliki wa rasilimali kama za gesi, mafuta na madini,” alisema.

Dk. Bana aliongelea vilevile nchi kupotoka katika eneo la kuongoza kuelekea umoja wa Afrika ambako mwalimu alikuwa mstari  wa mbele.

Alisema, kwa mfano katika suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania imebaki nyuma na badala ya kutoa uongozi imeacha kwa vijana kama akina Rais Yoweri Museveni, Uhuru Kenyatta na Paul Kagame.

Aidha, alizungumzia suala la marais  wastaafu kukaa kimya na kuachia mambo yaende isivyo siyo, tofauti na Mwalimu Nyerere aliyekemea mara moja pale alipoona mambo hayaendi sawa.

Dk. Bana alisema, ni muhimu kwa viongozi wastaafu kutokaa kimya pale masuala yanapoenda mlama kama mchakato wa katiba mpya.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),  Abdallah Bulembo, amewataka Watanzania kukumbuka mambo bora aliyoacha Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake.

Bulembo alisema Mwalimu Nyerere ndiye aliyesimamia kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya  siasa nchini.

“Tangu enzi za TAPA mwaka 1955 Hayati Mwalimu Nyerere alikuwa akisisitiza suala la elimu, malezi, utamaduni na mazingira. Mchango wake
unaonekana na unapaswa kuendelezwa na kuenziwa na siyo kupuuzwa,” alisema Bulembo.

Aidha, aliwataka watumishi wa serikali kuacha tabia ya kujisahau na kukaa ofisini na kukiuka maadili kutokana na ukweli kwamba haki bila maadili ni vigumu kupata ufanisi wa kazi jambo ambalo Mwalimu Nyerere alikuwa akilipigia sana kelele.

Mtafiti  wa Uchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Haji Semboja, alisema  baada ya kufariki k wa Mwalimu Nyerere baadhi ya mambo aliyokuwa akiyakemea yameendelea kuwapo.

Baadhi ya mambo hayo ni ubinafsi na tofati za kipato kati ya walionacho na wasionacho.

Alisema kwa sasa viongozi wengi hawana maadili tofauti na enzi za uhai wake, na kueleza kuwa wengi wao ni watoaji na wapokeaji wa rushwa.

Alisema  nguzo muhimu aliyokuwa anaisimamia Mwalimu Nyerere ya kujitegemea kwa sasa imevunjika, na kueleza kuwa nchi ina maliasili nyingi, lakini bado viongozi wanakwenda kukopa nje. Aliongeza kuwa  nchi bado haimuenzi Mwalimu kwa yale mazuri mengi aliyoyaacha na kuyakemea.

Imeandikwa na Raphael Kibiriti, Gwamaka Alipipi na Charles Lyimo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment