WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, October 1, 2013

Muswada wa Katiba kaa la moto

 
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),Jaji Fredrick Werema
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa na Bunge wakati wa mkutano wake wa 12 mwezi uliopita unaendelea kuipa wakati mgumu serikali kiasi cha viongozi wake kukwepa kuuzungumzia.
Hali hiyo imezidi kujitokea hasa baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kuitisha mkutano na waandishi wa habari wiki iliyopitana kueleza kushangazwa kwao na kipengele kilichopendekeza kuvunjwa kwa tume hiyo kabla ya mchakato wa kura maoni kuanza.

Jana, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema na Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, ambao ndiyo nguzo ya serikali katika kuwasilishwa kwa muswasda huo bungeni, ama walishindwa au kukwepa kujibu hoja za Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhusiana na kipengele hicho ambacho tayari kimepigiwa kelele siyo tu na Tume hiyo bali na wadau mbalimbali, ukiwamo muungano wa vyama vya upinzani vya Chadema, NCCR-Mageuzi na Cuf pamoja na wanaharakati, wanasheria na wadau wengine nchini.

Kwa mujibu wa shinikizo kutika vyanzo mbalimbali juu ya muswada huo, kipengele hicho mbali ya kuelezwa kuwa kimechomekewa kwenye sheria hiyo, pia inaelezwa kuwa ni kinyume cha sheria mama ya mwaka 2011 iliyoanzisha Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilisema tume iendelee kusimamia na kuratibu mchakato wa katiba mpya hadi kura ya maoni ili kusaidia kutoa elimu kwa wananchi.

Jaji Werema akizungumza na NIPASHE iliyotaka kujua ni kwanini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013 uliopitishwa na wabunge wa Chama Cha Maopinduzi (CCM) na Mbunge wa TLP, Augustine Mrema, katika mkutano wa 12, umependekeza kuvunjwa kwa tume hiyo, alijibu kwa kifupi kuwa yeye (Werema) hatungi sheria bali inatungwa na Bunge.

“Sheria inatungwa na Bunge siyo na mimi, kwa hiyo suala hilo siwezi kulitolea maelezo,” alisema Jaji Werema kwa kifupi  jana kisha akakata simu.

Kwa upande Waziri Chikawe alipoulizwa alisema hawezi kutolea maelezo suala hilo kwa kuzungumza kwenye simu na mtu ambaye hamuoni.

“Siwezi kuzungumza na suala hili na mtu ambaye simfahamu na wala simuoni, njoo ofisini kwangu,” alisema Chikawe jana.

Alhamisi wiki iliyopita, Jaji Warioba alilishangaa Bunge kwa kupitisha sheria mbili zinazokinzana kuhusiana na mchakato unaosimamiwa na Tume yake.

Jaji Warioba alisema kuwa wakati sheria mama iliyounda Tume ya Mwaka 2011 inatamka kuwa Tume iendelee kuwapo katika mchakato wote hadi pale kura ya maoni ya kupitisha au kukataa Katiba mpya itakapofanyika, muswada wa hivi karibuni unapendeza kuvunjwa kwa Tume kabla ya muda huo.

Alisema marekebisho yaliyofanywa katika mkutano wa 12 wa Bunge yanakinzana na sheria mama kwa sababu muswada wa sasa unataja muda wa Tume kumalizika pale itakapowasilisha rasimu ya katiba katika bunge maalum la katiba.    

Jaji Warioba alisema kuwa Tume yake inajua kuwa kazi ya kutunga sheria siyo ya kwake bali ni ya wengine na kwamba hata sheria inayoiongoza katika utendaji kazi wao waliikuta ikiwa imeshatungwa tayari na wahusika.

Aliongeza kuwa Tume yake inafanya kazi kwa mujibu wa sheria iliyo mbele yao.
Jaji warioba hata hivyo, alisema kwamba wakati Muswada wa Marekebisho unahitimisha ukomo wa Tume baada ya kuwasilisha rasimu katika bunge maalumu la katiba, sheria mama inawataka waendelee mpaka kwenye hatua ya kura ya maoni.

Alisema sheria mama inaitaka Tume iendelee mpaka kwenye hatua hiyo, ili pamoja na mambo mengine iweze kutoa elimu kwa wananchi.

“Sasa utafanya jukumu hilo kwa kutumia mamlaka ipi, wakati tayari shughuli zako zimefikia ukomo baada ya kuwasilisha rasimu kwenye bunge maalumu la katiba?” alihoji Jaji Warioba kwenye mkutano na waandishi wa habari ambao pia alieleza kuwa mchakato wa mabaraza la katiba uliingiliwa sana na wanasiasa kwa kuwapa maelekezo wanachama wao.

Ijumaa iliyopita ikiwa ni siku moja baada ya Jaji Warioba kueleza wasiwasi wa Tume kuhusiana na utata wa muswada uliopitishwa na CCM na Mrema huku wabunge wa CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi wakisusia mjadala na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge kwa siku tato mfululizo,  Waziri Chikawe alizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma na kusisitiza msimamo wa serikali kwamba ifikapo mwaka 2015 Katiba mpya itakuwa imekamilika na itatumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo.

Tangu muswada huo upitishwe, kumekuwapo na shinikizo kubwa kutoka kwa vyama vitatu vya upinzani na makundi ya wanaharakati.

Vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi na Chadema vimeshaungana kuupinga muswada huo kwamba utaleta katiba mbaya kutokana na mchakato mzima kuhodhiwa na CCM.

Wenyeviti wa vyama hivyo, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Freeman Mbowe (Chadema) wamekwisha kufanya mikutano miwili ya kadhara jijini Dar es Salaam na Zanzibar kwa lengo la kuwashawishi wananchi waupinge mchakato wa katiba.

Aidha vyama hivyo vimeazimia kuitisha maandamano Oktoba 10, mwaka huu na baada ya hapo kufanya mikutano ya hadhara katika mikoa yote nchini.

Kuvunjwa kwa Tume kabla ya kura ya maoni pia ni moja ya hoja zinazotumiwa na upinzani kupinga mchakato wa katiba kwa maelezo kuwa hatua hiyo itasababisha kutokuwapo na mjumbe halali wa Tume wa kwenda kutoa maelezo katika bunge la katiba ikiwa watahitajika kwa kuwa watakuwa wameshapoteza uhalali wa kuwa wajumbe.

Pia muungano huo unapinga muswada huo kwa kuwa hakuzingatia maoni ya Zanzibar kwa kuwa hawakushirikishwa kabla ya kuwasilishwa bungeni.

Muswada huu ndiyo ulikuwa chimbuko la ngumi kupigwa bungeni wakati wa mkutano wa bunge wa 12, ambao uliweka historia mpya mbele Naibu Spika, Job Ndugai, kwa kadhia hiyo kutokea ndani ya chombo hicho tangu uhuru mwaka 1961.

Ndugai amekuwa akitupiwa lawama kwa kushindwa kumudu kiti kiasi cha kusababisha kadhia hiyo ambayo imeibua lawama juu ya nafasi ya kiti cha spika wa bunge katika kusimamia kazi za bunge kutokana na hisia za kisiasa za chama chake kuonekena kukwamisha haki kwa upande mmoja wa bunge.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment