WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, October 7, 2013

Chadema, CUF, NCCR Mageuzi wakubaliana na JK

Lakini wataka waliompotosha Rais wawajibishwe
 
Washauri Rais akutane nao kabla ya Oktoba 10

Rais Jakaya Kikwete
Vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi , vimekubali ushauri wa Rais Jakaya Kikwete wa kutaka hoja ya Zanzibar kutoshirikishwa kutoa maoni irudishwe Bungeni.
Hata hivyo, vimetoa angalizo la kumtaka atumie kama sababu mojawapo ya kutosaini muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Aidha, vimemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu na Bunge), William Lukuvi, wawajibishwe kwa kumpotosha Rais kuwa Zanzibar ilishirikishwa kutoa maoni.
Viongozi wa Kamati ya Ufundi ya Ushirikiano wa vyama hivyo, walisema hayo wakati wakizungumza na waandishi wa habari jana makao makuu ya CUF jijini Dar es Salaam wakati wakitoa maoni yao kuhusu hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa juzi.
Mkurugenzi wa Habari wa Chadema, John Mnyika, alisema Rais atumie madaraka yake ya kwenye katiba ibara ya 97 (2) kuacha kusaini muswada huo na kutoa sababu za Zanzibar kutoshirikishwa.
“Suala la ushirikishwa wa Zanzibar ni la muhimu, kwa kuwa hii ni katiba ya Muungano, Rais amepewa maelezo yasiyo ya kweli kuhusu umuhimu wa Kamati ya Bunge Katiba, Sheria na Utawala kwenda Zanzibar kukusanya maoni ya wadau,” alisema Mnyika.
Kuhusu maandamano, Mnyika alisema kwa kuwa Rais amekubali kukutana na viongozi wakuu wa vyama hivyo, awaandikie barua ya kukutana nao kabla ya Oktoba 10, mwaka huu siku iliyopangwa kufanyika maandamano nchi nzima.
Alisema vyama hivyo vitaendelea na maandalizi kwa ajili ya maandamano yatakayofanyika nchi nzima na kwamba kama Rais atakuwa hajakutana na viongozi wakuu wa vyama, maandamano yao yatakuwapo kama walivyopanga.
Naye Mkuu wa Idara ya Taasisi za Dola na Vyombo vya Uwakikishi NCCR- Mageuzi, Faustine Sungura, alisema Rais awajibishe mawaziri hao, kutokana na kutoa kauli zinazokinzana katika suala la katiba.
Sungura alisema hotuba ya Rais ukiisikiliza na kuisoma kwa makini ina mitego kwa sababu hajaweka wazi kama atasaini muswada huo au la.
Mkurugenzi wa Habari CUF, Abdul Kambaya, alisema kama Rais atakutana na viongozi wakuu wa vyama hivyo, mapema, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Freeman Mbowe (Chadema), watasitisha maandamano yao.
Kimbaya alisema katika kipindi hiki ambacho wanasubiri wito wa Rais, wataendelea na maandalizi ya kuratibu maandamano hayo.
Vyama hivyo vimeungana kupinga muswada huo usisainiwe na Rais kutokana na baadhi ya vifungu kuingizwa kinyemela, Zanzibar kutoshirikishwa kutoa maoni na pia umehodhiwa na CCM.
Juzi Rais Kikwete, katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi alisema hoja ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau wa Zanzibar, irudishwe Bungeni ili wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi muafaka.

WASOMI, WANASIASA WASIFU HOTUBA YA RAIS JK
Hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa juzi na kugusia Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kuhusu suala la Zanzibar kurudishwa bungeni imesifiwa na baadhi ya wasomi na wanasiasa.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema Kikwete ameonyesha usawa na kuwapa Watanzania fursa baada ya baadhi ya watu kutaka kuwapotosha.
“Rais ameonyesha uwezo mkubwa na utashi wake kuhusiana na mchakato wa katiba mpya…wanasiasa walijichukulia suala hili kama lao pekee yao wakati katiba ni ya Watanzania wote hata mabao si wanasiasa,” alisema Dk. Bana.
Dk. Bana alisema, lazima wanasiasa wapinzani wapime kabla ya kuamua kama maandamano waliyopanga yafanyike ama la kwa maslahi ya Watanzania.
Alisema, kilichozungumzwa na Kikwete kuhusiana na kurejeshwa bungeni ili wabunge wazungumzie maoni ya wadau wa Zanzibar, ni suala la msingi na kutakiwa kumpongeza.
Naye Profesa Palamagamba Kabudi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema kinachotakiwa ni pande zote mbili kukaa katika meza moja kwani suala la katiba ni la wananchi wote.
“Suala la katiba haliamuliwi kwa wingi wa namba ama idadi ya watu, bali linatakiwa kukaa pamoja na kufikia muafaka wa wengi na wachache,” alisema Profesa Kabudi.
Aliongeza kuwa mchakato wa katiba ya sasa ni tofauti na ule wa miaka ya 1965, 1977, 1984 na 1992 ambao ulikuwa unaamuliwa na Rais pekee, lakini Kikwete ameonyesha njia kwa kuupeleka kwa wananchi na kumalizwa na wananchi wenyewe.
“Ni mara ya kwanza kwa wananchi kushirikishwa kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoundwa, hivyo lazima suala hilo limalizwe na wananchi wenyewe,” alisema.
Akizungumzia maamuzi ya Rais kutaka suala la Zanzibar lirudishwe Bungeni, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema anakubaliana na maamuzi ya ‘bosi’ wake kwa kurejesha suala hilo bungeni.
Vuai alisema wapinzani walikimbia suala hilo bungeni, lakini Kikwete ameamua kuwarejesha tena huko huko kwani ndiko muafaka unakopatikana.
“Suala la bungeni litamalizwa bungeni na wala si kwa maandamano, Rais Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa taifa CCM amefanya maamuzi ya busara sana,” alisema Vuai.
Akizungumzia suala hilo la Zanzibar, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika (Chadema), alisema kwa sababu Rais amekubali Zanzibar haijashirikishwa, basi anatakiwa kutumia madaraka ya Rais kwenye Katiba Ibara ya 97 (2) kuacha kusaini muswada huo.
“Kuhusu maamuzi kufanywa kwa awamu ya tatu kwenye Bunge la Katiba kwa kutumia wingi mdogo badala ya kutumia theluthi mbili na suala la kuchakachuliwa kwa kurasa, lazima Rais aangalie suala hilo,” alisema Mnyika.
Nao viongozi wa Chama cha Kijamii (CCK) na National Reconstruction Alliance (NRA), wameibuka kuushambulia muungano wa vyama vitatu vilivyopanga kufanya maandamano nchi nzima Oktoba 10, kushinikiza Rais asisaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Mwenyekiti wa CCK, Constantine Akitanda akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema vya Chadema, CUF na NCCR Mageuzi, havijaweka maslahi ya taifa mbele na badala yake vinataka kujiweka pabaya zaidi.
“Tumefanya utafiti na kubaini vyama hivi vinataka kusababisha katiba mpya isipatikane mwakani…tatizo lililopo hapa ni kuhodhi mchakato mzima,” alisema Akitanda.
Naye mwenyekiti wa NRA, Rashid Mtuta alisema wanasiasa wanatakiwa kutumia busara na hekima ili kupata wabunge wengi zaidi uchaguzi ujao kuliko kukimbilia kuandamana na kulalamikia mabadiliko ya muswada huo.
“Hawa wenzetu wanatumia mambo ya ajabu sana, inawezekana wenzetu wana mambo mengine nje ya amani ya Tanzania,” alisema Mtuta.
*Imeandaliwa na Thobias Mwanakatwe na Daniel Mkate  
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment