WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, May 7, 2014

Warioba ahimiza maridhiano Bunge la Katiba


Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba amesema wajumbe wa kundi la walio wengi linaloundwa na wabunge wa CCM na baadhi ya 201 katika Bunge la Katiba hawawezi kupitisha Katiba kwa kuwa hakuna maridhiano.

Jaji Warioba aliyasema hayo juzi usiku katika Kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na televisheni ya ITV na kusema kuwa lazima kuwapo na maridhiano.

Kauli hiyo imekuja baada ya kuwapo na kauli mbalimbali zinazosema kuwa akidi iliyopo ya wajumbe wa Bunge la Katiba inaweza kupitisha uamuzi wowote kwa mujibu wa Sheria za Marekebisho ya mabadiliko ya Katiba.

“Kwanza kilichotokea wajumbe walisahau kufanya kama ilivyokuwa kwenye tume, sisi tuliweka pembeni itikadi za vyama na kuweka mbele utaifa lakini Dodoma watu waliingiza siasa na kuanza kushindana,” alisema Warioba na kuongeza:

“CCM imeamua kupitisha yao, wale wengine wanatafuta njia ya kuzuia wasipate wingi wa kura na kuna uwezekano bila maridhiano tutapata matatizo katika mchakato...lazima kuwapo na maridhiano.”

Jaji Warioba pia alitoa angalizo kuhusu kutokuwapo kwa maridhiano, “Lakini kama wakienda hivi walivyopanga, wanaweza kukwama tu...haiwezi kupatikana Katiba kama kundi hili likipitisha, kundi lingine litadai, lingine likifanya hivyo, hawa watalalamika,” alisema.

Alisema awali Zanzibar iliingia katika matatizo na kupelekea hata kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa ajili ya kuleta utulivu kutokana na kusigana lakini kwa maridhiano yakamalizika.

“Binafsi nina wasiwasi mkubwa na Zanzibar na hata ukiangalia matusi yaliyokuwa yanaporomoshwa bungeni na Wazanzibari siamini kama maridhiano yatakuwapo.” Jaji Warioba alirejea kusema kuwa waliotoka bungeni kuna kila sababu ya kutafuta maridhiano nao kwa kuwa wasiporidhiana hapatakuwa na Katiba nzuri yenye sura ya Watanzania.

“Kwa hali iliyopo ni vigumu kupata theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar watakaokubaliana na hoja zao, ni vigumu kwani Wazanzibari wana mambo yao kwa hapa nisingependa tufikie huko ila kinachotakiwa ni maridhiano ili tupate Katiba ya Watanzania,” alisema Jaji Warioba.

Jaji Warioba aliwasisitiza wajumbe kufanye maboresho yaliyotoka kwa wananchi na yaliyopendekezwa na wao kuingizwa kwenye Katiba.

chanzo cha habari: mwananchi

No comments:

Post a Comment