WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, May 5, 2014

Theluthi mbili ilivyokwamisha nia ya kubadili rasimu



Kamati namba tano ni moja ya kamati 12 za Bunge Maalumu la Katiba, zilizoundwa na kuanza kuboresha Rasimu ya Pili ya Katiba, Machi 31 mwaka huu.
Tayari kamati zote zimeboresha Sura ya kwanza na Sita za Rasimu na kuwasilisha taarifa zake bungeni, ambako zimejadiliwa. Kamati hiyo namba tano ikiongozwa na mwenyekiti, Hamad Rashid Mohammed, haikuafikiana katika Ibara ndogo ya (1).
Hiyo imetokana na kura za Wazanzibari katika kuamua kipengele hicho, kutosha theluthi mbili lakini wakaangushwa na Watanganyika kwa kura zao kutofikia idadi hiyo.
Kwa upande wa Zanzibar, ibara hiyo ilifanikiwa kupata theluthi mbili ya kura za wajumbe wote. Hiyo ikimaanisha kuwa ibara hiyo ilishindikana kubadilishwa kama ilivyokusudiwa na maoni ya wengi.
Miongoni mwa wajumbe 53 wanaounda kamati hiyo ni Dk AshaRose Migiro, Aggrey Mwanri, Andrew Chenge, Gerson Hosea Lwenge, Lazaro Nyalandu, Dk Mary Nagu, Gregory Teu, Godfrey Simbeye, Musa Yusufu Kundecha, Dk Aley Soud Nasoro, Yasmin Yusufali Haloo, Ezekiah Oluoch na Jina Hassan Silima.
Wengine ni Joseph Selasini, David Kafulila Hawa Mchafu, Hamis Dambaya, Khamis Salum, Paulo Makonda, Rehema Said Shamte, Omar Yussuf Mzee, Asaa Othman Hamad, Mahmoud Thabit Kombo, Fatma Abdulhabib Fereji, Rashid Seif Suleiman, Ali Abdallah Ali, John Komba, Omar Nundu, Said Nkumba, Esther Matiko, Leticia Nyerere, Muhammad Amour Chombo na Thuwayba Idrisa Mohamed.
Pia wako Charles Kitwanga, Shadya Mohamed Suleiman, Luhanga Mpina, Dismas Bwanausi, Devotha Likokola, na Mgeni Juma.
Ibara ndogo (1) inasema, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi na Shirikisho lenye mamlaka kamili inayotokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, zilikuwa nchi huru.
Mapendekezo ya walio wengi ndani ya kamati hii, wakataka ibara ndogo hii ibadilishwe ili isomeke;
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi moja yenye mamlaka kamili, ambayo imetokana na muungano wa nchi mbili zilizokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa huru.
Kutokana na kukosekana theruthi mbili ya kura zilizopigwa na wajumbe wote kwa upande wa Bara, mapendekezo hayo hayakufanyika, ibara ikabaki kama ilivyo na hivyo Kamati ikalazimika kuiwasilisha tena bungeni kwa hatua zaidi.
Hata hivyo, ibara ndogo ya (2) na (3) za sura hiyo ya kwanza katika rasimu, zimepata theluthi mbili ya kura za wajumbe wote kutoka Zanzibar na Tanganyika.
Kwa nini wengi wanataka mabadiliko?
Waliotaka mabadiliko kwenye ibara ndogo ya kwanza wanataja sababu ya kwanza kuwa ni Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, kuwa msingi wa kuwa na Muundo wa Serikali mbili.
Wanasema katika makubaliano hayo, Zanzibar ilikubali kuhamishia sehemu ya mamlaka yake kwenye Serikali ya Muungano, huku iliyokuwa Tanganyika ikikubali kuhamishia mambo yake yote kwenye Serikali ya Muungano.
Wanasema Muundo wa serikali moja haukukubalika kwa sababu Zanzibar ni ndogo, iliyokuwa na watu 300,000, wakati Tanganyika ikiwa na watu 12 milioni. Hata kiuchumi, Tanganyika ilikuwa juu zaidi ya Zanzibar hivyo ingeonekana imemezwa na iliyokuwa Tanganyika.
Ikaonekana Zanzibar ibaki na utambulisho wake kwa maana ya serikali na vyombo vingine vya utendaji.
Kamati hiyo inasema ukweli huo, maudhui ya hati ya makubaliano na ikiwa changamoto zilizobainishwa kwenye muungano zikitatuliwa kisheria na kikatiba, serikali mbili ndiyo mfumo unaofaa kuendelea kuongoza Tanzania.
Wanapinga rasimu iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayopendekeza Mfumo wa Serikali tatu kwa maelezo kuwa ni mwendelezo wa Hati ya Makubaliano, wakisema hati hiyo ilikusudia kuanzishwa muundo wa serikali mbili.
“Waasisi walitia sahihi makubaliano ya serikali mbili, waliunganisha nchi mbili, hivyo kisheria na kisiasa hati hii haiwezi kurekebishwa na watu ambao hawakuasisi Muungano huu,” anaeleza Hamad Rashid Mohammed.
Mohammed anasema msingi wa muundo wa Serikali tatu unaopendekezwa na Rasimu, hauwezi kuwa hati hiyo ya muungano na kwamba ikiwa kuna nia ya kuunda aina hiyo ya muungano lazima kuwe na makubaliano mapya.
Sababu nyingine ambayo inaonekana kuwa na uzito wa aina yake, ni inayoeleza kuwa pendekezo la Serikali tatu halitekelezeki kwa kuwa Tanganyika haipo; mamlaka, uendeshaji na masuala yake yote yalikwishakabidhiwa kikatiba na kisheria kwa nchi inayoitwa “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” tangu mwaka 1964.

source ya Habari: mwananchi

No comments:

Post a Comment