WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, May 13, 2014

Ugonjwa wa dengue wazidi kutikisa nchi

Charles Pallangyo
Ugonjwa  wa homa ya dengue umeendelea kuwa tishio nchini kutokana na idadi ya watu wanaoambukizwa kuongezeka.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii jana ilitoa tamko ikisema kwamba idadi ya wagonjwa wa dengue imefikia watu 400 na vifo vya watu watatu na waliolazwa ni 13.

Aidha, wizara hiyo imesema Mei 9, mwaka huu idadi ya wagonjwa waliogundulika katika Mkoa wa Dar es Salaam walikuwa ni 60 kati ya hao, Manispaa ya Kinondoni 42, Temeke 14 na Ilala wanne.

Tamko hilo lilitolewa jana na jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Charles Pallangyo, kwa waandishi wa habari.

“Hadi sasa idadi ya wagonjwa ambao wamethibitishwa kuwa na ungonjwa huu ni 400 na vifo vitatu, hivyo wizara inapenda kutoa taarifa kwa umma juu ya mwenendo wa ugonjwa huu nchini,” alisema.

Alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu na kuwa dalili hizo huanza kujitokeza kati ya siku tatu na 14 tangu mtu alipo alipoambukizwa kirusi cha ugonjwa huo.

Aidha, aliwataka wananchi kusafisha mazingira yao ikiwa ni pamoja na kufukia madimbwi ya maji, kuondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vifuu  vya nazi, makopo ya maua na magurudumu ya magari.

Hata hivyo, Pallangyo alisema wizara  imejipanga kwa kutumia Timu ya Taifa ya Maafa na wadau mbalimbali zikiwamo halmashauri za miji kukutana mara mbili kila wiki kutathmini mikakati iliyowekwa na kuendelea kutoa elimu na uhamasishaji kwa jamii kupitia vyombo mbalimbali ikiwamo mitandao.

MTOTO AFA MUHIMBILI

Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Aminieli Eligaeshi, jana aliiiambia NIPASHE  kuwa usiku wa kuamkia jana.Alifafanua kwamba hadi jana, wagonjwa 65 wa ugonjwa huo walipokelewa hospitalini hapo na baadaye kuruhusiwa kurudi makwao.

MAT WAJA JUU

Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kimeitaka serikali kuhakikisha wanawekewa kinga kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo.

Rais wa MAT Dk. Primus Saidia, aliliambia NIPASHE kuwa wanatarajia kukutana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuhakikisha inanyunyizia dawa katika hospitali zote kuhakikisha mazalia ya mbu hao wanaoeneza ugonjwa huo wanakufa.

Pia, alisema wanataka kuwepo kwa dawa za mbu kwa ajili ya kujipaka ambazo zitatumiwa na  wauguzi wanapokuwa wodini.

Dk. Saidia alisema vifaa vya kupimia ugonjwa kwa sasa vimeisha, hali ambayo inawafanya wawe katika mazingira magumu.

Hata hivyo, alisema hawawezi kuendelea kutoa huduma mpaka hapo serikali iwahakikishie inawapatia kinga.

“Kila mgonjwa anayefika hospitali hapo anatakiwa awe ndani ya neti ili asiambukize vidudu kwa wagonjwa wengine waliopo wodini, hivyo serikali inatakiwa kuhakikisha kunakuwa na neti za kutosha katika hospitali zenye wagonjwa hao,” alisema.Kadhalika, alisema serikali inatakiwa kuhakikisha kuwa elimu ya kutosha inatolewa ili jamii ielimike.

MUHAS KUFANYA UTAFITI

Katika hatua nyingine, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi cha Muhimbili (MUHAS) kipo katika mchakato wa kuanza utafiti dhidi ya ugonjwa huo ili kuishauri serikali nini cha kufanya kwa ajili ya kuisaidia jamii.

Hayo yalisemwa jana na  Kaimu Mkuu wa Makamu wa chuo hicho, Profesa Eligius Lyamuya, na kueleza kuwa kuna kikosi kazi kipo tayari na wakati wowote wataanza kufanya tafiti ya kisayansi dhidi ya ugonjwa huo.

Alisema suala hilo litaanza mapema kutokana na ukubwa wa tatizo hilo na kwamba utafiti huo wataufanya kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii, Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na manispaa kwani zinajua maeneo yaliyoathirika zaidi.

JK ATOA KAULI
RAIS Jakaya Kikwete amewaomba Watanzania kwenda kwenye hospitali na vituo vya afya kupima afya  zao wakati wanapopata dalili za malaria ili kujua kama ni homa ili wapate matibabu sahihi.

Aidha ameagiza Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuhakikisha inasambaza vifaa vya kupimia ugonjwa huo nchi nzima ili kutoa huduma haraka kwa waathirika.

Alitoa kauli hiyo jana jijini Arusha, wakati alipokuwa akizungumza na wauguzi katika siku ya maadhimisho ya Wauguzi Duniani, ambayo kitaifa ilifanyika jijini Arusha.

Alisema ugonjwa huo kwa sasa ni tishio nchini kwani kwa mara ya kwanza uliibuka mwaka 2010 na watu 30 walipata matibabu, lakini umeibuka tena Januari mwaka huu na kwamba hadi mwezi huu  369 wameugua na kati yao wawili wamepoteza maisha.
Watanzania wengi tumezoea, tunapozikia dalili za homa kama malaria tunaenda kununua dawa za malaria, lakini sasa haifai kabisa kwa sababu unaweza ukanunua ya malaria kumbe dengue, alisema..
Rais alisema wilaya inayoongoza ni Kinondoni ambayo ina wagonjwa 322,Ilala 61 na Temeke 16.Alisema vifaa vyake vya kupimia ugonjwa huo ni vichache, hivyo ni vizuri vikasambazwa kwa haraka na MSD pamoja na dawa ili kuopambana njanga hilo.

SALMA AMTEMBELEA MBUNGE

Wakati huo huo, mke wa Rais, Salma Kikwete, jana alimtembelea Mbunge wa Viti Maalum (CCM) wa Unguja Kaskazini,  Bahati Ali Abed, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Dk. Mvungi tangu Jumatano iliyopita.

Hali ya mbunge huyo inaendelea vizuri. Nimelazwa hapa tangu juzi, na nimechukuliwa damu kwa ajili ya vipimo zaidi ili kubaini kama ninaumwa homa ya dengue au la, na bado sijathibitishiwa kama naumwa homa hiyo, alisema Abed jana katika hospitali hiyo Mbunge huyo alionekana kuendelea vyema huku akiwa ameketi katika kitanda cha wagonjwa wodini.

DK. BUBERWA KUZISHWA KESHO DAR
Daktari Gilbert Buberwa ambaye alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya kudaiwa viungo vyake vya mwili kushindwa kufanyakazi kutokana na  ugonjwa huo, anatarajiwa kuzikwa  kesho Tabata Kinyerezi, Dar es Salaam.

Afisa Habari wa Hospitali ya Temeke, Joyce Msumba, alithibitisha kulazwa kwa  watumishi tisa wa hospitali hiyo wanaougua ugonjwa huo na kwamba wanaendelea vizuri na matibabu.

Alisema mbali na watumishi hao kuna watu watano ambao wamelazwa hospitali hapo kutibiwa  dengue.
Mwisho

Imeandikwa na Beatrice Shayo, Christina Mwakangale, Damian Ndelwa, Dar na Cynthia Mwilolezi, Arusha.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment