WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, May 17, 2014

HONGERA DIAMOND KWA KUTEULIWA KUWANIA TUZO ZA BET

Nyota ya Tanzania katika sanaa imepata mwangaza na msukumo mpya baada ya msanii wake mahiri, Naseeb Abdul au Diamond kuteuliwa kuwania tuzo maarufu za BET zitakazofanyika baadaye mwaka huu kule Marekani.
Tuzo hizo ambazo zilianza rasmi 2001, zinalenga katika kuwaunganisha wasanii wote wenye asili ya Afrika nchini Marekani na tangu kuanzishwa kwake zimekuwa zikiwashirikisha wasanii mbalimbali kutoka sehemu nyingi duniani ikiwamo nchi za Afrika.(Martha Magessa)
Uteuzi huu wa Diamond ambaye anashiriki kwa mara ya kwanza ni sifa kwa Tanzania na pia ukanda wa Afrika Mashariki kwa jumla.
Tunapenda kumpongeza msanii huyu kijana ambaye mwezi huu pia ametwaa tuzo saba kwenye tuzo za Kilimanjaro, jambo ambalo linaifanya nchi yetu kuingiza mshindani halisi.
Hata hivyo, Diamond ambaye anashiriki pia tuzo za MTV pamoja na zile za Kora, anachuana na wakali wengine kutoka barani Afrika kama vile, Mafikizolo (Afrika Kusini), Davido, Tiwa Savage (Nigeria) na wasanii wengine kadhaa kutoka Ghana na Togo.
Tunatambua kuwa huu ni mtihani mkubwa si kwake kama Diamond, bali kwa Tanzania na Afrika Mashariki kwa jumla, lakini tunatambua kuwa ushindi wake unamtegemea kila mmoja wetu.
Hata hivyo, imekuwa ni kama bahati mbaya kwetu sisi Watanzania kwani hatuna utamaduni wa kuwapigia kura washiriki wetu kwenye matukio mbalimbali ya kimataifa, jambo ambalo hatuna budi kulibadili sasa ili kumwezesha Diamond awe mshindi. Tumeona, huko nyuma kwa mfano kwenye shindano la Big Brother Africa, tuzo za filamu bora ya Kiafrika kwa Kiswahili zilizofanyika Nigeria mwaka huu ambako wasanii wetu waliangushwa si kwa kukosa sifa, vigezo bali kwa kukosa kura.
Hivyo, tunasema wakati ukifika, kushiriki kwetu na kupiga kura zetu kwa njia ya mtandao, bila shaka tutakuwa tumemwezesha kijana wetu huyu kushiriki, kushindana na pengine kufanya vizuri mwaka huu kwenye tuzo hizo.
Tuna imani kwamba vijana ambao ni wengi na ambao siku hizi wanaishi kwenye mitandao ya kijamii bila shaka watakuwa mabalozi wazuri wa kumwezesha Diamond kuwa mshindi na pia balozi mzuri wa nchi yetu huko Marekani.
Tunadhani, Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo na hata balozi zetu zilizoko nje pia zitashiriki katika kuhakikisha kuwa Diamond anaibuka mshindi kwani hakuna kisichowezekana chini ya jua na washindi siku zote hutengenezwa.
Inawezekana hata sisi kumtengeneza mshindi etu, ambaye ni Diamond kwani yeye ndiye pekee kutoka Tanzania, ingawa ukanda wa Afrika Mashariki unaye pia Lupita Nyong'o kutoka Kenya ambaye mapema mwaka huu alishinda tuzo za Oscars kwenye uigizaji.
Tunapenda kutoa ushauri kwa wasanii wengine wa fani mbalimbali waige kutoka kwenye mafanikio ya mwenzao huyu na kuamini kuwa inawezekana kuwa mshindi, hasa kwa kufanya kazi kwa nidhamu, kujiamini na kujituma.

source: mjengwa blog

No comments:

Post a Comment