WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, May 7, 2014

Bila Serikali ya Umoja ZNZ ni machafuko


 

Bila shaka wananchi wengi wa pande zote mbili za Muungano watakuwa wameshtushwa na kauli ya mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Salmin Awadh Salmin kwamba wawakilishi wa chama chake cha CCM wanajiandaa kuwasilisha hoja binafsi kwenye Baraza hilo ili kuwapa nafasi wananchi kuulizwa iwapo wanataka kuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) au vinginevyo.
Akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho ulioongozwa na katibu mkuu wake, Abdulrahman Kinana mwishoni mwa wiki mjini Zanzibar, Salmin alisema wajumbe hao wamefikia hatua hiyo kutokana na kile alichodai kuwa wanaona kwamba lengo na matumaini ya kuundwa kwake yamefutika. Alisema ni vyema wananchi wakaulizwa kama bado wana hamu na mfumo huo au ule wa zamani urejeshwe.
Aliwatuhumu viongozi wa CUF kwa kile alichokiita kitendo chao cha kupinga Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar. Kauli ya kiongozi huyo iliungwa mkono na katibu wa itikadi na uenezi wa CCM,Nape Nnauye ambaye alisema ni jambo muhimu kuitishwa kura ya maoni ili wananchi wapate nafasi ya kuulizwa kama wanataka mfumo wa Serikali iliyopo kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka ujao.
Awali, Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana alitumia muda mrefu kumshambulia katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad na kudai kwamba kiongozi huyo amekuwa akiwayumbisha Wazanzibari kwa kile alichokiita tabia yake ya kubadilisha ajenda za kisiasa na kutikisa misingi ya umoja wa kitaifa nchini. Alidai kwamba kiongozi huyo haeleweki na haijulikani anatafuta kitu gani licha ya kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa SUK.
CUF imepinga madai hayo na kusema wanasiasa wanaojadili suala la kuendelea au kutokuendelea na SUK wanapaswa kujiuzulu. Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Abdallah Bimani anasema viongozi hao wanakwenda kinyume na uamuzi wa vyama vyao ambao ulipitishwa na kuridhiwa na vikao vya juu, huku akisema CUF haina ajenda ya siri ya kuvunja Muungano au kuyasambaratisha mapinduzi, bali inapigania kile alichokiita Muungano wenye usawa, haki na heshima kwa kila upande wa washirika.
Tumeandika kauli za viongozi hao kwa kirefu kutokana na unyeti wa kauli zenyewe. Tumekuwa tukisema mara kwa mara kwamba sisi ni waumini wakubwa wa Muungano ambao SUK ni sehemu yake. Kwa maneno mengine, kuiyumbisha SUK ni kuuyumbisha Muungano na kuuyumbisha Muungano ni kuiyumbisha SUK. Katika hali hiyo, hatuwezi kukaa kimya pale tunapoona hatari inayoweza kusababisha nyufa katika msingi wa Muungano.
Tungependa kuwashauri viongozi wa Zanzibar kuilinda SUK kama mboni za macho yao. Wasisahau kwamba SUK ilitokana na maridhiano baina ya vyama hivyo baada ya kuwapo machafuko ya muda mrefu kutokana na siasa za visasi na utengano visiwani humo. Kutokana na ushindani mkubwa wa kisiasa uliopo kati ya vyama hivyo, amani itatamalaki pale tu vyama hivyo vitakaposhirikiana katika masuala ya msingi kama kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama ilivyo sasa.
Rai yetu kwa viongozi wa CUF na CCM ni kwamba tofauti kati yao hazitamalizika kwa kuivunja SUK, bali kwa mazungumzo na maridhiano. Kuivunja SUK ni kuwakwaza wananchi na kuirejesha Zanzibar katika machafuko na zama za giza za kulia na kusaga meno.

chanzo cha habari: mwananchi

No comments:

Post a Comment