WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, November 13, 2013

Wasifu na ari ya sengondo mvungi vilianza zamani




Je, hali yetu Tanzania itakuwaje- miaka kumi ijayo? Sharti tujifunze sana mambo yanayotokea Kongo leo. Toka alipouawa Waziri Mkuu mteule wa kwanza, Patrice Lumumba mwaka 1961, Kongo imegeuzwa makamasi na matope. Sasa hivi askari wanafanya dhambi tupu. Kuwalazimisha kina baba kulala na binti zao, wakikataa wakatolewa macho na kukatwa katwa masikio kisha wakauawa mbele ya familia zao? Askari wanaowabaka kina mama wazee na watoto wadogo wa miaka mitatu kisha wakachomeka mtutu wa bunduki ndani ya uke na kufyatua risasi!
Askari mmoja mstaafu aliyehojiwa runinga ya SKY, Jumapili iliyopita, alieleza upo ubakaji aina mbili –wa “kunajisi kwa ashki” iliyotokana na miezi mingi msituni (bila wanawake) na wa kufuata amri ya maofisa viongozi ilikuharibu motisha wa wananchi wa kawaida.
Jamii ya Kongo inaendelea kuangamia kama ilivyo Mexico.
Kuna video imesambazwa mtandaoni karibuni ikiwaonyesha wanawake wanne wa Kimeksikana: mmoja kigoli, mwingine nyanya, wa tatu na wa nne wanawake wa makamo. Wamefungwa mikono, wakavuliwa sidiria, wakapigishwa magoti na baada ya kusema majina na shughuli zao kwa woga, wakatukanwa, wakasukumwa kifudifudi kisha wakakatwakatwa, shingo, mikono kwa shoka na panga wangali hai.
Hii ni mifano ya jamii zilizovurugwavurugwa- kwa utajiri wa madini, ukorofi wa viongozi wanaoshirikiana na makampuni ya Magharibi (Kongo) na ushetani wa dawa za kulevya (Mexico) ambapo hata polisi na wanausalama ‘wanaogopa’ kufanya kazi.
Zamani sana mawe, mikuki, visu na mashoka vilitumika kuua. Huo utamaduni umeibuka tena dunia ya sasa. Ukatili umefika saa sita mchana.
Tumemwona kiongozi wa Kitanzania akivamiwa kwake na kukatwakatwa kwa mapanga. Hadi safu hii ikiandikwa, Dokta Sengondo Mvungi - mjumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba Mpya na kiongozi wa NCCR-Mageuzi alikuwa mahututi hospitali na juhudi za kumpeleka je ya nchi kwa matibabu zaidi zilikuwa zikiendelea. Tumtakie kila la kheri apone haraka...
Kabla ya kujitoma katika siasa, Sengondo Mvungi alikuwa mwanahabari. Tulianza kazi pamoja magazeti ya chama enzi hizo (TANU) -Uhuru na Mzalendo- mwaka 1976.
Mvungi alikua mchapa kazi.
Lakini takriban kila mtu pale alikua mchapakazi. Sema Mvungi alikua na ngozi na mabaka tofauti. Tuchukue mfano wa namna alivyoianza siku yake. Miye nilikua naishi Mwananyamala; yeye, Mwenge. Ni mbali sana na Barabara ya Nyerere ambayo miaka hiyo iliitwa Pugu. Ukingoni mwa barabara hii zilisimama ofisi za magazeti ya Chama na pia Redio Tanzania (RTD).
Ilikubidi upande mabasi kadhaa (yaliyoitwa UDA) hadi ofisini saa mbili na nusu asubuhi. Daladala hazikuwepo mwaka 1976, na UDA ilishindwa hata na konokono kimwendo na kiufanisi.
Ingawa baada ya muda tulipewa mikopo ya pikipiki(iliyokatwa mishaharani), wakati tunaanza kazi(tuliyoichangamkia kwa hamasa za ujana) ilibidi kuwahi. Mwenzetu Sengondo Mvungi alidamka saa kumi na moja za asubuhi akavaa nguo za mchakamchaka (bukta na fulana), mkoba mgongoni, akakimbia toka Mwenge hadi ofisi za Uhuru.
Mwaka 1976 hakukua na barabara ya mkato ya Sam Nujoma au Nelson Mandela kutokea njia ya Nyerere. Ama kupitia Kawawa na Mpiji sijui. Ilibidi akimbie hadi Magomeni, ashukie Kigogo hadi Ilala na hatimaye Pugu.
Hiyo ni alfajiri ya hatari za vibaka na mbwakoko. Lakini Mvungi kajaaliwa azma na ari. Akishafika ofisi za Uhuru atakoga kisha abadili nguo, afungue msosi alioubeba na kujisetiri.
Sikumbuki kama alikoga kwa maji ya ndoo au kama tulikua na mabafu; ila saa mbili na nusu ambazo wafanyakazi wenzake tuliingia mgodini, yeye tayari mezani kwake akisubiri wanahabari wenzake, tuingie. Kati yao – wote marehemu- Abdi Mushi (mtangazaji mashuhuri wa redio), Omar Bawazir (michezo), Costa Kumalija (mhariri mkuu), Yahya Buzaragi, John Rutayisingwa, Hannah Kasambala, John Mkamwa, nk.
Wengine walio hai ni akina Salva Rweyemamu (Ikulu), Dk Harrisson Mwakyembe (Waziri), Ndimara Tegambwage, nk.
Hapo sasa utafuata mkutano wa wanahabari kupanga kazi za siku. Utamsikia Mvungi (kama wenzake) akichangia mawazo. Hachelei kusema, haachi kucheka panapostahili. Kifupi si mwongo; si mnafiki. Jioni wanahabari tukielekea mabaa hakuwepo. Sikuwahi kumwona Mvungi ulevini.
Ndiyo kati ya mambo aliyoendelea nayo miaka iliyofuata. Nilijiuzulu 1978 nikazama ndani ya muziki na magazeti mengine; Mvungi akaelekea masomo ya juu hadi alikofikia na huo udokta wa sheria.
Alipenda kusoma ndiyo
Tulisoma wote, awali, Sekondari ya Mzumbe.
Kule alikua kiranja mkuu wa shule.
Alishangaza kwa kutokuchoka.
Kila mara anaongelea matatizo ya wanafunzi, anakutana nao, anasikiliza, anatatua na kutanzua. Kuna wakati nilimuuliza: “Hivi wewe unalala saa ngapi?”
Maana alijituma sana; hakua na uvivu na kero za vijana wa mijini, ana hulka na tabia za shamba, za wana jembe vijijini. Kama hachezi mchezo fulani (alihusudu riadha), atasoma kitabu au kusikiliza redio. Kawaida vijana Mzumbe tulipenda sana kufanya masihara na kutembelea shule za akina dada, hususan, Kilakala. Mazungumzo yatakuwa utani utani wa kirijali na mavazi. Ukiwa naye Mvungi ataongea hayo lakini utajua masikio na hisia zake zilikua kwingine. Tulimstahi na kumheshimu, tukinong’onezana, iko siku atakuja kuwa mtu wa mfano.

Takriban miaka 40 imepita toka enzi hizo.
Sasa hivi Sengondo Mvungi yu mahututi.
Tungependa kusikia kapona; ari yake ya kuishi kali. Swali muhimu la kujiuliza ni je, kiongozi wa hadhi yake alikosaje ulinzi imara?
Mwaka juzi, Dk Mvungi alifurahisha sana alipotoa kauli ya kupinga kuweka hoja ya ‘mapenzi na ndoa za jinsia moja’ katika Katiba Mpya.
Akasema kuipachika kauli hiyo ndani ya utamaduni wetu ni mchango wa udunishaji wa akili za watu. Msimamo thabiti ukizingatia Wazungu wameisimanga Afrika kufuata ‘itikadi hii’ la sivyo kunyimwa misaada. Kauli dhahiri ya ukoloni mambo leo!
Nchi yetu inasifika dunia nzima kwa uadilifu na amani. Miaka 100 sasa hatujawa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mara ya mwisho kupigana ilikua Maji -Maji dhidi ya Mjerumani 1905- 1907. Vita nje vimekua kuchangia tu ukombozi barani (Uganda, 1979 nk).
Kilichotufanya tuwe vile, ni kujaaliwa viongozi wasiochinjachinja na kuonea wananchi; ingawa hapa na pale machache yametokea. Tofauti za umaskini na utajiri zinakua haraka na wezi na majambazi wanatumia ukatili wa giza kufikia malengo. Tuombe Mungu yasigeuke kinyaa cha Kongo, Mexico na Somalia.
-Bpepe: kilimanjaro1967@hotmail.com

-Tovuti: www.freddymacha.com
source: mwananchi

No comments:

Post a Comment