WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, November 9, 2013

JK awapa vidonge Museveni,Kagame, Uhuru Kenyatta

  Atoboa kisa kisa cha Tanzania kutengwa
  Asema ni shirikisho, ardhi, ajira na uhamiaji

Rais Jakaya Kikwete, akilihutubia Bunge mjini Dodoma jana. Kulia ni Spika wa Bunge, Anne Makinda.(Picha na Selemani Mpochi)

Rais Jakaya Kikwete amewapa vidonge marais wa Kenya, Uganda na Rwanda, kwa kufanya mambo yanayoigawa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kueleza kuwa msimamo wa Tanzania ndio uliopelekea kutengwa na viongozi hao.

Hata hivyo, amesema Tanzania haina mpango wa kujitoa kwenye Jumuiya hiyo na ameahidi kuwa itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa kufanikisha malengo ya EAC.

Rais Kikwete aliyasema hayo jana bungeni mjini alipolihutubia Taifa na kuzungumza mambo mbalimbali ikiwamo operesheni tokomeza, mchakato wa Katiba mpya na msimamo wa Tanzania kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tanzania ni mwanachama mwaminifu wa EAC, kwa maana ya kutekeleza mkataba ulioanzisha jumuiya hiyo na makubaliano yaliyofikiwa kwenye vikao halali, mengine ambayo hatujayatekeleza ni kwasababu yanatukwaza na siyo kupuuza jumuiya,”| alisema Rais Kikwete.

“Tumepoteza muda mwingi na fedha nyingi kuianzisha jumuiya na tunachangia dola za Marekani milioni 12 kwa mwaka, hivyo hatuwezi hata kidogo kuidhohofisha.”

Alisema msimamo wa Tanzania uko bayana kwamba mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo, utekelezwe hatua kwa hatua, lakini baadhi ya viongozi wanataka vipengele vingine virukwe.

Alisema tatizo kubwa ni msimamo wa Tanzania kutaka masuala ya ardhi, ajira na uhamiaji, yaachiwe nchi wanachama kama ilivyopendekeza tume ya mtaalam kutoka Kenya, Amos Wako.

Tume hiyo ilikusanya maoni ya wananchi kuhusu kuharakisha kuingia kwenye shirikisho la kisiasa na masuala ambayo wanayahofia na kuonekana ardhi, uhamiaji na ajira ni hofu kwa raia wengi wakiwamo Watanzania.

Rais Kikwete alisema Tanzania pia imekuwa ikisisitiza kuwa mkataba ulioanzisha jumuiya hiyo utekelezwe hatua kwa hatua ili kuijenga kwenye msingi imara.

“Tanzania imekuwa ikiwasihi wenzetu kwamba tujenge jumuiya hii hatua kwa hatua kama tulivyokubaliana kwenye mkataba, siyo kuruka hatua. Mkataba unaelekeza kuwa tunaanza na soko la pamoja, ushuru wa forodha, umoja wa kifedha na hatimaye shirikisho la kisiasa,” alisema.

Hata hivyo, alisema baadhi ya viongozi wanataka kuharakisha kuingia kwenye shirikisho la kisiasa kabla ya kukamilisha taratibu muhimu za awali.

“Ni kweli kabisa hatukuunga mkono kuharakisha shirikisho kabla ya kukamilisha taratibu hizi za mwanzo, tulifanya hivyo kutaka shirikisho lijengwe kwenye msingi imara, yaani mtangamano wa kiuchumi, soko la pamoja, ushuru wa forodha na umoja wa kifedha...tunaamini kwamba haya ndiyo muhimu,” alisema.

“Kama mambo ya kiuchumi yakipangika vizuri tutajenga shirikisho imara. Kama hili halitafanyika kwa umakini, shirikisho litayumba au litayumbishwa na uhai wake utakuwa wa mashaka.”

Rais Kikwete aliongeza kuwa Tanzania inaamini kuwa uundaji wa shirikisho la kisiasa litakuwa rahisi kama uchumi wa jumuiya utakuwa imara, biashara ikawa nzuri, soko la pamoja likaimarika, ushuru wa forodha na umoja wa kifedha mzuri.

“Tanzania ni moja ya nchi zinazotaka hatua zote za jumuiya zitekelezwe bila kuruka moja, huu siyo msimamo wa Serikali peke yake bali wa Watanzania walio wengi,” alisema.

Rais Kikwete alisema hata tume ya Wako iliyopendekeza masuala ya ardhi yabakie kwa nchi wanachama, haikipendekeza utekelezaji wa mkataba wa EAC uruke baadhi ya hatua.

Badala yake, alisema tume ilipendekeza nchi wanachama zipunguze muda wa kutekeleza makubaliano ya mkataba na itifaki mbalimbali.

Alisema hivi sasa majadiliano yanayoendelea ni kuhusu umoja wa kifedha na katika kikao cha Wakuu wa Nchi cha Novemba 30, mwaka huu, makubaliano yanaweza kufikiwa.

“Inawezekana kama tunakubaliana itifaki ya umoja wa kifedha ikatiwa saini kwenye kikao kijacho na hatimaye wananchi wa nchi wanachama ndio watakaokubali shirikisho liwepo au lisiwepo kwa kura ya maoni,” alisema.

“Inasikitisha kuona vitendo vinavyoibua mvutano usiokuwa na sababu vinavyofanyika hivi sasa. Kama mwendo huu hautabadilika, sijui hali itakuwaje,” alisema.

Aliongeza: “Nchi yetu inapenda kuona tunakuwa na jumuiya imara na endelevu, jumuiya ambayo inanufaisha nchi zote wanachama na watu wake wananufaika nayo. Tanzania tunapata tabu kuruka hatua moja kwa sababu kufanya hivyo kutaijenga Jumuiya kwenye msingi dhaifu hivyo hatupendi ya mwaka 1977 yatokee tena.”

Rais Kikwete alifafanua kuwa: “Tanzania itaendelea kushiriki kwenye Jumuiya kwa kuzingatia matakwa ya mkataba na itifaki zake na tutafanya kila jitihada jumuiya isidhohofike...tutaendelea kukumbushana kufanya mambo yanayojenga badala ya yale yanayotugawa.”

Alisema: “Napenda kuwahakikishia kuwa hatutatoka, tupo na tutaendelea kuwepo.”

Msimamo wa Tanzania unakuja baada ya marais wa Kenya, Uganda na Rwanda, kukutana kwenye vikao kadhaa na kukubaliana mambo ambayo mengine yalishakubaliwa kwenye vikao vya nchi wanachama wa EAC.

Alisema baada ya kikao cha viongozi wakuu wa EAC cha Aprili 28 kilichofanyika Nairobi nchini Kenya, marais watatu ambao ni Uhuru Kenyatta (Kenya), Yoweri Museveni (Uganda) na Paul Kagame (Rwanda), wamekuwa wakikutana na kukubaliana mambo ambayo mengine yameamuliwa kwenye vikao vya nchi zote wanachama.

Rais Kikwete alisema katika vikao hivyo, viongozi hao wamekubaliana mambo mbalimbali yakiwamo yanayoihusu jumuiya huku wakizibagua Burundi na Tanzania, ambazo ni wanachama halali wa EAC.

Alisema viongozi hao watatu walikutana kwa nyakati tofauti kuanzia Juni 25 na 28, Agosti 28 na Oktoba 28, mwaka huu na kukubaliana mambo manane likiwamo la kuharakisha uundaji wa Shirikisho la Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na himaya moja ya ushuru wa forodha.

Alisema mambo mengine ambayo yamekubaliwa na viongozi hao ni kujenga reli ya kisasa kutoka Kenya-Bujumbura hadi Sudan Kusini, kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta Uganda na kujenga bomba la mafuta kutoka Kenya-Uganda hadi Sudan Kusini.

Makubaliano mengine ni matumizi ya vitambulisho vya taifa kwa wananchi wake, visa moja ya utalii kwa wageni wanaotembelea nchi hizo na kujenga na kuzalisha umeme kwa nchi hizo.

Alisema orodha ya mambo yaliyokubaliwa kwenye vikao hivyo imechanganya mambo akieleza kuwa yapo ambayo yanaihusu jumuiya yote na yale ambayo yalishakubaliwa kwenye vikao halali vya EAC ambayo yalihitaji utekelezaji wa kila nchi.

Akizungumzia uzalishaji na usambazaji wa umeme, Rais Kikwete alisema suala hilo lilishakubaliwa kwenye vikao vya wakuu wa nchi wanachama na mpango ni kwamba EAC iwe na hifadhi ya pamoja ya umeme na kisha nchi zitengeneze utaratibu wa kuutumia.

Alisema katika mkakati huo, kila nchi iliachiwa jukumu la kusambaza nishati hiyo kwa wananchi wake. “Mradi huu ulibuniwa na EAC, sijui wanaona tabu gani kuishirikisha Tanzania,” alisema.

Kuhusu ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda, alisema katika kikao cha mwisho cha wakuu wa nchi, Rais Museveni alieleza mpango wa nchi yake kuhusu mradi huo na kuwaalika wawekezaji kutoka nchi wananchi wenye nia ya kukijenga wafanye hivyo.

Rais Kikwete alisema ni katika hali ya kushangaza, Tanzania imewekwa kando kwenye mpango huo ambao ungezipunguzia nchi zote wanachama gharama za uagizaji mafuta kutoka Uarabuni kwa kuwa mafuta ya Sudan Kusini sasa yatasafishwa Uganda.

“Tunajiuliza au pengine hawataki kutuuzia mafuta yao?” alihoji.

Kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya-Uganda hadi Sudan Kusini, alisema halipo kwenye mkataba wala itifaki za Jumuiya na kwamba ni jambo jema ambalo hata Tanzania ingeweza kuunganishwa kwa kuwa ina mpango wa kujenga bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.

Akizungumzia makubaliano ya ujenzi wa reli ya kisasa, Rais Kikwete alisema hilo halina tatizo japokuwa upo mpango kabambe wa miundombinu wa jumuiya ukiwamo ujenzi wa reli ya kisasa, barabara na usafiri katika ziwa Victoria.

Alisema nia ya mpango huo ni kuunganisha masoko kwa nchi za Afrika Mashariki hivyo inashangaza nchi hizo kuibagua Tanzania.

Kuhusu wananchi kutumia vitambulisho vya Taifa na visa moja ya watalii, alisema jambo hilo lilishakubaliwa kwenye vikao halali vya EAC na nchi zilizokuwa tayari kuyatekeleza ziliruhusiwa kufanya hivyo.

KATIBA MPYA
Awali, Rais Kikwete alizungumzia mchakato wa Katiba Mpya na kueleza kuwa umefikia kwenye hatua nzuri na kamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba inakusudia kutoa rasimu ya pili kabla ya Desemba 15, mwaka huu.

Alisema wananchi wanategemea Bunge litunge sheria ya kura ya maoni na kuifanyia marekebisho ile ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013.

Alisema hivi sasa Serikali inatafakari utakapofanyika mkutano wa Bunge la Katiba na kwamba moja ya mapendekezo ni bungeni mjini Dodoma.

OPERESHENI TOKOMEZA
Kuhusu kampeni ya operesheni tokomeza majangili, alisema ilikuwa na lengo la kulinda rasilimali za nchi kama misitu na wanyama walio hatarini kutoweka kama tembo na faru.

Alisema kasi ya mauaji ya tembo na faru inatisha na kwamba kuisitisha ni kuwapa majangili kibali cha kuteketeza rasilimali za Taifa.

“Kasi ya mauaji ya ndovu ni kubwa sana. Katika kipindi cha kuanzia mwaka 201o hadi Septemba 2013, meno 3,899 yenye uzito wa kilo 11,212 yalikamatwa na vipande 22 vilivyochakatatwa vyenye uzito wa kilo 3,978 vilikamatwa  nchini wakati pembe zilizokamatwa nje ya nchi zenye asili ya Tanzania ni 4,692 zenye uzito wa kilo 17,797 kwa hiyo tusipochukua hatua za haraka faru na ndovu watakwisha,” alisema.

Alisema serikali imesitisha kwa muda operesheni hiyo ili kutafakari maoni ya wabunge na kutathmini operesheni ilivyoendeshwa na kwamba ikibainika kuna watumishi walikiuka maadili watachukuliwa hatua.

Hata hivyo, Rais Kikwete alisema wananchi wanapaswa kufahamu kuwa sheria ya uhifadhi inazuia kuchunga mifugo kwenye hifadhi za Taifa na kwamba wabunge wanapaswa kuwaelimisha wananchi wao.

HALI YA DRC
Kuhusu hali katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya kundi la waasi la M23 kusambaratishwa na Bgigade maalum ya Umoja wa mataifa iliyoundwa na Afrika Kusini, Tanzania na Malawi, alimppongeza Rais Joseph Kabila na wananchi wan chi hizo na kuwatakia maisha mapya ya amani.

Pia aliwapongeza wanajeshi wa Tanzania, Afrika Kusini na Malawi waliosaidia kuwasambaratisha waasi hao.

PINDA ASIFU HOTUBA
Akimshukuru Rais Kikwete, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alimpongeza rais kwa hotuba yake nzuri hasa msimamo wa Tanzania kuhusu EAC.
“Umetukonga moyo kwa sababu umeweka bayana kabisa msimamo wa Tanzania juu ya EAC hasa uliposema Tanzania ni mwanachama mwaminifu wa jumuiya, tupo na tutaendelea kuwepo,” alisema.

“Naamini wabunge watakubaliana nami kwamba kazi uliyoifanya leo (jana), ni nzuri na hata yale uliyosema ni yaa kuchomekea tu (Katiba Mpya na Operesheni tokomeza), kwetu sisi ni elimu tosha.”

WABUNGE WAMPONGEZA RAIS
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema amependa msimamo wa Rais Kikwete aliouotoa kwa niaba ya Taifa kuhusiana na ushiriki wa Tanzania katika EAC.

Alisema msimamo huo wa Rais Kikwete umekuwa tofauti na kauli, ambazo zimekuwa zikitolewa katika siku za hivi karibuni na baadhi ya mawaziri zikiashiria kwamba Serikali ya Tanzania ina mwelekeo wa kujitoa katika jumuiya hiyo.

Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, naye pia aliungana na Mbowe kusifu hotuba hiyo ya Rais Kikwete na kusema katika hali iliyofikia hafikirii kama kulikuwa kunahitaji msuluhishi katika mvutano uliopo baina ya nchi hizo, kama ilivyokuwa ikielezwa na baadhi ya watu.

Mbunge wa Chonga (CUF), Haroub Mohammed Shamis, alisema hotuba ya Rais Kikwete ni nzuri kwani imetoa mwelekeo kwa Watanzania kuhusiana na EAC, kwani amekuwa muwazi juu ya hilo kwamba, Tanzania haina nia mbaya, bali muhimu ni mkataba husika ufuatwe.

Mbunge wa Namtumbo (CCM), Vita Kawawa, alisema hotuba ya Rais Kikwete imesisimua, kwani ameonyesha jinsi gani Tanzania inavyofuata sheria na itifaki zote za EAC.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment