WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, November 18, 2013

Dk Mvungi azikwa

Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi alizikwa jana kijijini kwake, Chanjale, Kisangara Juu katika mazishi ambayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wajumbe wa tume hiyo, vyama vya siasa na wananchi.

Akizungumza katika mazishi hayo, Askofu Rogath Kimario wa Kanisa Katoliki Dayosisi ya Same alisema tukio la kushambuliwa lililosababisha kifo chake halikuwa la ujambazi.(P.T)

Akizungumza wakati wa ibada ya mazishi iliyofanyika Kanisa la Moyo Mtakatifu Yesu la Parokia ya Kisangara Juu iliyopo Chanjale, ambayo pia ilihudhuriwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu; Askofu wa Jimbo la Mbulu, Beatus Kinyaiya na Askofu Damiani Ngalu wa Geita wote wa Kanisa Katoliki, Askofu Kimario alisema waliofanya mauaji hayo ni wauaji wa kimtandao na kuitaka Serikali kutoa majibu sahihi kuhusiana na tukio hilo badala ya majibu mepesi yasiyofanyiwa utafiti.

Kauli hiyo ilionekana kujibu ile ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kuwa mauaji ya Dk Mvungi ni tukio la ujambazi.

"Eti waliotenda hilo ni majambazi, nani kasema ni majambazi?... Ni research (utafiti) ipi ama upelelezi gani umefanyika?... Hawa ni wauaji wa kimtandao, kuna maswali mengi yasiyo na majibu," alisema Askofu Kimario na kuongeza:

"Ni kifo cha fedheha hata kuku hauawi hivyo. Watu wana uchungu, kila mtu ana maswali ambayo hayana majibu... kwa nini auawe? Kwani alikuwa tajiri hata majambazi watake pesa?"

Askofu Kimario alisema Watanzania wanamlilia Dk Mvungi na familia yake inamlilia kama ambavyo wasomi na wanazuoni wanavyomlilia hivyo Serikali inawajibika kutoa majibu sahihi juu ya kifo chake.

"Damu yake inadai Watanzania tujiulize Dk Mvungi yuko wapi... wanausalama ndugu yetu yupo wapi? Wasomi mlikuja hapa kwenye harusi yake mkafurahi naye leo mnatuletea marehemu," alisema.

Askofu huyo alisema kinachofanya taifa kubwa kama Marekani liheshimike ni wepesi wake wa kuwaeleza wananchi wake ukweli na kutaka Watanzania wasiridhike na majibu mepesi ya kifo hicho.

"Tusiridhike na majibu rahisi. Marekani wanafanya uchunguzi mpaka ukweli unajulikana kama ilivyokuwa kwa Osama Bin Laden... ilichukua muda mrefu lakini ukweli ulijulikana," alisema.

Akitoa salamu za Serikali katika mazishi hayo, Waziri Mkuu Pinda alisema Serikali inafanya jitihada kuwakamata waliohusika na mauaji hayo.

"Ni kweli Serikali inafanya jitihada za kuwakamata waliofanya tukio hili la ovyo lakini hata tukiwapeleka mahakamani wakahukumiwa kunyongwa hiyo si mbadala wa Dk Mvungi," alisema.

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema watamuenzi Dk Mvungi kwa kukamilisha kazi ya kutunga Katiba Mpya yenye masilahi ya nchi.

"Tunawaomba wananchi wote tumuenzi Dk Mvungi kwa kuangalia mapendekezo ya Katiba kwa masilahi ya Taifa ili tupate Katiba ya maridhiano," alisema.

Mwenyekiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alisema kifo cha Dk Mvungi kimewaumiza lakini akasisitiza kuwa tukio hilo halitarudisha nyuma harakati za kupigania haki ya Watanzania.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria mazishi hayo ni Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira, Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki.

Wengine waliohudhuria ibada hiyo ni Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba.

Chanzo:Mwananchi

No comments:

Post a Comment