WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, November 13, 2013

JK arudisha zawadi ya dhahabu

  Aagiza isaidie watoto yatima

Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete, ameirudishia kampuni ya Nyamigogo Grand Vezir Holdings ya mkoani Geita zawadi ya gram 227 za dhahabu safi aliyopewa na kampuni hiyo na kuelekeza itumike kuwasaidia yatima.   
Rais Kikwete alitoa maelekezo hayo juzi baada ya kukabidhiwa zawadi ya dhahabu hiyo wakati wa sherehe ya kuzindua mgodi wa uchenjuaji dhahabu wa kampuni hiyo nje kidogo ya mji mdogo wa Kharuma ambako ndiko makao makuu ya wilaya mpya ya Nyang’hwale, mkoani Geita.
Gram hizo 227 za dhahabu ambazo ni sawa na aunzi nane, zina thamani ya Sh. milioni 16 kwa bei ya sasa ya soko la dhahabu duniani.
Baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo, Rais Kikwete aliuliza: “Sasa nifanye nini na zawadi hii? Nawarudishieni, iuzeni popote mnakotaka na fedha zitakayopatikana tutawapa watoto yatima.”
Akizungumza na wananchi katika mgodi huo, Rais Kikwete aliupongeza uongozi wa mgodi huo akisema kuwa umeongeza thamani ya dhahabu na ya maisha ya wananchi katika eneo hilo.
Hata hivyo, Rais Kikwete aliushauri uongozi wa mgodi huo kufanya jitihada za kuboresha teknolojia inayotumika.

“Mmefanya vizuri sana na mgodi huu ni mradi wa maana sana kwa kuongeza thamani ya dhahabu na kuboresha maisha ya wananchi katika eneo hili. Ubunifu huu unastahili pongezi,” alisema.

Aliongeza: “Lakini lazima tuboreshe teknolojia. Teknolojia inayotumika kwenye mgodi huu bado ni ya zamani kidogo.

Hii ni sawa na hadithi ya mtu mwenye chongo katika jamii ya vipofu watupu. Yeye anaonekana kama mfalme.” Mgodi wa Nyamigogo ambao ni marudio kwa maana ya kwamba unazalisha dhahabu kutokana na mchanga ambao huko nyuma umepata kufuliwa na kutoa dhahabu, ulianzishwa mwaka 2011 na mpaka sasa zimewekezwa kiasi cha Sh. bilioni 1.6 katika uendelezaji wake.   

Risala ya uongozi wa mgodi huo ilisema mgodi huo unaozalisha kiasi cha gram kati ya 500 na 600 kwa mwezi, umeajiri wafanyakazi  45 wakiwamo wanawake 10.

Tangu kuanzishwa kwake, mgodi huo umekuwa unaunga mkono shughuli za jamii inayouzunguka ikiwa ni pamoja na kujenga zahanati na madarasa ya shule katika vijiji viwili.

Rais Kikwete alizindua mgodi huo ikiwa sehemu ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika ziara yake rasmi ya kikazi katika Mkoa wa Geita, moja ya mikoa minne ambayo aliianzisha mwaka jana. Mikoa mingine ni Simiyu, Njombe na Katavi.
Ziara hiyo ya siku tano ilimalizika jana.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment