WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, November 9, 2013

Warioba: Kabla ya kuumizwa Dk. Mvungi niliomba ulinzi

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema wiki moja kabla ya kushambuliwa kwa mjumbe wa Tume hiyo Dk. Sengondo Mvungi, ofisi yake iliomba kuimarishiwa ulinzi zaidi kufuatia matukio yaliyokuwa yakijitokeza ambayo hata hivyo hakuyataja.
Jaji Warioba aliyasema hayo katika mahojiano maalum na NIPASHE Jumamosi kuhusu suala la ulinzi dhidi ya makamishna ndani ya Tume hiyo. Alisema suala la ulinzi kwa makamishna wa Tume hiyo ni wa kawaida.

“Sisi ndani ya tume ni raia wa Tanzania hivyo ulinzi wetu ni wa kawaida kama ilivyo kwa watumishi wengine wa serikali,” alisema na kuongeza kuwa inapotokea wanahitaji ulinzi serikali imekuwa ikitekeleza hilo bila tatizo.

“Kipindi tulipokuwa tunaenda mikoani katika shughuli zetu za Tume tulipewa ulinzi pale tulipokuwa tunahitaji, ndio maana mara zote ninapotoa taarifa za tume nilikuwa naishukuru serikali kwa ulinzi wake kwetu,” alisema.

Jaji Warioba alisema wiki moja kabla ya tukio la Dk. Mvungi kuvamiwa, walilazimika kuomba kuimarishiwa ulinzi kwenye Ofisi ya Tume kufuatia matukio mbalimbali yaliyojitokeza.

“Yapo matukio ambayo yalikuwa yakijitokeza hivyo tuliviarifu vyombo vya dola na viliweza kutuimarishia ulinzi hapa ofisini kwetu, kwa hivyo pale tulipokuwa tuna mashaka tulikuwa tunawaarifu kama wafanyavyo raia wengine kusikilizwa,” alisema.
Bila kuyataja matukio hayo, alisema wanaishukuru serikali kwa kukubali ombi lao na kuimarisha ulinzi huo.

“Kama umefika katika ofisi zetu siku za nyuma na ndani ya wiki hii utagundua tofauti, ulinzi umeimarishwa zaidi,” alisema.

Mwandishi alipouliza kuhusu ulinzi wa Makamishna wa Tume nyakati zote hata wawapo nyumbani, Jaji Warioba alijibu kuwa ulikuwa hauna tofauti na ule wa watumishi wengine wa serikali.

“Nimekwambia sisi ni watumishi wa serikali, kwa hiyo ulinzi wetu hauna tofauti, kama linatokea jambo basi tunatoa taarifa kwenye chombo husika kwa hatua zaidi, hatuna ulinzi special,” alisema
Akijibu uvumi uliozagaa kuhusu safari ya Dk Mvungi ilihairishwa siku ya Jumatano usiku kutokana na deni la matibabu ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai, DCI, Robert Manumba linalodaiwa serikali ya Tanzania na hospitali aliyotibiwa alipopelekwa Afrika ya Kusini, Jaji Warioba alisema hilo hafahamu.

Taarifa za ndani ambazo NIPASHE Jumamosi ilidokezwa ni kuwa safari ya Dk. Mvungi iliahirishwa siku hiyo na kufanyika siku iliyofuata baada hospitali hiyo kukumbushia deni la matibabu la Manumba ambaye mapema mwaka huu alipelekwa huko kwa matibabu.

Kutokana na deni hilo, taarifa hizo zilieleza kuwa, Tume ya Katiba ililazimika kutoa fedha ambazo siku iliyofuata Dk. Mvungi alisafirishwa.
Jaji Warioba alisema wao wanachoangalia ni afya ya Dk Mvungi na ndio maana wametoa fedha hizo.

“Sisi tumeamua kumsafirisha kwa sababu tulitaka iwe hivyo tena kwa haraka iwezekanavyo,” alisisitiza.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, alipoulizwa alikanusha uvumi huo na kusema kuwa hayo ni maneno ya mtaani na kwamba habari ya Manumba ni ya zamani.

“Unataka habari za Dk. Mvungi au za Manumba ambazo ni za zamani, kwanza zinakusaidia nini hizo kama ni mgonjwa ‘Dk. Mvungi amesafirishwa’ kila kitu kilichokuwa tatizo tume-clear (tumekamilisha) leo (alhamisi) na ameenda kutibiwa,” alisema. 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment