WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, November 10, 2013

Sumaye amhusisha Lowassa na uongoSumaye amhusisha Lowassa na uongo

WAZIRI Mkuu wa Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, amemtaja mwenzake aliyemfuata baada ya kuondoka katika wadhifa huo, Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa kuhusika kutoa taarifa za uongo, alizodai kuwa zinalenga kumsaidia kujisafisha.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam Jumanne wiki hii, Sumaye alidai Lowassa alisema uongo kwamba ni yeye pekee aliyefanikisha mradi wa maji wa Ziwa Victoria, Kanda ya Ziwa na kwamba mawaziri wengine wote walimpinga.

Akinukuu gazeti moja la kila siku, Sumaye alisema; “Liliandika kuwa siri ya mradi wa kuvuta maji Ziwa Victoria yafichuliwa na katika maelezo yake, mtoa habari alisema ni mawaziri wawili tu waliouunga mkono mradi huo na wengine wote waliupinga.

“Najua mhusika (Lowassa) ameutumia sana mradi huu kisiasa na sisi wengine tumenyamaza japo ukweli tunaujua sana. Lakini hili la mradi ametukanyaga vidole wengine na kutupia miiba na magogo kwenye njia yetu wengine, amenilazimisha niseme ukweli kuhusu mradi huu kwa sababu mimi ndiye niliyekuwa waziri mkuu na mradi umetekelezwa chini ya uangalizi wangu kama kiongozi na msimamizi mkuu wa utekelezaji wa shughuli zote za serikali.

“Pamoja na kwamba hilo lililoelezwa ni uongo mkavu, mhusika  kama waziri mwandamizi wakati huo na sasa kama anayewinda nafasi kubwa katika nchi hakutegemewa kutoa siri za baraza la mawaziri; labda amediriki kufanya hivyo kwa sababu anajua anayoyasema siyo ya kweli vinginevyo ni kosa la jinai na akishitakiwa anafungwa jela.”

Sumaye ambaye katika mazungumzo yake hayo na waandishi wa habari alianza kwa kumuunga mkono Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kuhusu vitendo vya rushwa katika siasa za ndani ya CCM, alisema kuna mbinu mbalimbali zinazotumika na wahusika wanaotafuta nafasi mbalimbali za uongozi kufanikisha malengo yao.

Alisema ziko mbinu nzuri za kistaarabu na ziko mbinu chafu kama za kupakazana matope (character assassinations).

“Mbinu ambazo ni chafu ni pale mhusika anatengeneza mbinu ama za kuwamaliza wengine wanaodhaniwa kuwa washindani wake baadaye au kuwawekea vikwazo katika mbinu zao za kujisafishia njia.… huyo ama anachimba mitaro kwenye barabara wanazofyeka wenzake au anatupia miiba na magogo yanayotoka kwake na kuyatupia kwa wenzake ili mradi wenzake wakwame wakati ukiwadia,” alisema.
 Mradi  wa maji wa Ziwa Victoria

Akizungumzia kwa kina kuhusu mradi wa maji wa Ziwa Victoria, Sumaye alisema mradi huo ni mradi wa serikali na haukuwa wa mtu.

“Ni kweli kwa mkataba uliokuwepo wa miaka ya 1952 au 1953 nchi za huku juu mito ya Nile inapoanzia na inakopitia hazikutakiwa zitumie maji ya Mto Nile ili nchi za Misri na Sudan zisiathirike. Nchi hizi Tanzania ikiwamo, ziliona makubaliano hayo siyo sahihi na tulianza kudai mabadiliko ya sheria hiyo.

“Jambo hili lilishughulikiwa mwanzo na Waziri Dk. Pius Ng’wandu na baadaye likakamilishwa na ‘Agreed Minutes’ zilizoweka msingi wa makubaliano baina ya nchi hizo kusainiwa na nchi kumi na kwa Tanzania aliyesaini ambaye kwa bahati nzuri alikuwa ndiye mwenyekiti wa baraza hilo la nchi kumi alikuwa Musa Nkhangaa aliyekuwa Waziri wa maji wakati huo,” alisema.

Alisema katika kusukuma jambo hilo yeye binafsi akiwa Waziri Mkuu aliwahi kukutana Addis Ababa na marehemu Meles Zenawi, aliyekuwa waziri mkuu wa Ethiopia kabla ya serikali ya Uholanzi kusaidia kuandika mradi.

Alisema baada ya Waziri Nkhangaa kutembelea chanzo cha kuchukulia maji cha Smith Sound na kuona mradi unawezekana, Rais Benjamin Mkapa alishauriwa kuwa mradi huo unawezekana na kutekeleza ahadi ya kufikisha maji kutoka Ziwa Victoria mkoani Shinyanga.

“Matatizo ya maji Shinyanga yalivyotutesa isingewezekana baraza la mawaziri kuupinga mradi huo na mimi nisingeupinga kabisa maana wakati mji wa Shinyanga ukikosa maji nilikuwa silali usingizi. Jambo ambalo ni kweli ni kuwa mradi huo uliiva wakati Lowassa akiwa waziri wa maji na ameusimamia hadi ukakamilika kama ambavyo angeusimamia waziri mwingine wa maji,” alisema.

Alisema  hakuna waziri mwenye uwezo wa kutekeleza mradi kama baraza la mawaziri likiukataa na kuhoji: “Fedha atapata wapi za kuendesha mradi huo? Pili mradi wowote ni wa serikali na unatengenezwa na wizara husika. Katika wizara wanaofanya kazi sana ni wataalamu chini ya katibu mkuu. Pamoja na kuwa sisi wanasiasa tunapenda kubeba sifa zote mambo yakienda vizuri na kuwatupia lawama wataalamu yakienda vibaya, ni vema tujue tunafanya kama timu moja na mwenye serikali ni moja tu yaani Rais.”

Alisisitiza kwamba uamuzi wake wa kuzungumzia kauli ya Lowassa si kuingilia mambo ya watu wengine bali anapoguswa hatoweza kunyamaza.

“Lakini pia ni wajibu wangu kueleza ukweli pale ukweli unapopotoshwa kwa makusudi. Nataka niwaase hasa wanasiasa wenzangu kuwa tuwatendee Watanzania haki kwa kuwapa ukweli mtupu na tusiwape uwongo uliopakwa utamu wa ukweli juu kumbe ndani ni machungu ya uwongo,” alisema.

Akizungumzia rushwa na ufisadi, alisema ukiona mtu anatoa rushwa ujue kuna anayedhulumika na kuumia na hiyo rushwa yako.

“Unapofanya ufisadi kwa mradi wa serikali unaliumiza taifa katika siku zijazo kwa kuipiga kiharusi cha uchumi na huduma kwa jamii. Na unapouza dawa za kulevya wewe ni muuaji wa taifa kwa sababu unaangamiza vijana wa taifa hili ambao ndiyo nguvu kazi yetu tunayoitegemea,” alisema.

Akimpongeza Rais Kikwete kuhusiana na rushwa ndani ya CCM, alisema ni imani yake kwamba waliokabidhiwa dhamana hiyo hawatalionea haya na hawataangalia sura ya mhusika wakati wa kuchukua hatua.
“Wanachama wa CCM na wananchi wote tumepata matumaini mapya kwamba kauli ya mwenyekiti wa chama tawala haitapotelea hewani bali itatekezwa na italeta mabadiliko makubwa katika vita dhidi ya rushwa nchini. Ndugu mwenyekiti wangu mimi nakupongeza sana sana kwa kukemea rushwa na ninakuunga mkono katika vita hii na ninaamini unajua kuwa mimi ni askari wako mojawapo wa mstari wa mbele,” alisema.

Kauli hiyo ya Sumaye inajitokeza katika wakati ambao vuguvugu la kulenga kuwania uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ukipamba moto, huku rafu zikiwamo za matumizi ya rushwa zikiripotiwa mara kwa mara kufanya na baadhi ya makundi ya wasaka urais.

No comments:

Post a Comment