WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, September 7, 2013

Uraia pacha ni muhimu, tusidanganyike




NIANZE kwa kumpongeza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kwa jitihada zake kubwa kupigania kupitishwa kwa sheria ya uraia pacha.
Pamoja na upinzani mkubwa katika suala hilo, Waziri Membe ameendelea kusimama kidete na majuzi tu aliendeleza jitihada hizo katika mkutano wa rasimu ya Katiba Mpya uliofanyika katika wizara yake.
Binafsi, ninaelewa mantiki ya hoja za wanaopinga uraia pacha. Hata hivyo, mantiki hizo zimepitwa na wakati. Kimsingi, moja ya sababu za kuharamisha uraia pacha ni siasa yetu ya nje katika zama za Ujamaa. Wakati huo, nchi yetu ilielemea upande wa Wakomunisti, na kwa hakika enzi hizo za kinachofahamika kama Vita Baridi zilitawaliwa sana na matishio ya kiusalama. Kwa wakati huo, raia mwenye uraia wa nchi mbili angeweza kuonekana kama kibaraka wa nchi za Magharibi na hivyo kuwapo kwa uwezekano wa raia huyo kutumiwa kuihujumu nchi.
Kwa sasa hakuna hoja nzito dhidi ya uraia pacha. Kama ni suala la utiifu kwa nchi (hoja ambayo imekuwa ikipigiwa mstari kwa nguvu na wapinzani wa uraia pacha), sote tunafahamu jinsi nchi yetu inavyohujumiwa na kutafunwa na Watanzania wenzetu ambao naamini baadhi yao hawajawahi kutoka nje ya mipaka ya nchi yetu.
Kadhalika, baada ya kuua na kuzika itikadi ya Ujamaa, tumeshuhudia sio tu wageni kutoka nchi mbalimbali wakija huko nyumbani kwa minajili ya uwekezaji au ajira bali pia watawala wetu wamekuwa wakizunguka kila kona ya dunia kuhamasisha wageni kuja huko nyumbani, si kutalii bali kuifanya Tanzania kuwa nyumbani kwao kwingine (second home).
Sasa kama ni ruksa kwa wageni ambao hawana ‘udugu’ na nchi yetu kuwa na haki ya kuifanya Tanzania kuwa nyumbani kwao, kwa nini isiwe hivyo kwa Watanzania ambao kwa sababu moja au nyingine walilazimika kuchukua uraia wa nchi nyingine?
Na kwa vile kwa mujibu wa sheria zilizopo, Mtanzania akichukua uraia wa nchi nyingine anapoteza uraia wa Tanzania, basi pengine kuwahukumu waliolazimika kuukana uraia wa Tanzania ili wapate uraia wa nchi nyingine sio kuwatendea haki.
Ninatambua kunaweza kuwa na hoja “kwa nini utake uraia wa nchi nyingine ilhali tayari una uraia wako wa kuzaliwa (wa Tanzania)?” Jibu jepesi ni kwamba sio kila aliyeamua kuchukua uraia wa nchi nyingine (na hivyo kulazimika kuukana uraia wa Tanzania) alifanya hivyo kwa kupenda. Kuna baadhi ya wenzetu waliolazimika kutafuta hifadhi ya ukimbizi nje ya nchi yetu na hatimaye kupatiwa uraia wa nchi zilizowapa hifadhi (mfano ni kundi la Wazanzibari waliopewa hifadhi Uingereza kutokana na vurugu za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000)
Lakini kubwa zaidi katika suala hili la uraia pacha ni ukweli kwamba kumlazimisha Mtanzania anayetaka uraia wa nchi nyingine akane uraia wa nchi yetu ni kinyume cha haki za binadamu za raia huyo kwa sababu kimsingi ni Mtanzania kwa kuzaliwa. Huwezi kumnyima mtu haki kwa sababu za kufikirika kama hizo za kukosa utiifu kwa nchi. Kama ni hivyo basi hata wanasiasa wanapogombea kutuongoza katika chaguzi tungelazimika kuwanyima haki ya kuongoza kwa hisia tu ya “kuna wanasiasa wasio na utiifu kwa nchi yetu.”
Majuzi nimemsikia Mzee Kingunge Ngombale Mwiru akizungumzia suala la uraia pacha. Binafsi nadhani japo tunaaswa kusikiliza ushauri wa wazee wetu lakini sababu za kibaiolojia zinaweza kutufundisha kuwa uwezo wa kiakili huathiriwa na umri. Tumeshasikia habari za wazee “wanaozeeka vibaya,” na japo ninamheshimu Mzee Kingunge lakini nadhani anazeeka vibaya.
Nisingependa kumjadili Kingunge kwa undani katika makala hii bali binafsi nimekuwa nikimwona mzee huyo kama mmoja wa watu waliomsaliti Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, walishirikiana katika jitihada za kujenga jamii ya usawa na haki lakini akamsaliti kwa kuungana na makundi ya kifisadi yaliyoifikisha Tanzania ilipo sasa. Ushauri wangu mwepesi ni kumpuuza Mzee Kingunge kwani mitizamo yake iliyopitwa na wakati haina nafasi katika Tanzania tunayoihitaji sasa.
Kimsingi, suala la Mtanzania kuishi nje ya nchi yake linaambatana na hisia za kibaguzi kwa namna fulani. Majuzi tu niliingia katika malumbano na ndugu yangu mmoja kuhusu mustakabali wa taifa nililolizungumzia. Alidai kuwa kwa vile nipo mbali na huko nyumbani (Tanzania) basi nitakuwa “mtu wa kuambiwa tu” (kana kwamba kila tunachoambiwa si sahihi).
Kuna kasumba ya kibaguzi iliyoshamiri kwa muda mrefu kwa baadhi ya wenzetu huko nyumbani kutoangalia Watanzania tulio nje ya nchi yetu kama “Watanzania vipande” (yaani si Watanzania kamili). Japo ni ruhusa kwao kubobea kwenye uchambuzi wa Ligi Kuu ya England kana kwamba wanaishi hapa, ni “kosa la jinai” kwa sie tulio mbali na nyumbani kuzungumzia masuala yanayoigusa Tanzania yetu. Hawa ni wabaguzi tu wasiotaka kuelewa kuwa kwa sie wengine uwepo wetu huku unapelekea “kukabwa koo” na swali “Kwa nini iwe hivi kwa wenzetu lakini kwetu sivyo?”
Sina maana kila linalofanyika hapa Uingereza, kwa mfano, ni jema na ningetamani liwe hivyo huko nyumbani. Lakini kuna maswali kadhaa, hususan katika mfumo wa utawala unaotanguliza maslahi ya taifa badala ya watu binafsi au itikadi za kisiasa, au kufanikiwa kutenganisha taasisi na mtu binafsi. Kadhalika, wenzetu hawa licha ya wengi wao kutokuwa wacha Mungu wamefanikiwa sana kutilia mkazo maadili katika uongozi, huduma kwa umma na utawala bora kwa ujumla.
Ninaamini kuna wazalendo wengi tu Watanzania waliolazimika kuchukua uraia wa nchi nyingine lakini nafsi na akili zao zipo huko nyumbani. Na hiyo ni kuweka kando ukweli kwamba wengi wetu bado tuna ndugu, jamaa na marafiki huko nyumbani. Kuwanyima Watanzania hawa haki ya kushiriki katika ujenzi wa Taifa letu ‘changa’ (na sasa kushiriki katika jitihada za kupigania uhuru wa pili dhidi ya maadui wa nchi yetu kama vile ufisadi) ni kutowatendea haki.
Ninatambua kuwa baadhi ya wasomaji watahusisha mtizamo wangu katika suala la uraia pacha na ukweli kuwa nami ni miongoni mwa Watanzania walio nje, lakini ukweli ni kwamba hakuna sababu japo moja ya msingi ya kuwabagua Watanzania wenzetu, iwe ni kwa waliochukua uraia wa nje au kwa sababu nyingine yoyote ile. Ubaguzi ni suala lisilokubalika.
Nihitimishe makala hii kwa kutoa wito kwa Watanzania wenzangu kuunga mkono jitihada za Waziri Membe katika suala la uraia pacha, huku nikitegemea kuwa Katiba Mpya itatambua umuhimu wa suala hilo na hatimaye kuliruhusu. Umoja na nguvu.

www. raiamwema.co.tz: Evarist Chahali

No comments:

Post a Comment