WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, September 12, 2013

JK katika mtihani wa Katiba Mpya


“Muswada umepitishwa na wabunge wa CCM kwa asilimia 80, sidhani kama hii ni sawa katika hatua muhimu kama hii na haitoi picha kamili ya mwelekeo chanya wa kupata katiba stahiki.” Dk Hellen
Share
Dar na Zanzibar. Wakati Rais Jakaya Kikwete akisubiriwa asaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa 2013 ili kuwa sheria kamili, wasomi, wanasiasa na wanaharakati wamemshauri asifanye hivyo, wakisema itapatikana Katiba Mpya isiyo na tija.
Wananchi hao kutoka Tanzania Bara na Zanzibar walisema kwa nyakati tofauti kuwa, Rais Kikwete anatakiwa kutumia busara ya kushauriana na kupata maoni ya watu wa kada mbalimbali ili kujua nini kifanyike, kabla ya kuamua kusaini muswada huo.
Mjadala wa muswada huo uliopitishwa Ijumaa iliyopita na wabunge wengi wakiwa wa CCM, ulizua tafrani bungeni iliyosababisha Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) kutolewa nje na askari. Katika tafrani hiyo, baadhi ya wabunge wa upinzani walirushiana makonde na maofisa usalama, huku wabunge wote wa upinzani, isipokuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, wakiususia.
Wapinzani walisema Serikali iliubadili kwa nguvu muswada huo kwa kuondoa maoni muhimu ya wadau, pia walilalamikia kitendo cha wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge kutokwenda Zanzibar kuchukua maoni ya upande huo wa muungano.
Wasomi
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Gaudence Mpangala alisema mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya ulikuwa ukienda vizuri... “Lakini umebadilika vibaya, tena katika kipindi muhimu. Kupitishwa kwa muswada na kusubiri saini ya Rais kunaweza kuleta Katiba Mpya, ikawa siyo ile ambayo Watanzania wanaitarajia.” Alishauri busara itumike kabla ya kusainiwa kuwa sheria kamili.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tunguu Zanzibar, Ali Uki alisema hakuna haja ya muswada kukimbiliwa kusainiwa kwani katiba ni mali ya wananchi na kuupitisha ili uwe sheria bila kuyashirikisha makundi mengine, kutaendeleza malalamiko na kurudisha nyuma malengo ya kupatikana kwake. Uki alisema upo wasiwasi kwamba Katiba Mpya itatokana na utashi wa kisiasa badala ya matakwa ya wananchi, jambo ambalo alisema linaweza kuathiri malengo ya kuandikwa kwake.
“Utashi wa vyama umeanza kujitokeza, huku chama kimoja kikiwa na uwakilishi mkubwa kwenye Bunge hilo, chama kimoja kina uwakilishi wa asilimia 72 katika Bunge la Katiba,” alisema Uki.
Alikosoa Kifungu cha 8 na Kifungu kidogo cha 4 na 5 cha muswada huo kwamba vina kasoro kwa kuruhusu wabunge wa Bunge la Katiba kufanya uamuzi kwa wingi wa kura badala ya kutumika utaratibu wa theluthi mbili kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.
Profesa mwingine wa UDSM, Chris Peter Maina alisema ikiwa kuna nia njema ya kupata Katiba bora, lazima suala la uwiano wa idadi ya wabunge katika Bunge la Katiba litazamwe upya.
“Rasimu ya pili ikishatolewa na kukabidhiwa kwa Bunge la Katiba, kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ndiyo itakuwa imekwisha. Sasa inakuwaje Bunge linajadili Rasimu ya Katiba huku waliyoiandaa hawapo, hiki kitu kinashangaza,” alisema Profesa Maina.
Mhadhiri Mwandamizi wa chuo hicho, Dk Frank Tilly alisema hakuna umuhimu wa kukimbiza muswada kutiwa saini wakati kuna mambo mengi ya msingi ambayo hayajapatiwa ufumbuzi... “Watanzania hawajakubaliana kwa pamoja, ili jambo liwe zuri ni lazima pande mbili au zaidi zenye masilahi na kitu husika zikubaliane, sasa hilo halijafanyika tunakimbilia wapi?” alihoji.

Mhadhiri wa UDSM, Bashiru Ally alisema mchakato mzima wa Katiba umeshaingia doa kwa kupitishwa muswada unaolalamikiwa na kwamba manung’uniko ya wananchi hayajajibiwa.
Alisema busara zisipotumika, itapatikana Katiba isiyokuwa na uhalali wa kisiasa... “Nasema hivi kwa sababu wanasiasa hawajakubaliana katika kupitisha sheria itakayounda Bunge la Katiba”.
Vyama vya kiraia
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, Hassan Nassor Moyo alisema Rais anapaswa kutafakari kwa umakini kabla ya kusaini muswada huo na kuwa sheria mpya kwa kuwa bado kuna manung’uniko.
“Hakuna mantiki ya kuupitisha muswada ukawe sheria wakati kuna manung’uniko. Wakati umefika misimamo ya vyama kuwekwa kando ili malengo yenye manufaa na tija yaweze kufikiwa kutokana na mahitaji ya wananchi.”
Moyo alisema ushirikishwaji wa Wazanzibari ulikuwa finyu kwani waliopata fursa ya kutoa maoni yao walikuwa ni viongozi wa Serikali pekee.
“Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umetokana na washirika wawili, Zanzibar si mtoto wa kambo, ni mshirika na mdau mkuu katika kupata Muungano uliopo,” alisema Mzee Moyo.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema kitendo cha kupitishwa muswada wenye kasoro ni wazi kuwa kitazalisha Katiba isiyo na tija kwa taifa.
“Muswada umepitishwa na wabunge wa CCM kwa asilimia 80, sidhani kama hii ni sawa katika hatua muhimu kama hii na haitoi picha kamili ya mwelekeo chanya wa kupata katiba stahiki,” alisema Dk Bisimba.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alisema: “Ukipitisha sheria kinyemela maana yake ni kwamba unataka ifanye kazi kinyume na matakwa ya watu wengi, jambo ambalo ni hatari kiuchumi na kielimu.”
Alisema Rais Kikwete anatakiwa kutumia busara katika suala hilo, kwa maelezo kuwa, amebakiza muda mfupi kumaliza kipindi chake cha utawala, hivyo aache Katiba yenye tija kwa Watanzania.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Nicolaus Mgaya alisema: “Ikiwezekana muswada uliopitishwa usisainiwe na urejeshwe bungeni na kupitiwa upya ikiwa ni pamoja na pande zote mbili za Muungano kutoa maoni sambamba na kurekebishwa kwa kasoro zilizopo.”

Alisema watu wataondoka lakini Tanzania itaendelea kuwapo, hivyo ni jambo la busara kama ikipatikana Katiba itakayokuwa na masilahi kwa wakati huu na ujao.
Wanasiasa
Katibu Mkuu wa TADEA, Juma Ali Khatib alisema muundo wa Bunge la Katiba ndio unaozua malalamiko kutokana na wanasiasa kupewa nafasi kubwa, jambo ambalo alisema linaweza kutanguliza dhima ya kisiasa na kuweka kando masilahi ya kitaifa na utaifa.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema kitendo cha Zanzibar kutoshirikishwa ni kosa kwani Katiba hiyo ni ya Jamhuri ya Muungano... “Namshauri Rais asisaini muswada huu kwani utakuwa ni majanga. Namshauri akutane na watu walioonyesha wasiwasi na sheria hiyo ili kusikiliza mawazo yao, huenda wakamshauri jambo la msingi la kufanya na iwapo atasaini bila kufanya hivyo mchakato mzima hautakuwa wa taifa, bali wa CCM.”

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment