WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, September 7, 2013

Kuku tuliowafungulia asubuhi ndio hawa wanarudi



INAWEZEKANA kwamba sasa watu wengi zaidi wanatambua yale yaliyokuwa yakisemwa huku yakibezwa, na wanaona yale waliyokuwa wakiambiwa waone huku wakikataa kuona, japo wanayo macho.
Tumekuwa na tabia, kwa muda mrefu hadi sasa ni utamaduni, kwamba tunaposikia jambo lisilotupendeza tunaziba masikio na tunapoonyeshwa kitu kisichotufurahisha tunafumba macho. Tunasahau kwamba kuziba masikio au kufumba macho hakulifanyi jambo hilo na wala hakusababishi kitu hicho kutoweka.
Baadhi yetu tumekuwa tukionya kwamba mambo tunayoyafanya leo yanazo athari zake kesho na keshokutwa, na kwamba kila tendo lina tendo-rejea (For every action there is a reaction), lakini bado tunao watu miongoni mwetu wanaoelekea kuamini kwamba wanaweza kutenda watakavyo na zisitokee athari zozote.
Mifano ni mingi, lakini inatosha kuchukua miwili au mitatu. Hivi sasa Tanzania imejijengea sifa ya hovyo, sifa ya aibu, ya kuwa njia ya mpito (transit) ya dawa za kulevya ziendazo huko ziendako. Inaumiza roho kila mara unapopata habari kwamba Mtanzania mwingine amekamatwa akivuka mpaka wa nchi nyingine akiwa amebeba mihadarati.
Kama lilivyosema gazeti moja nchini, Watanzania wamegeuka ‘punda’ wa kubeba mizigo ya mihadarati ya watu wengine (siku hizi wabebaji hao wanaitwa makontena kwa sababu ya kubeba dawa hizo tumboni). Maana yake ni kwamba mizigo wanayobeba si ya kwao, bali wao ni wapagazi wa kuwabebea hao wenye mizigo yao.
Kwa kuangalia tatizo hili juu-juu, bila uchambuzi kidogo tunawaona vijana hawa waliogeuka kuwa punda kama wana wapotevu waliokosa maadili na waliowaasi wazazi wao na wanaolisaliti taifa lao.
Aidha, tumekuwa na janga la baadhi yetu kuwaua na kuwakata viungo wenzetu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kiasi kwamba dunia nzima sifa moja ya nchi yetu ni kwamba albino hawana usalama hapa. Watu wengi wanaotupenda wamesumbuliwa na jambo hili, wakijiuliza ni jinsi gani nchi iliyowahi kuwa na sifa ya utu, uungwana na ukarimu inaweza kugeuka na kuwa na jamii ya nyang’au kama hawa.
Najaribu kuzichukua sifa hizi mbili za aibu kwa pamoja, huku nikijaribu kudadisi chimbuko lake na jinsi zilivyojitokeza kuwa ni sifa za taifa letu. Sifa hizi mbili ni matokeo ya kile nilichokiita tendo-rejea, ‘reaction.’ Jamii inayoachana na maadili ya uongofu, ikashindwa kuwafundisha watoto wake jinsi ya kuishi katika uadilifu; jamii inayoonyesha dhahiri kwamba utajiri kwa njia yoyote ile ni jambo jema na kwamba ukiiba si tatizo bali tatizo ni kukamatwa; jamii inayotukuza wezi na matapeli, badala ya kuwasweka jela inawachagua na kuwatuma bungeni, jamii hiyo inalea punda wa mizigo ya mihadarati.
Hali kadhalika, tunapopuuza elimu yakinifu ya watu wetu na watoto wetu wakafundishwa kushinda mitihani bila kupata maarifa; tunapokubali kwamba ‘multiple choice’ ndio wa kupima uwezo wa mwanafunzi, na tunapowaachia watu wachache wafanye wanachotaka na elimu ya watoto wetu bila kuwasaili, tunakuza u-mbumbumbu ambao baadaye unajitokeza katika medani zote za maisha ya jamii yetu, kutoka ngazi za chini hadi za juu.
U-mbumbumbu huu ndio huo unaotufanya tukubali kwamba kuna mzee mmoja Loliondo anayetibu maradhi halaiki kwa kikombe kimoja na taifa zima likaonekana liko mbugani kwenda ‘kunywa kikombe.’ Watu wanakufa kwa kuacha dawa zao, hospitali zinaachia wagonjwa waende kupata ‘kikombe,’ sote tunaonekana wajinga, lakini mwisho wa siku hakuna mtu wa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu hicho ‘kikombe’ na tunajifanya hamnazo, kama vile hakuna kilichotokea. Tunajibaraguza, hatuoni haya!
Ujuha huu ni ujuha unaoambukiza, haubakii kwa mtu mmoja mmoja, kwa sababu unayo misingi yake katika elimu ya ujuha, na hii maana yake ni kwamba mbegu zake zimesambazwa shamba zima.
Sasa, ujuha unaotokana na elimu ya uzuzu inapokutana na mmomonyoko wa maadili unaotokana na kufundishana wizi, tunakuwa tumefanikisha kupata muungano baina ya punda wa kubeba mihadarati na dalali wa kuchinja albino. Hawa wawili, baba yao ni ujinga na mama yao ni mmomonyoko wa maadili. Mkunga aliyewazalisha ni uongozi mbovu.
Nataka nieleweke kwamba nasema uongozi mbovu ni wetu sote: Tunajiongoza vibaya, tunaongozana vibaya na tunawaongoza vibaya hao tunaotakiwa kuwaongoza. Binafsi hupenda kusema kwamba kiongozi si yule aliyakabidhiwa ofisi kwani huyo ni ofisa tu; kiongozi ni yule anayeonyesha njia. Katika mambo haya ninayoyajadili sote ni viongozi, na sote tumewasaliti watu wetu.
Maofisa waliokabidhiwa ofisi hizi tumewachagua wenyewe, na kwa sababu ofisi hizo wanazozishikilia ni sisi tuliowakabidhi, kwa kawaida ni juu yetu kuwaandama ili waziendeshe vyema kwa maslahi yetu. Kwa kweli, ni sisi tunaotakiwa kubeba lawama iwapo tumewakabidhi ofisi zetu watu wasio na uwezo wa kutufanyia kazi. 
Iwapo sisi ni wakweli katika nafsi zetu, iwapo tutajichunguza kwa undani na kujisaili kwa dhati, tutagundua kwamba masuala mazito na yenye umuhimu mkubwa tunayachukulia kipuuzi, tunayachezea na kuyatomasatomasa na kuyatania, kama vile hatujui hatari zinazotokana na upuuzi huo. Halafu yanapotulipukia, ni kama tunashangaa.
Tunaposhangaa tunataharuki na kuchukua hatua za kuchekesha – kama tunaweza kucheka -- ambazo hazina chembe ya kuonyesha kwamba tumetambua chanzo cha tatizo. Hatua tunazochukua ni za kujishikiza tu, kama vile tunasubiri kitu fulani kitokee ndipo tuokoke, na kwa jinsi hii tunasogea kwa mtindo wa siku hadi siku, mpaka hapo itakapotokea gharika.
Nakumbushia tena, kila tendo lina tendo-rejea, na Waingereza wana msemo kuhusu “chickens coming home to roost,” ambao maana yake ni kwamba kuku unaowafungulia asubuhi usiwashangae ukiwaona wanarudi nyumbani jioni; ni wako hao, na wanakuja kulala.
Naangalia kila upande, kila idara, kila medani, kila eneo la maisha (siasa, uchumi, elimu, afya, kilimo, michezo, utamaduni, maadili) na ninaona kuku wengi wanarudi, mmoja baada ya mwingine, na nikiwaangalia vizuri na kuchunguza rangi za manyoya yao, naona ni wale wale kuku wetu tuliowafungulia asubuhi. Sasa tunashangaa nini?

No comments:

Post a Comment